Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Mwiba mdogo-1

Kutana na binti mrembo, mpole anayeamua kujivika roho ya kinyama na kuwaua watu maarufu mmoja baada ya mwingine. Ni nini kimemsukuma kufanya hayo, endelea kufuatilia hadithi hi na Mtunzi Ally Mbetu...

Dakika tano baada ya mkuu wa upelelezi Juma Shila kuingia ofisini, kabla ya kuanza kazi alipitia magazeti ya siku ile, ili ajue mpaka yeye anapanda kitandani jana yake kulikuwa kumetokea kitu gani ambacho yeye hakukijua.

Habari kuu za wiki ile zilikuwa juu ya kutekwa kwa mwanamke mwenye ualbino mjamzito kwenye Super Market ya Mlimani City.

Ulikuwa mkasa mzito uliotikisa nchi baada ya serikali kudhibiti utekwaji kukatwa viungo na mauaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi. Lilikuwa tukio la kushtukiza sana baada ya utulivu kwa kuyadhibiti matukio yale.

Hivyo ili kurudisha imani kwa wananchi, waziri wa mambo ya ndani alimpa mkuu wa upelelezi nchini saa 24 kuhakikisha yule mwanamke mjamzito anapatikana akiwa mzima wa afya njema.

Vijana wake wa kazi wakiongozwa na mpelelezi makini Maliki na jopo lake walimuahidi kumtafuta kabla siku ya pili hakujapambazuka kumtia mikononi, japokuwa walikuwa wametoka kwenye kazi nzito ya kuziba kashfa iliyotaka kuichafua nchi kwa kuuawa kwa mhariri mtendaji wa Gazeti la Ukweli Mtupu, pia kutekwa kwa waziri mkuu mstaafu.

Tukio lile liliipasua nchi vipande viwili, kila mtu akisema lake, lawama zote zilikuwa kwa serikali iliyokuwa madarakani kutaka kuficha uchafu wake, baada ya kufichua njama mbaya za kuichafua nchi na kufanikiwa kumrudisha waziri mkuu akiwa mzima wa afya njema.

Kutokana na kufanya kazi iliyotukuka, mkuu wa nchi aliwaandalia tafrija kwa ajili ya kuwapongeza vijana wake. Lakini wakati wakijiandaa kukutana na mkuu wa nchi likatokea tukio zito la kutekwa mwanamke huyo albino mjamzito katika supermarket, na wao kuingia mara moja kazini kumtafuta bila kujali uchovu wao.

Walikuwa hawajapumzika vizuri kutoka kwenye kazi nzito ya kumrudisha waziri mkuu mstaafu aliyetekwa na watu waliotaka kuipaka nchi matope, vijana wa Kitanzania wenye uchungu na nchi waliojitoa muhanga kwa ajili ya nchi yao.

Kikao kizito na vijana wake kilichoisha usiku wa manane bila fununu zozote za kupatikana kwa mwanamke albino, kilizidi kumweka kwenye wakati mgumu na kufanya siku ikatike bila kupata lepe la usingizi.

“Mkuu kikombe cha kahawa ili kupunguza usingizi,” alikuwa sauti ya sekretari wake, sajenti Suzy huku akiweka kikombe cha kahawa juu ya meza baada ya kumkuta mkuu wake ameshikilia gazeti huku amefumba macho.

“Ooh! Suzy asante mama labda kichwa kitachangamka, maana nakiona kizito kama nimebeba kontena,” Juma Shila alisema huku akiweka gazeti pembeni na kunyanyua kikombe cha kahawa na kupiga funda tatu za haraka haraka na kukiteremsha kikombe chini, huku akili yake ikichangamka kidogo.

Akiwa anapeleka mkono kwenye gazeti ili aendelee kusoma na kujua waandishi nao wana taarifa gani ambazo zinaweza kuwapa mwanga kidogo baada ya wao kutoka kapa, simu yake ya mezani iliita. Hakurudisha mkono, alibadilisha mwelekeo, badala ya kwenda kwenye gazeti ulikwenda kwenye mkono wa simu na kuunyanyua:

“Haloo.”

“Haloo,” ilikuwa sauti ya kike.

“Ndiyo, nikusaidie nini?”

“Naitwa mtoto wa marehemu.”

“Sawa, nikusaidie nini?” wazo la mkuu lilikuwa huenda kuna mtu ana taarifa za kuonekana mwanamke albino aliyetekwa.

“Nimepiga kukupa taarifa.”

“Sawa, taarifa gani?”

“Ya mauaji ya Mchungaji Samwel.”

“Mchungaji wa kanisa gani na mauaji yametokea wapi?”

“Mchungaji wa Kanisa la Chemchem ya Faraja lililopo Mbezi Kibanda cha Mkaa amefia ofisini mwake, hakuna anayejua mauaji haya ila mimi na wewe ni mtu wa pili.”

“Ooh! Kanisa hilo nalijua hata Mchungaji namjua, nini sababu ya kifo chake.”

“Hiyo siyo juu yangu, nimetoa taarifa kama raia mwema.”

“Wewe ni muumini?”

“Hapana.”

“We ni nani sasa?”

“Mzee Shila, hata kama nitakuwa muumini ndiyo itarudisha uhai wa marehemu?” Sauti upande wa pili iliuliza.

“Umelijuaje jina langu?”

“Mkuu hayo si muhimu, wahi kuchukua mwili wa marehemu mkauhifadhi, mkichelewa utaharibika vibaya, sumu iliyomuua mkichelewa kuchukua mwili, inaozesha haraka.”

“Wewe up...” hakumalizia sentensi yake, simu upande wa pili ilikatwa, alipopiga simu ambayo ilionesha imepigiwa kwenye kibanda ilionesha upande wa pili haipo sehemu yake sahihi, ilikuwa imeachwa pembeni ya simu.

Bila kupoteza muda aliwachukua vijana wake wanne na kuelekea Mbezi Kibanda cha Mkaa. Walipofika eneo la Kanisa la Chemchem ya Faraja hali waliyoikuta ilikuwa ya utulivu.

Baadhi ya wahudumu walikuwa bize na shughuli zao za kila siku, kanisa lile lilikuwa moja ya makanisa maarufu kwa huduma zake za kiroho zilizovuta watu wengi wa dini tofauti.

Pamoja na huduma nzuri za kiroho zilizokuwa zikitolewa, ndilo kanisa lililokuwa kubwa jijini Dar, lenye ghorofa tatu na zote hujaa waumini siku za maombi.

Mchungaji Samwel alikuwa mmoja wa viongozi wa kidini wenye ukwasi wa pesa. Alimiliki ndege na boti binafsi.

Alikuwa ni mtu aliyefahamika kona yote ya nchi kwa huduma zake za kiroho mpaka nje ya nchi.

Alikuwa mtu mnyenyekevu, mpole mwenye hofu ya Mungu, kila aliyekwenda kwake kweli alimwagikiwa na chemchem ya faraja iliyofanya wengi kurudiwa na faraja baada ya kukatishwa tamaa na shetani. Mkuu wa upelelezi Juma Shila alipoteremka kwenye gari aliingiwa na hofu kwa kuamini huenda mtoa taarifa alimchezea akili na kuwaza zaidi huenda watu waliomteka mwanamke albino waliamua kuwachanganya akili.

Lakini kwa vile alikuwa amefika pale alitakiwa kufika kabisa ili ajue kuna ukweli gani katika taarifa alizopewa na mtoa taarifa.

Alielekea ofisi ya Mchungaji Samweli iliyokuwa na hadhi ya juu ya vioo vitupu vyenye ‘tinted’ ambavyo ukiwa nje huoni ndani.

Alitembea taratibu huku akisoma mazingira yale ambayo hayakuonesha tukio lolote la kushtusha, kila mtu alikuwa akiendelea na majukumu yake.

Alipofika kwa sekretari wa Mchungaji alikaribishwa kwa heshima zote:

“Karibu mkuu.”

“Asante binti yangu.”

“Karibu sana.”

“Asante, baba Mchungaji tumemkuta?”

“Yupo, japokuwa amesema asisumbuliwe mpaka atakaponiita,” alijibu yule binti ambaye alionekana alikuwa akiandika taarifa za kanisa.

“Nina shida naye ya muhimu sana.”

“Kwani hamuwezi kuacha maagizo ili akitoka nimpe, siku zote akiwa kwenye maombi hataki mtu amsumbue.”

“Binti unanijua mimi?” Shila alimuuliza kwa sauti kali kidogo.

“Sasa mkuu nitafan...”

“Nina uwezo wa kukusweka ndani na huyo mchungaji wako, haya nenda kamwambie serikali ipo nje,” mkuu Shila alisema kwa sauti ya mamlaka.

Yule binti mrembo aliyekuwa amevalia sketi ya bluu na blauzi ya bluu bahari huku nywele zake kazibana kwa juu na kumfanya kazidi kupendeza, alinyanyuka na kuelekea ndani ya ofisi ya mchungaji.

Alipofika aligonga hodi zaidi ya mara tano bila majibu na kuamini mchungaji alikuwa kwenye maombi mazito. Alirudi kutoa taarifa kuwa mchungaji yupo kwenye maombi labda wamsubiri amalize maombi.

“Kwani hayo maombi hutumia muda gani?”

“Saa moja au mbili.”

“Mara ya mwisho kuwasiliana na bosi wako ni muda gani?”

“Mmh! Saa tatu sasa.”

“Kwani maombi yana siku maalumu?”

“Ndiyo.”

“Leo ni moja ya siku zake?”

“Hapana.”

“Sasa kwa nini useme yupo kwenye maombi?”

“Mkuu kama kuna dharura hufanya siku yoyote ikiwa kuzuia tatizo zito aliloliona likija mbele.”

“Mmh! Sawa, basi akimaliza mwambie Mr Shila alifika hivyo anitafute haraka.”

“Sawa, poleni kwa usumbufu.”

“Asante,” Shila aligeuka na kutoka nje huku akiamini kuna mtu anamchezea akili.

Alijikuta akijiuliza huyo mtu anafanya vile kwa ajili gani, lakini aliamini kupitia mamlaka ya mawasiliano TCRA kujua nani anamchezea akili ili amtafute na kumshikisha adabu.

Baada ya kutoka nje ya kanisa alitembea taratibu huku akiyahamisha mawazo yake na kuyarudisha kwenye tukio zito la kutekwa mwanamke albino mwenye ujauzito na uzito wa kujua amepelekwa wapi.

Aliingia kwenye gari baada ya kufunguliwa mlango na dereva wake, wakati anafunga mkanda ili gari liondoke warudi ofisini simu yake ya mkononi iliita.

Itaendelea...