Wazazi CCM waahirisha sherehe kufuatia zuio la mikutano ya hadhara
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 27, 2026 kuhusu kuahirishwa kwa Wiki ya Wazazi iliyokuwa ifanyike Julai 4, 2026 mkoani Mwanza, kufuatia zuio la Serikali la mikutano ya kisiasa. Picha na Rachel Chibwete.
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kutangaza kuwa kuanzia Juni 27, 2026, Jeshi la Polisi halitatoa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa hadi hapo itakapotolewa maelekezo mengine.
Dodoma. Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetangaza kuahirisha sherehe za Wiki ya Wazazi Taifa 2026 zilizokuwa zifanyike Julai 4, 2026 jijini Mwanza, hadi itakapotoa taarifa nyingine.
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumamosi, Juni 27, 2026 na Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya hiyo, Fadhili Maganya, baada ya Serikali kutangaza kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Maganya amesema tarehe mpya ya sherehe hizo itatangazwa baadaye baada ya hali kuruhusu.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, kutangaza kuwa kuanzia Juni 27, 2026, Jeshi la Polisi halitatoa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa hadi hapo itakapotolewa maelekezo mengine.
Kauli hiyo ilitolewa kufuatia hoja ya Mbunge wa Dodoma Mjini, Paschal Chinyele, aliyeitaka Serikali kueleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya taarifa za baadhi ya watu wanaohamasisha maandamano.
Maganya amesema sherehe hizo zilikuwa zifanyike kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM na maandalizi yalikuwa yamekamilika, huku taarifa zikiwa tayari zimeshawafikia wanachama, viongozi na wananchi.
Amesema baadhi ya viongozi na wanachama walikuwa tayari wameanza safari kuelekea Mwanza kushiriki katika sherehe hizo, hivyo kuomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na mabadiliko hayo.
Aidha, amewahakikishia wanachama na wadau wote waliochangia maandalizi kuwa michango yao itaendelea kuhifadhiwa na kutumika mara baada ya kutangazwa kwa ratiba mpya ya sherehe hizo.
“Tunapenda kutumia fursa hii kuwataarifu wanachama wetu, viongozi na wananchi wote, hususan wa Jiji la Mwanza, kwamba sherehe hizi zimeahirishwa hadi hapo tutakapowaarifu tena,” amesema Maganya.