Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira atoboa siri uteuzi wa Dk Nchimbi, Makonda CCM

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Stephen Wasira (kushoto) akifanyiwa mahojiano na mwandishi mwandamizi wa Mwananchi, Elias Msuya, yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Loveness Bernard

Dar es Salaam. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira amevitaka vyama vya siasa kushiriki kwenye michakato ya maridhiano ili kutibu misukosuko ya kisiasa kati kati ya upinzani na chama tawala.

Kauli ya Wasira imekuja wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakitangaza kwa nyakati tofauti kutokuwa na imani na vikao vya maridhiano na CCM, vilivyodumu kwa zaidi ya mwaka tangu mwaka 2022.

Akizungumza juzi katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaam, Wasira alirejea historia ya vyama vya siasa nchini, akisema CCM iliruhusu mfumo wa vyama vingi licha ya asilimia 80 ya Watanzania kutaka mfumo wa chama kimoja.

“Wakati ule wananchi walisema wanataka mfumo wa chama kimoja kwa asilimia 80 na asilimia 20 walitaka vyama vingi.

“Rais (Ally Hassan) Mwinyi alitokana na chama kimoja na mshauri wake Julius Nyerere ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa chama hicho. Kwa hiyo wangeweza kusema, hawa wamesema chama kimoja, si basi? Lakini wakasema hapana,” alisema.

Akifafanua zaidi, alisema licha ya uchaguzi wa mwaka 1995 kuwa na upinzani mkali, aliyekuwa Rais wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alimshinda mpinzani wake wa karibu Augustine Mrema (NCCR Mageuzi).

Mwalimu alitoa mchango wake katika hilo, maana aliona chama kikipoteza nchi na hakuna chama mbadala ambacho kimejizatiti basi tulikuwa tunaingia kwenye tatizo,” alisema.

Hata hivyo, alisema ilipofika mwaka 2010 ndipo misukosuko ya kisiasa upande wa Bara ilianza wakati Rais mstaafu Jakaya Kikwete akigombea mara ya pili.

“Mwaka 2010 kulikuwa na kamsukosuko katika uchaguzi, wakati huo Dk Wilbrod Slaa aligombea urais (kupitia Chadema) dhidi ya Kikwete. Nadhani kuna watu walitaka tuwe na rais mbadala na Dk Slaa alikuwa na mvuto wake,” alisema.

Aliendelea, “Kuanzia mwaka 2010 kulikuwa na msukosuko katika siasa zetu, nadhani ni baada ya Chadema kushindwa uchaguzi, wakaanzisha Operesheni Sangara Kanda ya Ziwa, sijui kwa nini wanapapenda kule.

“Kuna wakati pia waliandamana mkoani Arusha hadi watu wakafariki na pia kukatokea mauaji ya (Daudi) Mwangosi mkoani Iringa, yote hayo yalikuwa ni matatizo ya vyama kutoelewana. Hivi ukiwa na vyama vingi unagombana tu? Mbona waliotufundisha demokrasia hawagombani?” alihoji.

Kutokana na operesheni za Chadema, Wasira wakati huo akiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Uratibu) anasema walifanya maridhiano.

“Jakaya alikuwa fimbo akakaa nao Ikulu, ilikuwa ni jitihada tu ya kuleta makubaliano,” alisema.

Kwa upande mwingine, Wasira alisema CCM ilipata msukosuko mwaka 2015 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuhamia Chadema na kugombea urais.

“Huwezi kusema ule ni msukosuko mdogo kwa sababu Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa zamani na (Fredrick) Sumaye naye akatoka akamfuata, kwa hiyo kukawa na mawaziri wakuu wawili wametoka, lakini Rais (John) Magufuli akashinda kwa asilimia 58,” alisema.

Alisema hata hivyo, Hayati Rais Magufuli hakuwa akipenda mijadala kama mtangulizi wake, bali aliwadhibiti wapinzani.

“Akawaambia hakuna kufanya mikutano ya hadhara, ingawa sheria iliwaruhusu, magazeti nayo yalikuwa yanaandika lakini walikuwa wanafuta, wakiona italeta shida,” alisema.


Samia na maridhiano

Kwa mujibu wa Wasira, baada ya Rais Samia kuingia madarakani kufuatia kifo cha Rais Magufuli, aliona maridhiano yanaweza kuleta umoja kuliko mapambano.

“Akafungua nchi kiuchumi, akasema ndani ataleta madhiriano baina ya vyama na wananchi, vyombo vya habari vinajua vikaruhusiwa zaidi katika uhuru, wananchi waliokuwa wakiogopa kusema wakaanza kusema kwa sauti,” alisema.

Alisema ili kufikia lengo hilo, ndipo alikuja na 4R, ambazo ni Reconciliation (maridhano), Resilience (uvumilivu), Reform (Mageuzi), rebuild (kujenga upya) akitafuta maridhiano na wapinzani.

“Mtu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa Freeman Mbowe tena akitokea jela. Alipokwenda Ubelgiji akakutana na Tundu Lissu. Amefanya hayo yote kuonyesha mkono wa maridhiano.

“Alikaribishwa na Bawacha (Baraza la Wanawake wa Chadema) walikuwa na sherehe zao, akaenda. Kuwa na vyama vingi si chuki, mnabishana kwa hoja mkimaliza basi,” alisema.

Alipoulizwa kama maridhiano yaliyoanzishwa na Rais Samia yamefanikiwa, Wasira alisema, “mimi nasema yamefanikiwa, kwa kiasi gani nakuachia uweke asilimia.”


Uteuzi wa Nchimbi, Makonda

Oktoba 2023, CCM ilimteua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo akichukua nafasi iliyoachwa na Sofia Mjema.

Wiki iliyopita, Halmashauri Kuu ya CCM iliyoketi Zanzibar ilimteua Balozi Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu akichukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu Novemba 30, 2023.

Mabadiliko hayo yameipa sura mpya CCM kuelekea kwenye chaguzi za Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2025.

Akiyazungumzia mabadiliko hayo, Wasira alisema chama hicho kinaendana na mazingira.

“CCM ni chama cha siasa na chama hakiwezi kuwa rigid (kuganda), lazima kiwe flexible (kinyumbulike), lazima kitazame hali ya mambo na hasa chama cha siasa kinachotarajia kutimiza miaka 47 mwezi ujao lazima kifanye mabadiliko kulingana na wakati, vinginevyo kitapitwa na wakati,” alisema.

Alisema Makonda na Nchimbi wote ni makada waliopikwa kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM).

“Makonda aliwahi kugombea umakamu mwenyekiti wa jumuiya hiyo, aliposhindwa Rais Kikwete akamteua kuwa Mkuu wa Wilaya (Kinondoni), akaja akakutana na (Rais John) Magufuli, akambeba akamfanya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akamwongezea wasifu.

Hata hivyo, alisema mwaka 2020 Makonda aligombea ubunge Kigamboni, lakini alishindwa kwenye ngazi ya chama.

“Kwa hiyo Makonda hakufukuzwa na Magufuli, Mama Samia amemkuta Makonda akiwa akiba. Sasa katika ‘assessment’ (tathmini) za chama chetu, unahitaji mtu chakaramu kama Makonda kushughulika na uenezi, hakuna sababu kwa nini usimchukue,” alisema.

Alitoa mfano wa ziara ya Makonda mikoa ya Kanda ya Ziwa akisema amekiamsha chama hicho.

Kuhusu Dk Nchimbi alisema alianzia kwenye ngazi ya chipukizi na alipotoka akawa mwenyekiti wa Taifa UVCCM akiwa pia mjumbe wa Kamati kuu. “Chama kinataka mtu aliye na uzoefu wa Serikali, yule amekuwa naibu waziri wa wizara tatu, na Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Habari.

Alisema pia Dk Nchimbi amekuwa balozi na aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya kule Bunda mkoani Mara.

“CCM tunahitaji watu wenye misimamo ambao wanaweza kusimamia wanachokiamini mpaka watakaposhawishiwa vinginevyo.

“Kama alivyosema mwenyewe pale Zanzibar, sio ndumilakuwili. Mwanasiasa lazima uwe na msimamo na uutetee,” alisema.

Wasira ni nani?

Stephen Masato Wasira ni kada mkongwe wa CCM aliyezaliwa mwaka 1945 akishika nyadhifa ndani ya chama hicho na serikalini.

Alianza safari ya siasa tangu awamu ya kwanza ya Julius Nyerere, akigombea ubunge katika jimbo la Bunda na aliwahi kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa.

Katika awamu ya pili ya Rais Ally Hassan Mwinyi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.

Wakati wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji na baadaye kuhamihishiwa Wizara ya Kilimo, Usalama wa Chakula na Ushirika kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Februari 12, 2008.

Novemba 24, 2010 aliteuliwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu.

Kwa sasa Wasira ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na pia amewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu.

Kielimu, Wasira ana Shahada ya sanaa katika uchumi na uhusiano wa kimataifa (American University in Washington), Shahada ya uzamili ya uchumi na Shahada ya uzamili ya utawala wa umma kutoka chuo hicho.