Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira afichua sababu ya CCM kujifanyia tathmini

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira akizungumza alipokutana na viongozi wa CCM katika wilaya za Buhigwe na Kasulu pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, akiwa katika ziara ya kichama jana Ijumaa Mei 15, 2026.

Muktasari:

  • Katika maelezo yake, Wasira amesisitiza, uongozi unahitaji uwezo, maadili na uelewa, huku akiwataka wananchi kuwa makini na vyama vinavyodai kuleta maendeleo bila ajenda zilizo wazi.

Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kuagiza chama kujifanyia tathmini unalenga kuboresha uongozi na kuhakikisha changamoto za wananchi zinashughulikiwa ipasavyo.

Wasira amesema katika kuelekea uchaguzi mkuu wa CCM, ni muhimu kwa wanachama na viongozi kujipima kabla ya kuomba nafasi za uongozi ili kuhakikisha wanakidhi vigezo, ikiwemo uadilifu na uwezo wa kiutendaji.

Amesema hayo jana, Mei 15, 2026, mkoani Kigoma alipokutana na viongozi wa CCM katika wilaya za Buhigwe na Kasulu pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, akiwa katika ziara ya kichama.

Katika maelezo yake, Wasira amesisitiza umuhimu wa kuzingatia Katiba, kanuni na miongozo ya CCM, akibainisha kuwa uongozi bora unapatikana kwa kufuata misingi iliyowekwa na chama.

Amesema baadhi ya changamoto ndani ya chama zinatokana na wanachama na viongozi kupotoka njia kuu na, badala yake, kufuata tabia zinazokinzana na taratibu za chama.

“Tunataka kurudi njia kuu ya chama. Chama hiki kina katiba, kanuni na miongozo inayoelekeza kila kitu kuanzia sifa za mwanachama hadi masharti ya uongozi,” amesema.

Wasira ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kuwa na maadili na msimamo thabiti, huku akisisitiza kuwa kiongozi anayeyumba kimtazamo hawezi kukisaidia chama kufikia malengo yake.

Amesema uongozi ni jukumu linalohitaji uwezo na uelewa wa kutosha, na si jambo la kujaribiwa bila maandalizi.

“Kama unataka kuwa kiongozi, omba nafasi unayoweza kuimudu kwa wakati huo. Uongozi si utajiri, ni uwezo na uelewa,” amesema.

Amefafanua kuwa uamuzi wa kufanya tathmini ya chama umetokana na maazimio ya NEC iliyokutana hivi karibuni jijini Dodoma, na ilikubalika tathmini hiyo ifanyike kuanzia ngazi ya matawi hadi taifa ili kubaini na kurekebisha upungufu.

Amesema tathmini hiyo inalenga kujenga chama imara zaidi, chenye uwezo wa kujisahihisha na kujiboresha pale kinapokosea.

Katika hatua nyingine, Wasira amewataka wananchi kutoshawishika na vyama vya siasa vinavyodai kuwa na ajenda za kuleta maendeleo, huku akidai kuwa baadhi yake vinaweza kuwa na misukumo ya nje isiyo na maslahi kwa Taifa.

Amesema Watanzania wanapaswa kuwa makini na viongozi wanaoibuka na ahadi zisizo wazi, akisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi dhidi ya uhitaji wa mataifa ya nje.