Wananchi, wasomi wakoleza mjadala uongezwaji majimbo

Muktasari:
- Mei 12, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza majimbo mapya manane ya uchaguzi katika utekelezaji wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Dar es Salaam. Wananchi na wasomi wamekoleza mjadala wenye mitazo tofauti kuhusu nyongeza ya majimbo mapya manane yaliyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), baadhi wakisema hatua hiyo inakwenda kuongeza mzigo kwa walipakodi.
Pia wapo waliopongeza uamuzi huo, wakisema utawezesha wabunge kuwafikia wananchi kwa urahisi na kuchukua kero zao.
Mei 12, 2025 Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele alitangaza mgawanyo wa majimbo mapya uliosababisha kuzaliwa kwa majimbo manane ya uchaguzi na kufikisha majimbo 272, Tanzania Bara na Zanzibar.
Majimbo yaliyogawanywa ni Ukonga, ambalo kuzaa Kivule, Mbagala limezaa Chamazi, Dodoma Mjini limezaa Mtumba wakati Jimbo la Mbeya Mjini limezaa Uyole na Bariadi limezaa jimbo la Bariadi Mjini.
Mengine ni Jimbo la Busanda mkoani Geita ambalo limezaa Katoro, Chato limezaa Chato Kusini na Solwa la Mkoa wa Shinyanga, limemegwa na kuanzishwa Jimbo la Itwangi
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, vigezo vinne vilivyozingatiwa katika mgawanyo huo ni kwa Jimbo la Mjini liwe na idadi ya watu 600,000 na watu 400,000 kwa vijijini.
Akizungumza katika mjadala wa mtandaoni, X-Space, uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mada isemayo ‘Je, mgawanyo wa majimbo una tija kwa wananchi? Jumatano, Mei 14, 2025, Mwandishi mwandamizi wa siasa wa Mwananchi, Peter Elias amesema ugawaji wa majimbo lazima uakisi kiwango cha uchumi uliopo ili kuepuka kuwabebesha mzigo wananchi wanaolipa kodi.
“Wabunge wanapoongezeka na gharama za stahiki zao zinaongezeka na mzigo huo unaenda moja kwa moja kwa wananchi wanaolipa kodi wa kawaida,” amesema akichokoza mjadala huoulioendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Maoni ya Peter yameungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Christomus ambaye amesema akiangalia kwa kina ugawaji majimbo hayo INEC imekinzana na vigezo ilivyoviweka yenyewe.
Akitolea mfano idadi ya watu kama kigezo cha kugawanya jimbo, amesema kuna baadhi ya majimbo kama Arusha yana watu wengi zaidi ya 600,000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 lakini halijamegwa.
“Unaweza kujiuliza kama kigezo ni watu ilikuwaje wamekuja kuimega Mbeya yenye watu pungufu ya Arusha. Mbeya yenye watu 500,000 imemegwa pia Shinyanga imemegwa ina watu kidogo na kuliacha jimbo la Kasulu lenye watu wengi,” amesema.
Amesema ugawaji wa majimbo hayo ni kama INEC wamejielekeza zaidi kwenye kuangalia ushindani wa wanasiasa na si ukubwa wa eneo au idadi ya watu.
Mbali na hilo, Kiama Mwaimu, mchambuzi wa siasa na jamii amesema haukuwa muda muafaka kuyagawa majimbo kwa sababu hatua hiyo itaongeza gharama za uendeshaji kwa Serikali.
Mbali na hilo, Mwaimu amehoji ni faida zitakazopatikana kwa kuongeza majimbo mapya ya uchaguzi zaidi ya gharama za Serikali ikiwemo posho, tiba na mishahara.
Hili linaweza kuwa tatizo kubwa kwa Serikali, hata mwananchi wa kawaida haoni faida ya kuongeza majimbo, mimi naona kama hasara, lakini yule mwananchi wa kawaida ndio kabisa haelewi kuongeza majimbo kutakavyomsaidia.
Mwaimu amebainisha ongezeko la majimbo kwa watu binafsi lina faida kwa sababu atakayefanya kazi katika eneo hilo atapata hiki na kile na kuitwa mheshimiwa, lakini si kwa mwananchi mmoja mmoja atanufaika na hilo.
Mtazamo huo pia anao Mkazi wa Dar es Salaam, Bazo Komu alidai kuwa kuongeza majimbo ni hasara kubwa kwa Taifa na hakuna tija.
Komu amedai kuna baadhi ya maeneo bado hayana shule za msingi, yana ubovu wa miundombinu, uhaba wa vifaatiba haujatatuliwa, lakini Serikali inakwenda kuongeza majimbo yakayokuwa na bajeti yake pia katika mchakato wa kupiga kura.
“Baada ya uchaguzi atapatikana mbunge atakayelipwa posho na mshahara ambao si mdogo, sasa kama fedha hizo zipo kwa nini zisiende kuendeleza maeneo yaliyogawanywa,” amehoji Komu.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amedai kuongeza majimbo peke yake hakuwezi kuongeza thamani ya uwakilishi, ikiwemo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Dk Masabo amesema kwa namna ilivyo kisheria na kikatiba wananchi hawana mamlaka ya kumdhibiti mbunge ndani ya miaka mitano, akitolea mfano mbunge akichaguliwa leo na kuharibu itawalazimu wananchi kusubiria miaka mitano ili kumwajibisha.
“Sasa kama tutakuwa tunaongeza majimbo, tukitaka kuongeza kiwango cha uwakilishi na tukapata wabunge wasioweza kusemea wananchi, ni wazi tutapoteza dhana ya kiwango cha ubora wa uwakilishi, kwa sababu wananchi hawana namna ya kuwadhibiti.”
Mwingine mwenye mtazamo huo ni mdau wa demokrasia, Said Rashid ambaye piaamesema ugawaji wa majimbo una tija kwa wanasiasa lakini kiuchumi na kimaendeleo ni hasara kubwa kwa Taifa.
“Jambo la kusikitisha tuna wasomi wasiokuwa na msaada katika nchi yetu hasa waliobobea katika uchumi, hatuoni mchango wao katika mambo ya msingi kama haya, tunachelewa kuendelea na ukiangalia hata wenye uwezo wa kuzungumza wanakuwa na unafiki, hatuoni ukweli kutoka mioyoni mwao,” amesema.
Said amesisitiza uongezwaji huo ni hasara huku akihoji, kama mbunge ameshindwa kupata bajeti ya kukamilisha miradi ya barabara zenye changamoto jimboni kwake, kutakuwa na utofauti gani hata wakiongeza jimbo lingine kwa kugawanya.
“Hata akiongezeka mbunge hakuna kitu, kwa sababu bajeti ni ileile, hakuna jipya ni hadaa kwa umma na kuwabebesha mzigo wananchi,” amedai Said.
Yanarahisisha kazi
Kinyume na mtazamo wa wachangiaji hao, Dk Kanael Kaale, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Mwanza, amesema kuna tija katika mgawanyo wa majimbo kwa kuwa kutarahisisha kazi kwa mbunge atakayewafikia wananchi kwa urahisi.
“Kutakuwa na uwiano mdogo, mfano watu 150 kwa mbunge mmoja, kwa ajili ya uwakilishi ambapo akiwafikia watu kwa urahisi atapata wepesi wa kutatua changamoto zao.”
“Sasa utasikia wabunge hawaendi majimboni, wakati mwingine tunawalalamikia wapo tu kwa ajili ya masilahi. Lakini wakati mwingine unaona mbunge mmoja anawakilisha watu wengi zaidi, kulinganisha na jiografia na muundo wa mawasiliano yanayosababisha ugumu kwa mbunge kuwafikia wananchi wote kwa wakati mmoja,” amesema.
Dk Kaale amesema majimbo yanagawanywa ili wabunge waweze kuwafikia wananchi, kuwasikiliza na kuchukua kero zao watakazoziwasilisha bungeni kwa ajili ya utatuzi ili kuharakisha maendeleo.
“Mfano katika majadiliano, mbunge anapaswa kuwakilisha watu, unakuta hajawahi kufika kabisa katika maeneo mengine na hajui matatizo ya maeneo husika, hivyo kila atakachojadili kitakuwa si cha kuwakilisha wananchi,” amesema.
Mwanazuoni wa historia, Philemon Mtoi amesema kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kuhakikisha watu wanaolipa kodi wanakuwa na mwakilishi kwenye vyombo vya uamuzi kama bungeni.
“Lililofanyika Tanzania kwa upande mmoja nakubaliana nalo kwanza lina tija kwa waliopata hiyo fursa, lakini kunahitajika kufanyika kitu kingine cha ziada ambacho ni kugawa majimbo pasipokuwa na kiashiria chochote cha kisiasa,” amesema.
Mwanazuoni huyo amesema kugawa majimbo kutatoa fursa nzuri ya wananchi kutimiza hitaji lao la kusikilizwa, mathalan jimbo la Mbeya Mjini lilitabiriwa hata kabla mchakato wenyewe haujaanza.
“Lilitabiriwa kwa sababu ya msuguano wa wagombea sasa hilo ni tatizo, tusigawe jimbo kumsaidia mtu fulani ni muhimu Serikali ijikite kwenye usawa, akitolea mfano Ujerumani, kuwa inaingia mara mbili hapa Tanzania na ina wabunge zaidi ya 500,” amesema.
Amesema kinachotakiwa kwa viongozi wa Tanzania walipofikia uamuzi huo lazima wahakikishe kunakuwa na mtawanyo mkubwa wa uchumi ili kuweza kuhudumia wawakilishi hao wa wananchi.
Akitangaza majimbo hayo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mwambegele alisema tume inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa ibara ya 74 (6) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, ambavyo vimeipa tume jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge.
Alisema kwa mujibu wa ibara ya 75(4) ya Katiba, jukumu hilo linaweza kufanywa na tume mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka 10.