Prime
Walioshinikiza Heche akae pembeni, warejeshwa madarakani
Makamu Mwenyekiti wa Chadema bara, John Heche
Muktasari:
- Uamuzi huo umefanywa na ofisi ya katibu mkuu, Chadema zikiwa zimepita siku mbili baada ya miongoni mwao kwenda Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kumpata taarifa yenye hoja nane kuhusu malalamiko yao ya kusimamishwa uongozi bila taratibu za chama hicho kufuatwa.
Dar es Salaam. Viongozi wanane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosimamishwa uongozi baada ya kutoka hadharani kumtuhumu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche kwamba anakula fedha za michango, wamerudishwa kwenye nafasi zao.
Uamuzi huo wa Chadema umefanyika zikiwa zimepita siku mbili baada ya miongoni mwao kwenda Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kumpata taarifa yenye hoja nane kuhusu malalamiko yao ya kusimamishwa uongozi bila taratibu za chama hicho kufuatwa.
Miongoni mwa waliorejeshwa katika nafasi zao ni Katibu wa Jimbo la Bumbuli, Abubakari Mashambo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, wenyeviti wa Chadema Wilaya za Mkinga na Kilindi mkoani Tanga, Amuli Shindo, Joseph Mwakidasi na Mathias Cosmas.
Wengine ni Aquilin Claud ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema Kanda ya Kati, pamoja na kada mpya wa chama hicho, Joseph Selasini ambaye baada ya kumtuhumu Heche alipigwa marufuku ya kujihusisha na shughuli za chama.
Moja ya barua ya ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Garubindi ambayo Mwananchi imeiona imeeleza namna ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho, ilivyosikiliza rufaa iliyowasilishwa katika ofisi hiyo.
Katika barua hiyo, ofisi ya katibu mkuu Chadema, imekiri mlalamikaji aliyewasilisha maelezo katika ofisi yao, hakusikilizwa kabla ya hatua ya kumsimamisha uongozi.
“Kwa kuwa haki ya kusikilizwa ni haki ya msingi, uamuzi wa kumsimamisha uongozi uliofanywa na kanda ya kati unafutwa rasmi kuanzia tarehe ya barua hii,” imeeleza barua hiyo.
Chadema yafafanua
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Julai 23,2026, Garubindi amesema ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho imetengua uamuzi wa makatibu wa kanda wa kuwasimamisha viongozi hao, kwa kuwa hawakufuata taratibu za kikatiba na kanuni za chama hicho.
“Chadema tunaamini walitoa adhabu, lakini hawakujielekeza sawasawa kwenye matakwa ya katiba ya chama chetu na kanuni zake kwa sababu kitendo cha kusema unamsimamisha kiongozi kwenye wadhifa wake chenyewe ni adhabu,” ameeleza.
Kwa mujibu wa Garubindi, utaratibu sahihi unataka mtuhumiwa kupewa taarifa rasmi kuhusu tuhuma zinazomkabili kupitia barua, kisha apewe nafasi ya kujibu kwa maandishi ndani ya muda uliowekwa.
Amefafanua hatua inayofuata ni mtuhumiwa kuitwa mbele ya kikao husika ili kujitetea kwa mdomo na baada ya kusikilizwa ndipo kikao hicho kitoe uamuzi, si sahihi kuanza kwa kumsimamisha uongozi.
“Kutokana na kasoro hizo za kiutaratibu, ofisi ya Katibu Mkuu ilitengua uamuzi wa makatibu wa kanda na kuzielekeza ofisi hizo kufuta matangazo ya kusimamishwa kwa viongozi hao,” amesema.
Hata hivyo, Garubindi amesema iwapo kanda hizo, zinaamini viongozi hao walifanya makosa, zinatakiwa kuanza upya mchakato na taratibu za kuwachukulia hatua.
“Watuhumiwa hao wana haki ya kusikilizwa kwa kuwa ni haki yao ya msingi, na baada ya kusikilizwa, vikao husika ndivyo vitakavyotoa uamuzi.”
“Watuhumiwa wana haki ya kusikilizwa kwa kuwa ni haki yao ya msingi, na baada ya kusikilizwa, vikao husika ndivyo vitakavyotoa uamuzi. Kutengua uamuzi wa awali hakumaanishi kwamba viongozi hao hawakufanya kosa,” amesema.
Garubindi amesema msimamo wa Chadema, hakuna kiongozi anayesimamishwa kwenye wadhifa wake, kabla ya michakato yote ya kinidhamu kukamilika, kwa sababu kinaongozwa katiba na kanuni zake.
“Barua za kutengua uamuzi huo zilitumwa tangu jana (Jumatano Julai 22) wakati zikiwasilishwa, tukabaini baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa walishawasilisha malalamiko yao Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakitaka kupatiwa haki,” ameeleza.
Mbali na hilo, Garubindi amesema Ofisi ya Katibu Mkuu ilipitia pia rufaa mbalimbali zilizowasilishwa, zilizoonyesha uwepo wa presha kubwa wakati uamuzi huo ukichukuliwa dhidi ya viongozi hao.
Walichokisema makatibu kanda
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini (Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga) Yohana Kaunya amesema wamepokea maelekezo ya ofisi ya katibu mkuu, hivyo kinachofuata ni utekelezaji.
“Si rahisi katibu wa kanda kukaidi uamuzi wa chama ngazi ya juu. Nimepokea kwa utekelezaji,” amesema Kaunya.
Naye, Katibu wa Chadema Kanda ya Kati (Morogoro, Singida ana Dodoma) Ashura Masoud amesema uamuzi wa kuwasimamisha ulikuwa wa kiutawala na hakukuwa na makosa bali walilenga kutuliza hatari iliyokuwa inataka kutokea.
“Hatua tuliyochukua awali ilikuwa si adhabu, bali tulikuwa tuna punguza nguvu ya yeye kuwashawishi wengine kufanya kile alichokuwa amekifanya, “ameeleza.
Masoud amesema uamuzi uliofanywa na Kanda ulikuwa wa dharura katika kuninusuru chama hicho, kutokana na mazingira yalivyokuwa lakini ngazi ya kamati kuu ambayo kama VAR (Teknolojia ya Video Assistant Referee) imeona kuna tatizo.
“Refa akiwa uwanjani anaweza kutoa uamuzi tofauti, lakini ikiangaliwa kwenye VAR uamuzi unaweza kutenguliwa au kubaki ulivyo. Mwisho wa siku VAR (Kamati kuu) imejiridhisha,” amesema Masoud.
Kauli ya viongozi waliorejeshwa
Akizungumzia hatua hiyo, Okola amesema uamuzi huo, ingawa bado anauangalia kwa jicho la kisheria, akidai katibu wa kanda alimsimamisha kwa utashi wake binafsi badala ya kufuata utaratibu wa vikao kama iliyoelekezwa na katiba ya chama hicho.
“Ninachojua uamuzi wa kumsimamisha kiongozi unapaswa kuanza kwa mhusika kupewa tuhuma zake kwa maandishi, azijibu kwa maandishi, kisha aitwe kujitetea mbele ya kikao husika kinachotoa uamuzi,” amesema Okola.
Kwa upande wake, Cosmas amesema bado hajapata barua ya kurejeshwa katika nafasi yake, ingawa ametaarifiwa kuwa imetumwa kwa mtandao.
Kiongozi mwingine, aliyekumbana kadhia hiyo (jina limelihifadhiwa) amepongeza uamuzi wa ofisi ya katibu mkuu, akisema umeonyesha busara na nia ya kulinda umoja wa chama hicho.
Kiongozi huyo, amesema uamuzi huo utazuia baadhi ya wanachama kuendelea kusababisha vurugu au kuchukua hatua zinazoweza kusababisha Chadema kuvutana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hivyo kukipotezea uelekeo.