Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajumbe CCM wanoa vichinjio

Muktasari:

  • Wajumbe wa CCM wanakuwa na nguvu kubwa katika mchujo wa kura za maoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Wao huchambua majina ya wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge. Hata hivyo, mchakato unakumbwa na malalamiko ya rushwa, mizengwe na upendeleo.

Songea/Kilimanjaro. Ni zamu yao au muda wao kutamba wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiyo unavyoweza kusema kwa sasa. Hii inatokana na jukumu kubwa lililopo mbele yao la kuamua nani apite kwenye mchujo wa kura za maoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Kama wewe ni mgombea wa CCM na hujajipanga hadi sasa, basi itakuwia vigumu kupenya kwenye mchujo huo mbele ya wajumbe ambao katika nyakati kama hizi wanapewa kila aina ya majina, ikiwemo kuitwa "wajumbe si watu."

Kauli hii ya wajumbe si watu inamaanisha kuwa wanakuwa vigumu kubadilika au kutegemewa, kwani licha ya makubaliano ya awali na wagombea, wengi wao hugeuka dakika za mwisho wanapokuwa ndani ya sanduku la kura za maoni. Wanaamua kwa sababu zao binafsi au kwa kile wanachodai ni maslahi mapana ya chama.

Wajumbe hawa ni watu wa kawaida, wengi wao wakiwa ni mabalozi wa nyumba kumi, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa mashina au matawi ya CCM, lakini umuhimu wao huongezeka maradufu nyakati kama hizi, na wanajiandaa kunoa mapanga, kwa maana ya kuchambua majina ya wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge katika kura za maoni.

Kwa mujibu wa taratibu za ndani ya CCM, kura za maoni ndizo msingi wa uteuzi wa wagombea, hata kama si za mwisho. Wajumbe wa mashina na mabalozi ndio wanaopiga kura za awali.

Baadaye, kamati za siasa za wilaya, mikoa na hatimaye Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa huamua jina la mwisho kwa wabunge na wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM, jana Jumatano na leo Alhamisi, Julai 10, 2025, vikao vya kamati za siasa za mikoa vinafanyika. Miongoni mwa kazi wanayoifanya ni kuteua wagombea udiwani watatu na udiwani wa viti maalumu watatu, ambao watakwenda kwa wajumbe kupigiwa kura.

Baadhi ya maeneo majina yaliyoteuliwa yamekwishajulikana na kuibua mijadala kwa walioachwa. Kwa upande wa wabunge na madiwani, majina yaliyopendekezwa kwa Kamati Kuu nayo yataanza kujulikana, ingawa yatasubiri uteuzi wa vikao hivyo vya juu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema zaidi ya wanachama 30,000 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania udiwani.

Aidha, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, alisema wanachama 5,475 wamechukua fomu kuwania ubunge na uwakilishi.


Wagombea wahaha

Kama unaona wajumbe ni watu wa kawaida, waulize wagombea wa CCM wa ngazi zote kuanzia ubunge, udiwani hadi uwakilishi, wanavyohaha kuwatafuta kwa udi na uvumba kuhakikisha wanaungwa mkono.

Mmoja wa wagombea wa nafasi ya udiwani katika Mkoa wa Ruvuma, aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema kwa sasa wajumbe wapo katika hali ya utulivu, wakisubiri majina ya wagombea yaliyopendekezwa na kamati za siasa ili kufanya kazi yao ya kuyapigia kura.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 (toleo la 2022), mchakato wa kura za maoni huanzia kwa kuchukua na kurejesha fomu, kisha usaili, kabla ya kupigiwa kura na wajumbe. Wale wanaopita ngazi ya kata hupelekwa kwa kamati ya siasa ya wilaya, halafu mkoa, na kisha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tayari kamati za siasa za wilaya zimeshapendekeza majina ya wagombea watakaowania nafasi za udiwani na ubunge, na kuyapeleka ngazi ya mkoa. Hatua inayofuata ni kamati za siasa za mikoa nazo kuteua wagombea watatu wa udiwani na udiwani wa viti maalumu, ambao ndio watapelekwa mikutano ya kata kwa kura za maoni.

Baada ya kura hizo, kwa upande wa ubunge na uwakilishi, mapendekezo hufikishwa katika Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa Bara, na Kamati Kuu Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kwa upande wa visiwani.

Suala la wajumbe limekuwa gumzo, na jana Jumatano, Julai 9, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, akifungua kongamano la wadau wa sekta ya habari jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, amewagusia wajumbe.

Dk Doto amesema kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi, wajumbe wamekuwa hawatafutikani kirahisi, kwani kila anayeenda kwao huambiwa atashinda.

“Ndugu wajumbe… washiriki, samahani, nilijua ni wajumbe. Ndio mjue mwaka huu mambo yenyewe haya. Waandishi wa habari ni rahisi kuripoti mambo ya watu, lakini siku mkigombea nanyi mtaona.

“Unaenda mahali unakuta mjumbe anasema ‘wewe unapita,’ anakuja mwingine naye anamwambia hivyo hivyo,” amesema Biteko, anayeomba kuteuliwa na CCM kuwania kwa mara nyingine katika Jimbo la Bukombe, mkoani Geita.

Huku washiriki wa kongamano hilo wakifurahia, Dk Biteko amesema hiki ni kipindi ambacho wagombea wanapaswa kukaa karibu na wajumbe, kwani wanaweza kufanya jambo ambalo hukutarajia.

Mmoja wa wajumbe wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa), amesema: “Sisi bwana hatuna wasiwasi, tumeshajipanga. Tuko tayari, ni wao tu watuletee majina tuingie kazini.”


Manyara yazizima

Mkoani Manyara, mamia ya wanachama wa CCM wameonekana mjini Babati, makao makuu ya mkoa, wakifuatilia kuhakikisha majina ya wagombea wanaowaunga mkono yanapitishwa.

Wapambe na ‘machawa’ wa wagombea waliopata taarifa kuwa majina yao hayajapendekezwa na kamati za siasa wamekuwa wakihangaika mjini humo kuhakikisha majina hayo yanarudi kwenye orodha ya waliopendekezwa.

Uwepo wao mjini Babati umetokana na tetesi kwamba baadhi ya vigogo waliotarajiwa hawakupendekezwa na kamati za siasa za kata, wilaya au mkoa, hali iliyoleta taharuki na presha ya kisiasa.

Mmoja kati ya wapambe wa wagombea hao, Simon Mollel, amedai anafuatilia suala la kigogo mmoja kutoka Wilaya ya Simanjiro ambaye jina lake halikuwamo miongoni mwa waliopendekezwa.

Mollel amesema mgombea wake wa Kata ya Komolo pia hakupitishwa, hivyo wameamua kukata rufaa ngazi ya mkoa kwa mujibu wa haki waliyopewa kikatiba ndani ya chama.

Kwa upande mwingine, kada wa CCM, John Loishiye, amesema uamuzi wa kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Simanjiro kupendekeza majina ya wagombea wasomi ni wa kuungwa mkono.

“Wamependekeza viongozi wenye wivu wa maendeleo. Hatutaki tena watu wa migogoro na uchochezi,” amesema.


Vikao vya mchujo vyaendelea

Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba, amethibitisha kuwa wao wameishakamilisha vikao na kupeleka majina kwa kamati ya mkoa.

Shimba amesema kamati ya siasa ya wilaya ilizingatia vigezo vya chama, ikiwemo uadilifu, uwezo wa kuhimili changamoto za kiutendaji, na hali ya kupendwa na wanachama.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Manyara, John Nzwalile, ameeleza kamati ya siasa ya mkoa imekaa chini ya uenyekiti wa Peter Toima na kuchambua mapendekezo yaliyowasilishwa kutoka wilaya.

Nzwalile amesema ngazi ya mkoa haibadili mapendekezo ya kata au wilaya bila sababu nzito.

“Tunazingatia mapendekezo ya ngazi ya chini kwa sababu hao ndio wanaowafahamu wagombea kwa undani zaidi,” amesema.


Changamoto za mfumo

Pamoja na CCM kujivunia kuwa chama chenye mtandao mpana wa kisiasa nchini, mchakato wa kura za maoni umekuwa ukikumbwa na malalamiko ya mara kwa mara. Baadhi ya wagombea hudai upendeleo, rushwa au majina yao kuondolewa bila sababu za msingi.

Kwa mfano, katika kura za maoni za uchaguzi wa mwaka 2015, Tume ya Maadili ya CCM ilipokea zaidi ya malalamiko 2,800 kuhusu mchakato wa kura za maoni. Malalamiko hayo yalihusisha madai ya rushwa, mizengwe na ukiukwaji wa taratibu.

Takwimu za Twaweza mwaka 2021 zinaonesha asilimia 36 ya Watanzania wanaamini kuwa kura za maoni ndani ya vyama haziendeshwi kwa haki, huku wengi wakihusisha hali hiyo na ukosefu wa demokrasia ya ndani ya vyama.

Katika hali hiyo ya presha, matumaini na hofu, wajumbe wa CCM wanabaki kuwa turufu inayoweza kumtoa au kumuingiza mtu kwenye uongozi. Mgombea yeyote anayeidharau nguvu yao, anakosa ramani ya siasa za ndani ya chama.