Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi 16 CUF wajiuzulu

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja ikiwa ni takribani miezi minne tangu CUF ifanye uchaguzi mkuu uliomuingiza madarakani Mwenyekiti mpya, Yusuf Mirambo. Hata hivyo, uchaguzi huo umekuwa ukipingwa na baadhi ya wanachama waliofikisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakidai ulikiuka taratibu za kikatiba.

Unguja/Dar. Safari ya Chama cha Wananchi (CUF) kuwania dola inaendelea kukumbwa na changamoto baada ya viongozi wake 16, akiwamo Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Mohamed Ngulangwa, kujiuzulu nyadhifa zao wakieleza kutoridhishwa na mfumo wa sasa wa uongozi wa chama.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni takribani miezi minne tangu CUF ifanye uchaguzi mkuu uliomuingiza madarakani Mwenyekiti mpya, Yusuf Mirambo.

Hata hivyo, uchaguzi huo umekuwa ukipingwa na baadhi ya wanachama waliofikisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakidai ulikiuka taratibu za kikatiba.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Haroub Mohamed Shamsi amesema hadi sasa chama hakijapokea barua rasmi kutoka kwa viongozi hao.

"Chama kitatoa tamko rasmi endapo kitapokea barua za kujiuzulu. Hadi sasa hakuna barua yoyote iliyowasilishwa kwetu," amesema

Akiangazia hilo kwa jicho la kisiasa, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Ali Maulid Juma amesema kuondoka kwa viongozi 15 kwa wakati mmoja ni pigo kubwa kwa CUF na kunaweza kudhoofisha uwezo wake wa kisiasa na kiutendaji.

Amesema endapo chama hakitachukua hatua za haraka za kurejesha umoja, kinaweza kuendelea kudhoofika na kupoteza ushawishi wake katika medani ya siasa.


Ngulangwa sababu za kujiuzulu

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 28, 2026 kuhusu uamuzi wake, Ngulangwa amesema amejiuzulu baada ya Mwenyekiti wa chama, Yusuf Mirambo, kuuzuia mkutano na waandishi wa habari aliokuwa ameuitisha kulaani kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, iliyozuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

Amesema uamuzi wa kuitisha mkutano huo ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati ya Mashauriano ya Tanzania Bara kilichoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Vedasto Ngombale Mwiru.

Ngulangwa amesema baada ya kutuma mwaliko kwa vyombo vya habari na wanachama, Mirambo aliamuru mkutano huo usifanyike akidai ungeweza kumfanya aonekane hana mamlaka ndani ya chama.

"Ili kuitendea haki dhamira yangu, nimeamua kujiuzulu nafasi ya Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma ili nipate uhuru wa kusimamia ninachokiamini. Nitaendelea kubaki kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kupitia Kanda ya Pwani," amesema.

Mwenyekiti wa CUF, Yusuf Mirambo, amethibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa Ngulangwa pamoja na maelezo ya sababu za uamuzi wake.

Amesema alisimamisha mkutano huo baada ya kubaini uliandaliwa bila yeye, kama Mwenyekiti wa chama, kupewa taarifa wala kufahamishwa ajenda iliyokusudiwa kujadiliwa.

"Si utaratibu wa chama kwa mtendaji kuitisha mkutano na waandishi wa habari bila uongozi wa juu kufahamu ajenda. Nilipomweleza mkutano usifanyike, alikataa na kusema yuko tayari kuachia nafasi yake. Leo asubuhi amenikabidhi rasmi barua ya kujiuzulu," amesema Mirambo.

Amedai Ngulangwa ameshindwa kuendana na mfumo mpya wa uongozi wa chama unaotekelezwa chini ya uongozi wake.


Zanzibar wataja sababu

Akizungumza leo na waandishi wa habari kwa niaba ya viongozi waliojiondoa Zanzibar, Katibu wa Wilaya ya Kaskazini B Unguja, Omar Mohamed Hassan amesema wamefikia uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na mfumo wa uongozi uliopo pamoja na migogoro ya mara kwa mara inayokikumba chama.

"Sisi kwa umoja wetu haturidhishwi na mfumo wa uongozi uliopo, ndiyo sababu ya kujiengua," amesema.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya Kaskazini A, Vuai Kona Haji, amesema tangu ajiunge na CUF hajawahi kuwa mwanachama wa chama kingine, lakini sasa ameona hana sababu ya kuendelea kutokana na migogoro isiyokwisha.

Amesema viongozi hao walikuwa na matarajio ya kukifanya chama kishike dola na kuwatumikia wananchi, lakini hali ya sasa imeondoa matumaini hayo.

Wengine waliotangaza kuachia ngazi ni Ghanima Omar Sultan, Katibu wa Wilaya Magharibi B; Said Omar Mohamed; Abdi Khamis Ramadhani, Katibu wa Wilaya Mjini;

Mwajuma Hassan Khamis, Mwenyekiti wa Wanawake Kaskazini A; Khamis Ussi, Katibu wa Jimbo la Mwanakwerekwe; Mbaraka Azani, Katibu wa Jimbo la Tunguu; Asya Othman Haman, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa na Mshika Fedha wa Magharibi B; pamoja na Kamanda wa chama, Ali Hassan Hamad.

Wengine ni Faki Arazaki Faki, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee Taifa; Maryam Mohamed Hassan, Mjumbe wa Kamati ya Wilaya Magharibi A; Kitwana Juma Kombo na Hamiar Ali Zaidi, Katibu wa Wilaya Wete.