Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujumbe wa Lissu kwa wagombea udiwani, ubunge na Urais Chadema

Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa vikiendelea na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ametoa mwelekeo na msimamo kwa wanachama wanaotaka kuwania udiwani, ubunge na urais akiwamo yeye.

Amesema kwa sasa kilichopo mbele yao ni Azimio la ‘No reform no election’ (bila mabadiliko ya mifumo hakuna uchaguzi) ambayo kila mwanachama na kiongozi wa Chadema anapaswa kuijua na kuitekeleza kwa masilahi mapana ya Taifa.

Lissu ambaye amefikisha siku 33 tangu wajumbe wa mkutano mkuu walipomchagua kuwa mwenyekiti wa chama hicho akimbwaga Freeman Mbowe aliyekuwa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 21.

Mwenyekiti wa Chadema,Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari wa Mwananchi,nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.Picha na Michael Matemanga

Baada ya Lissu kushika usukani wa uongozi wa chama hicho alisisitiza azimio hilo linapaswa kusimamia na hata alipozungumza na vyombo vya habari Februari 13, 2025 kutoa kile walichojadili kwenye vikao vya kamati kuu Bagamoyo, Mkoa wa Pwani alisema bila mabadiliko ya mfumo hakutakuwa na uchaguzi.

Katika azimio hilo, kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya makada na hata viongozi wakiwa hawajui wanaweza kuendelea kujiandaa na kugombea nafasi ama wasubiri mabadiliko ya mifumo.

Hoja hizo wanazijenga katikati ya kushuhudia vyama vingine kama Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshapitisha wagombea urais, Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Dk Hussein Mwinyi (Zanzibar) na Dk Emmanuel Nchimbi, mgombea mwenza wa Rais Samia.

Pia, ACT - Wazalendo imeshafungua milango ya wagombea wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali na tayari kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amekwisha weka nia kuwania urais huku mwenyekiti wake ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othuman Masoud akiweka nia ya urais visiwani humo.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) Bara, Innocent Siriwa yeye ameweka nia ya kuwania urais wa Tanzania huku NCCR- Mageuzi wao wakisema mgombea wao wa urais atajulikana Aprili 2025. Vyama vingine vinaendelea na maandalizi.


Kinachoendelea Chadema

Jana Jumapili, Februari 23, 2025, Mwananchi ilifanya mahojiano maalumu na Lissu nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam yaliyochukua dakika 120 akigusia masuala mbalimbali likiwamo la ‘No reform no election’ linavyowavuruga wanachama wake.

Lissu anakiri suala hilo kutoeleweka vyema hasa ikizingatiwa ilipitishwa Desemba 3, 2024 siku chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 27, 2024 na siku chache baadaye wakaingia kwenye uchaguzi wa ndani.

Amesema ni lazima elimu iendelee kutolewa kwa wanachama na viongozi wote ili azimio hilo lielewe vyema.

Lissu atoa kauli sakata la kina Mnyika, Lema

Lissu mwenye miaka 57 amesema msimamo huo kama utafanikiwa maana yake uchaguzi mkuu utaahirishwa na kama haujafanikiwa, basi wao Chadema hawatokwenda kwenye uchaguzi.

Akifafanua zaidi msimamo wa azimio hilo na muelekeo wa Chadema kwenye uchaguzi mkuu, Lissu amesema kama hoja yao haitazingatiwa hadi Oktoba 2025 kwenye uchaguzi mkuu, Chadema hawatokwenda kwenye uchaguzi.

“Tumesema hakuna uchaguzi, maana yake ni kwamba sisi hatuendi kwenye uchaguzi, tutauzuia, tukishindwa tutakuwa tumeshindwa lakini tumejaribu,” amesema.

Alipoulizwa msimamo huo kuja kipindi ambacho chama kilishafungua milango kwa wagombea ubunge, udiwani na urais na baadhi tayari wametangaza nia akiwamo yeye (Lissu) aliyekwisha kutangaza nia ya kugombea urais, kwa kuandika barua kwenye kwa katibu mkuu Agosti 2024 amesema uamuzi huo wa kugombea bado upo palepale lakini uamuzi wa kushiriki uchaguzi ni wa vikao vya chama na si mtu binafsi.

Alipoulizwa kuhusu nini hatima ya wanachama waliowiwa kugombea ubunge, udiwani na urais kwa kuwa tayari chama kilishafungua milango kabla ya kampeni hiyo, Lissu amesema uamuzi wa kushiriki uchaguzi ni wa vikao vya chama, sio wa mtu binafsi.

“Tulisema watu watangaze nia, tuna utaratibu wa kutangaza nia, mimi pia nilitangaza, lakini msimamo wa chama uliotolewa baada ya mimi kutangaza nia ni no reform no election.

“Mapenzi yangu binafsi hayawezi kuathiri masilahi ya chama, tunaenda na msimamo wa chama, mwanachama binafsi anayetaka kugombea ubunge, uwakilishi, urais haamui yeye binafsi ni uamuzi wa vikao vya chama,” amesema.

Kuhusu msimamo huo kuwarudisha nyuma vigogo waliotaka kuingia Chadema kwa ajili ya uchaguzi mkuu, Lissu amesema kama nia yao ni uchaguzi basi watu hao wabaki huko huko na kama ni kwenda kuipambania nchi wanakaribishwa.

“Wale ambao wametangaza nia na wale ambao hawajatangaza msimamo wa chama ni huo, swali la msingi ambalo nimekuwa nikiwauliza kwenye vikao vya chama, tunakwenda kwenye uchaguzi ili iweje?

“Wanaotaka kugombea ili iweje, ili mkafanye nini katika mazingira haya ambayo wagombea wetu wanaenguliwa, twende kwenye uchaguzi ili tukathibitishe tena kwamba CCM hawataki uchaguzi? hamjalijua ili tangu 2019, hamkuliona kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024?”


Faida za kutoshiriki

Alipoulizwa haoni kuna athari chama hicho kutoshiriki uchaguzi ni pamoja na kukosa ruzuku, Lissu amesema hawawezi kuhalalisha haramu ili wakapate ruzuku.

“Sioni kama kuna athari, tusiposhiriki, hatutapoteza fedha na tatu haya maumivu yote ambayo tunayapata tangu 2015 hatuyapati,” amesema.

“Ni sawa hatutakuwa na madiwani na wabunge na nini, lakini kwani hivi sasa tunao.” amehoji Lissu, akifafanua athari na nafuu watakayoipata endapo Chadema hakitashiriki uchaguzi.


Alichokisema Rais Samia

Wakati Lissu akieleza hayo, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano wa hadhara leo Jumatatu, Februari 24, 2024, Korogwe mkoani Tanga aliwaomba kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ii waweze kushiriki uchaguzi mkuu.

“Jambo letu lipo mwaka huu, kama unafurahia maendeleo na miradi inayoletwa mwaka huu hakikisha unajiandikisha kwenye daftari na siku inafika unakwenda kupiga kura. Kila mwenye sifa ajitokeze,” amesema Rais Samia.

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM akiwamo makamu wake mwenyekiti bara, Stephen Wasira na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla wamesisitiza uchaguzi utafanyika kwa kuwa, hakuna mtu anayeweza kuzuia uchaguzi.

Viongozi hao wanajenga hoja kwamba kuna mabadiliko ya sheria yamefanyika ya kuboresha mfumo wa uchaguzi ikiwamo kwa sasa hakuna mgombea anayeweza kupita bila kupigwa bali atapigiwa kura za ndio ama hapana.


No reform no election ikikubalika

Lissu amesema hoja yao ya ‘No reform no election’ ikikubalika utahitajika muda wa ziada kabla ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu.

“Ni muhimu kutambua muda utahitajika wa ziada, hakuna kitu kinachofanyika cha aina hii kisitumie muda wa kutosha,” amesema Lissu akimaanisha uchaguzi utahairishwa kwa muda.

Akiufafanua mchakato huo, amesema kwa Katiba ya sasa kama ikikubalika kwenda kwenye mabadiliko Rais anaongezewa muda madarakani.

Amesema Bunge likishamaliza muda wake, likavunjwa wakati limevunjwa kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, Katiba ya sasa inasema likitokea jambo la dharura kama hali ya hatari,  Bunge lililovunjwa linaitwa upya, kama lilivyokuwa, wabunge walewale, spika yule yule, mawaziri wale wale na serikali ile ile.

“Wanapewa mwaka mmoja kukabiliana na hiyo dharura, ikishindika kwa muda huo, wanaongezewa mwaka mmoja, ikishindikana wanaongezewa mwaka mmoja, ikishindikana wanaongezewa mwaka mmoja tena, ikishindikana wanaongezewa mwaka mmoja tena,” amesema.

Lissu amesema itakapoongezwa hadi kufika miaka mitano baada ya hapo lazima uchaguzi ufanyike, hiyo ni kama kuna hali ya hatari, akitolea mfano vita na hali nyingine ya hatari.

“Hivi unaweza kusema mabadiliko ya Kikatiba na ya mfumo wa uchaguzi ni hali ya hatari? kama sio inabidi Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuruhusu muda wa Bunge na Serikali kuongezwa nje ya hali ya hatari,” amesema.

“Suala ni je? Kuna muafaka wa kitaifa juu ya mabadiliko? ukiwepo haya mambo mengine yatakauwa marahisi sana, kama hakuna muafaka hakuna kinachowezekana,” amesema.

Katika hilo, Februari 11, 2025, Wasira alisisitiza uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 utafanyika kama ulivyopangwa na wala hakuna chombo chochote cha Serikali kitakachouzuia.

Akizungumzia msimamo huo wa Wasira, Lissu amesema Chadema haina muda wa kupoteza muda na Wasira.

“Yeye sio mwenye maamuzi, sio atakayeamua, atakayeamua ni Samia Rais, tulikuwa na mazungumzo na Kinana (Abdulrahman aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CCM) ya mwaka mzima.

“Rais (Samia) alisema hadharani kwamba watakayokubaliana hawa wa hizi timu mbili, ya Mbowe (aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema) na Kinana, Serikali itayateeleza.

“Wameyakataa yote, tunaposema no reform no election ndiyo hayo tuliwapelekea mwaka 2022 wameyakaataa,” amesema.

Amesema, kuna mtu anayefikiria kwamba Chadema wanakuja na jambo jipya, lakini jambo jipya lao ni kwamba kwa vile wamekataa waliyokubaliana 2022 basi watalazimisha.

“Jambo jipya ni no reform no election, presha ni jambo jipya kwa sababu hawataki mazungumzo, hawataki suluhu za kisiasa, wanataka mashinikizo, wanataka tushinikizane, tutashinikizana,” amesisitiza Lissu.