Prime
UCHAMBUZI WA MALOTO: Faida kwa nchi kuwa na Serikali ya kibunge
Mfumo wa Serikali ya Kibunge, yaani Parliamentary System, una faida tatu kubwa. Kwanza kabisa utaponya changamoto za Muungano, pili utatoa uhuru kwa mihimili ya Bunge na Mahakama, tatu ni kuikinga nchi na gharama kubwa pale Bunge linapovunjwa na Mkuu wa Nchi.
Kuvunja Bunge kabla ya muda wa umri wake ni kitendo chenye hasara kubwa kwa nchi, kiuchumi, kiutawala na kiuwakilishi.
Hasara hizo tatu zinasababishwa na ukweli mmoja kwamba kuvunjwa kwa Bunge, maana yake ni kuitishwa kwa Uchaguzi Mkuu.
Katiba ya Tanzania imetoa mamlaka ya kuvunja Bunge lakini mamlaka hayo yamekaa kimtego. Rais ndiye ana nguvu kisheria kuvunja Bunge lakini akishafanya hivyo naye habaki salama. Nje ya utaratibu wa Bunge kuishi kwa kipindi cha miaka mitano, linaweza kuvunjwa pale yanapokosekana maelewano kati ya Bunge na Serikali.
Kwa nchi ambazo Serikali imechukua mfumo wa Kibunge (Parliamentary System) kama Uingereza, Ujerumani na nyinginezo, faida yake ni moja kwamba mtoa tamko la kuvunja Bunge yeye anabaki salama.
Ujerumani, Mkuu wa Nchi ambaye ni Rais siyo Mkuu wa Serikali. Mkuu wa Serikali ni Kansela, kwa hiyo Bunge la Ujerumani lisipoelewana na Serikali, Rais anavunja Bundestag kisha Kansela na mawaziri wake wote wanapoteza kazi na kurejea kwenye uchaguzi.
Uingereza kwa vile ni nchi ya Kifalme, Mkuu wa Nchi ni Mfalme au Malikia. Kwa kuwa Serikali ya Uingereza hufuata mfumo wa Bunge, tamko la kuvunja Bunge hutolewa chini ya Tangazo la Mfalme, hivyo Mkuu wa Nchi (Mfalme au Malkia) ndiye huvunja Bunge kisha Serikali nayo inakwenda na maji.
Tanzania yenyewe imeshika mfumo wa Nusu-Urais, kwa hiyo kuna Rais ambaye ni Mkuu wa Nchi lakini pia ni Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali.
Katika mfumo huo, Bunge linaweza kumwajibisha Waziri Mkuu kisha Baraza la Mawaziri kuvunjika lakini Rais hubaki salama kisha kumteua Waziri Mkuu mpya na baraza jipya.
Wabunge pia wanaweza kumwondoa madarakani Rais lakini wao wakabaki salama kwenye nafasi zao, huku nafasi ya Rais ikijazwa kwa utaratibu wa Kikatiba. Hata hivyo, inapotokea Rais anavunja Bunge, naye anapoteza urais wake.
Kama Tanzania ingekuwa inashika Parliamentary System, maana yake Rais angekuwa mwamuzi wa juu.
Bunge na Serikali wameshindwa kuelewana, kwa hiyo Rais anavunja Bunge lakini uchaguzi unaitishwa wa wabunge peke yake bila kulazimika kuchagua Rais upya.
Hii ni kwa sababu katika Parliamentary System, Rais anakuwa hana maslahi na Serikali, yeye mamlaka yake ni Ukuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu.
Katika Semi-Presidential System, Rais anakuwa na maslahi na Serikali, kwani yeye ndiye Mkuu wa Serikali.
Bunge na Mahakama haiwezi kuwa mihimili huru, yenye kufanya kazi yake kama inavyotakwa kwenye Katiba bila mabadiliko ya kikatiba kufanyika. Kwa hali halisi iliyopo sasa hivi mwangwi wa Serikali utaendelea kuathiri usawa na uhuru unaotakiwa.
Tatizo la kimsingi lililopo ni kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mkuu wa Serikali lakini pia ni Mkuu wa Nchi, vilevile Amiri Jeshi Mkuu. Tuachane na uamiri jeshi kisha tushike ukuu wa nchi.
Shida ambayo inajitokeza ni kuwa Rais ndiye mkuu wa Serikali. Bunge linatakiwa kufanya kazi ya kuisimamia Serikali. Wakati huohuo Rais ana mamlaka ya kuvunja Bunge na kuitisha uchaguzi upya kama kunatokea mvutano kati yake na Bunge. Yaani, unayemsimamia ana nguvu kubwa kuliko wewe. Huo usimamizi gani?
Mahakama inapobidi inapaswa kuihukumu Serikali. Jaji anamhukumu aliyemteua? Maana jaji anapatikana baada ya Rais kushauriana na Tume ya Uajiri ya Mahakama, kama inavyotamkwa na Katiba, Ibara ya 109 (2) kisha, ndipo Rais anamteua.
Vilevile Rais akiamua, anaunda tume ya kumchunguza jaji kisha inampa ashauri halafu yeye mwenyewe anamwondoa kazini. Mamlaka hayo Rais anayo kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 110 (6).
Katiba Ibara ya 112 (1), inaeleza namna ya uajiri wa mahakimu, kwamba inakuwapo tume ya kuajiri mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama za Tanzania Bara.
Wajumbe wa Tume hiyo ni Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambaye atateuliwa kwa ajili hiyo na Rais baada ya kushauriana na Jaji Mkuu.
Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu na wajumbe wawili ambao watateuliwa na Rais. Ukiangalia orodha yote ya wajumbe wa tume ya kuajiri mahakimu ni wateuliwa wa Rais.
Tafsiri ni kuwa kivuli cha Rais kipo kwenye kila eneo la ajira za Mahakama. Katiba imetoa mwanya huo kwa Mkuu wa Serikali kutamalaki kwenye mihimili mingine.
Tukishakubaliana kuhusu Parliamentary System, jukumu linabaki moja tu, kuunda Serikali mbili zisizoingiliana. Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar, kila moja inaongozwa na Waziri Mkuu.
Serikali ya Tanganyika ifanye kazi ya kuhudumia wananchi Tanzania Bara, na Serikali ya Zanzibar iwahudumie Wazanzibari, kusiwe na mwingiliano katika masuala ya Serikali hizo mbili. Kila moja itimize wajibu wake kwa uhuru.
Halafu anakuwapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye hatakuwa na Serikali, isipokuwa Mkuu wa Nchi, vilevile Amiri Jeshi Mkuu. Rais ndiye anakuwa nembo ya Muungano, maana cheo chake ni mwavuli utakaofunika pande zote mbili za Muungano.
Mkuu wa Nchi hatakuwa na mamlaka ya kuingilia Serikali yoyote, kwa hiyo itapunguza malalamiko ya Muungano kwa sehemu kubwa, kwamba Wazanzibari watajiendesha wenyewe na Serikali yao, kama Watanganyika na Serikali yao, halafu tutabaki nchi moja kupitia mwavuli wa Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais.