Prime
UCHAMBUZI WA DANIEL MJEMA: Chadema ni kama mmekanyaga mdudu sio bure

Huku mitaani kuna simulizi za watu kukanyaga mdudu na kisha kupotea njia nami nafananisha simulizi hii na namna chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinavyofanya mambo yake kana kwamba kimekanyaga mdudu.
Katika simulizi hizo, unakuta mtu anafahamu kabisa nyumbani kwa wazazi wake hadi umbali na hata akifumba macho anaweza kutembea, lakini unakuja kushangaa siku moja anakutwa anakwenda eneo tofauti hadi ashtuliwe.
Kuna baadhi ya makabila wanamwita huyo mdudu Chechele kwamba ukimkanyaga tu, unapotea njia hata kama hiyo njia unaijua kama unavyofahamu chumba chako cha kuishi au unafahamu kilipo choo cha nje hata kama kuna giza.
Kisayansi hakuna kukanyaga mdudu bali kinachotokea ni njia ya ufahamu na utambuzi katika ubongo ndio huingiliwa kutokana na muingiliano wa shughuli nyingi na kuleta msongamano kwenye ubongo na kufuta kila kitu kwa muda.
Kimsingi hakuna kukanyaga mdudu kwa maana ya mdudu kama simulizi zilivyo, bali ni ubongo unacheza kwa muda na kupoteza kumbukumbu ya kutafakari kule unapokwenda, nami naifananisha na Chadema kwa yale ambayo wanapitia.
Chadema wamekanyagia wapi mdudu? ukiniuliza nitakuambia tatizo lilianzia mara tu baada ya aliyekuwa mwenyekiti wao, Freeman Mbowe kutoka gerezani alipokuwa akishikiliwa mahabusu kwa kosa la ugaidi ambalo halina dhamana.
Mara baada ya kutoka mahabusu Ukonga baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kumfutia mashitaka, alialikwa na kwenda moja kwa moja Ikulu kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan, kabla ya kukutana na viongozi wenzake Chadema.
Pamoja na kuwepo taarifa za yaliyojadiliwa Ikulu kufikishwa vikaoni na kuridhiwa, tukio hili ndio liliibua madai baadae kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema tena wengine wakiwa ndani ya Kamati Kuu, kuwa Mbowe amelambishwa asali.
Kwamba ni kutokana na kulambishwa huko asali ndio na akaja na misimamo ya maridhiano ambayo hata hivyo ilishindikana.
Kuanzia hapo, ule upendo, mshikamano na heshima ya baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema kwa Mbowe ambaye ni mwasisi na amekijenga sana chama hicho ilianza kushuka kwa tuhuma ambazo hazina ushahidi wowote.
Hapo ndio tukaanza kumsikia Makamu Mwenyekiti wa chama wakati huo, Tundu Lissu na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu wakija na slogan ya kusema Mbowe aliyeingia gerezani sio huyu aliyetoka gerezani, kwamba amebadilika.
Yaani ni kama vile lilikuwa kosa la jinai kwa Mbowe kukutana na Rais. Hivi unaitwaje na kiongozi wa juu wa nchi ukatae? Ukitafakari sana haya yalitengenezwa kwa malengo mahsusi ili kumshushia hadhi.
Eneo la pili ambalo Chadema ninaona ilikanyaga mdudu na kupotea njia ni kipindi cha kampeni za uchaguzi wao. Kulikuwa na aina ya kampeni ambazo zilikosa utu, ustaarabu na kuchafuana kwa tuhuma ambazo wala hazina ushahidi.
Hapo ndipo wanachama waliaminishwa mambo ya ajabu kuwa kuna fedha za mama Abdul zinatembea kuweka wagombea, mara kuna fedha za Chadema haziingii akaunti ya chama na mengine mengi ilimradi tu kuchafuana.
Hapa ndio tuliona baadhi ya mawakala wa Mbowe, tena wengine hata bila kutumwa, wakimshambulia Lissu kuwa ni mtu asiyeambilika, anakipeleka chama kwenye uanaharakati na kwamba kisingeweza kuwa ndani ya mwezi mmoja.
Mambo haya si tu kwamba yalimchafua Mbowe,Lissu na baadhi ya wagombea licha ya kutokuwepo kwa ushahidi wowote, bali yalikigawa chama na kujenga chuki miongoni mwao, chuki ambazo zinakitafuna hadi leo baada ya uchaguzi.
Jambo la tatu, Mbowe alipopewa nafasi ya kuaga baada ya Lissu kushinda, alisisitiza sana suala la maridhiano, lakini hakuna chochote kimefanyika, bali ni muendelezo wa kutukanana na kudhalilishana hadharani na mitandaoni.
Inaonekana kuna kikundi cha watumia mtandao kilichopewa jukumu maalum la kumshambulia Mbowe na wale waliomuunga mkono hata kama hajawahi kufungua mdomo, wakidhani kupotea njia kwa Chadema kuna mkono wake.
Hoja nyingine inayowafanya Chadema wapotee njia ni ya “No Reforms No Election”, kwamba ililenga kususia uchaguzi au Chadema ishiriki uchaguzi mkuu ama wauzuie, ni kama wamepoteana kuhusu nini hasa malengo yake.
Ukimsikiliza Mbowe wakati anatangaza slogan hiyo Desemba 2025, hakusema watazuia uchaguzi, la hasha, alichokisema kama hadi kufikia kwenye uchaguzi hakuna mabadiliko, basi chama kingesema nini kingefanyika. Sio kuzuia uchaguzi.
Slogan hiyo lengo lake ilikuwa ni amshaamsha na kuitumia kutafuta uungwaji mkono kutoka makundi mengine ya Jamii kama viongozi wa dini, vyama vingine vya upinzani, wanaharakati na wananchi lakini sio kuzuia uchaguzi.
Kwa kiwango kikubwa slogan hii imesaidia kuamsha vuguvugu la kudai mabadiliko ya msingi katika sheria zetu za uchaguzi ambazo hata angekuja Yesu au Mtume Mohamed leo, atakuambia kwa namna zilivyo, uchaguzi hauwezi kuwa wa haki.
Tayari tumewasikia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na baadhi ya Maaskofu, Masheikh, wanaharakati na watu mashuhuri wanahubiri mabadiliko.
Katika kuiunga mkono Chadema, makundi yote hayasemi uchaguzi uzuiwe, la hasha, wanapigania mabadiliko ya msingi katika sheria zetu za uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu 2025, hakuna aliyehubiri matumizi ya nguvu kuzuia uchaguzi.
Wazee mashuhuri kama Jaji Joseph Sinde Warioba na Joseph Butiku wote wanaona haja na umuhimu wa marekebisho ya sheria zetu na wanasema muda upo wa kutosha kabisa kuweza kufanya marekebisho hayo ya kisheria.
Hebu niwaulize Chadema, ni kikao gani cha Kamati Kuu kilikaa na kujadili kuwa wanakwenda kuzuia uchaguzi mkuu kwamba ndio yalikuwa malengo ya “No Reforms No Election”? mkibisha leteni mihustasari ya kuanzia Januari, 2025.
Kwa hiyo kama kulikuwa hakuna kikao cha Kamati Kuu kilichojadili “No Reforms No Election” na kuja na azimio la kuzuia uchaguzi basi hapo Chadema walikuwa wamekanyaga mdudu na kupotea njia na hata G55 walipowashtua hawakusikia.
Mathalan, hivi nikiwauliza Chadema leo, ni kikao gani cha chama kilikaa na kutoa maazimio kuwa Chadema wasiende kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu wanaweza kueleza? Maana ilibidi wajadili wanazuia wakiwa ndani au nje.
Lakini kikao hicho kama ni Kamati Kuu (mathalan), kilipaswa kijadili endapo kama wanakwenda kuzuia uchaguzi, Katiba na Sheria zinasemaje na je kwa mazingira ya kisiasa na vyombo vya Dola ni jambo linawezekana? Umma uko upande wao?
Kwa sababu kama maandamano tu wananchi hawajitokezi, ndio kuzuia kweli uchaguzi ambao uko Kikatiba? Hawa Polisi wetu ambao misimamo yao mnaifahamu watawaacha salama? Hapa Chadema ilikanyaga mdudu.
Jambo la tano, niwaulize Chadema, baada ya mwenyekiti wao Tundu Lissu kukamatwa na kushitakiwa kwa uhaini, hivi hawakuona haja ya kuitisha kikao cha dharura cha Kamati kuu kujadili jambo hili kubwa katika historia ya chama chao!?
Tangu Lissu akamatwe Aprili 9,2025 hadi leo Mei 4,2025 ni siku 25 zimepita, viongozi wamepatwa na nini hawaitishi kikao cha Kamati Kuu cha dharura kujadili mwelekeo wa chama na mikakati gani wafanye kukabiliana na kesi ya Mwenyekiti?
Jambo la sita na la mwisho, uhai wa chama chochote cha siasa cha upinzani unategemea makundi matatu makubwa, la kwanza ni viongozi wanaochaguliwa na wanachama kushika nyadhifa mbalimbali kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.
Kundi la pili ni la wanachama wanaowachagua hao viongozi na kundi la tatu ambalo lina umuhimu mkubwa ni la wagombea. Mkumbuke makundi haya wote wanajitolea muda, fedha na mawazo yao kwa sababu chama hakina Dola.
Mathalan, wagombea ni kundi muhimu sana kuliko hata makundi hayo mengine mawili kwa sababu ndio wenye watu huko chini, wanachama na wasio wanachama wanawaunga mkono. Bila wao uhai wa chama uko shakani.
Kundi hili, kwenye kampeni na Uchaguzi kwa kiasi kikubwa wanajigharamia wenyewe ikiwemo gharama za mikutano, usafiri, vitendea kazi, kulipa mawakala na kila kitu, kwa maneno mengine ndio wanaoimarisha uhai wa chama.
Hao ndio ambao wananchi wanawafahamu kule chini, kwa hiyo ukilivuruga hili kundi, uhai wa chama unakuwa mashakani kwa sababu kwanza ndio wananchi wanawafahamu kule chini, lakini ndio hukipa uhai chama kwa kuchangia.
Sasa kitendo cha kugomea uchaguzi, ambao sio malengo ya awali ya “No Reforms No Election”, maana yake unakwenda kupoteza kundi kubwa ambalo lilitarajia kutimiza ndoto zake kwa kugombea urais, ubunge au udiwani.
Badala ya kuwapa majina mabaya ya usaliti, hoja zao zingesikilizwa na kupimwa na vikao vya maamuzi na sio kuwachukulia kama maadui na bahati nzuri walisema hawapingi msimamo wa chama, lakini walitoa mapendekezo kuuboresha.
G55 ilikuwa na mawazo mazuri sana, kwamba Chadema iendelee kupigana ikiwa ndani kama ilivyofanya uchaguzi mkuu 2020 na uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, na sio nje kwa sababu Slogan hii ilikuwapo na walishiriki chaguzi hizo.
Sasa pamoja na uamuzi huo kuonyesha dhahiri Chadema kuna mahali ilikanyaga mdudu, lakini kitendo cha uongozi mpya kuondoa karibu viongozi wote wa juu waliokuwa katika uongozi wa Mbowe, ni kosa lingine kubwa la kiufundi.
Mbowe na timu yake wanafahamu vichochoro vyote vya kupita, kuanzia kutafuta fedha na namna ya kuibana Serikali ya CCM Kidiplomasia (huwezi kushindana nayo kwa sababu ina Dola), lakini uongozi mpya ni kama wamewaweka pembeni.
Haya yote niliyoyaeleza yananifanya niamini Chadema kuna mdudu imekanyaga na hadi haijui imepotea njia, hata G55 walipowashika mkono kuwa mmepotea, hamtaki kuwasikiliza kwa sababu tu ya chuki, fitna na propaganda za uchaguzi.
Ni kweli kusaliti msimamo wa chama uliopitishwa katika vikao halali ni usaliti na adhabu yake ni kufukuzwa uanachama, lakini nilivyotangulia kusema, hili la kutumua nguvu (kukinukisha) kuzuia uchaguzi hakina baraka za kikao chochote.
Vikao vyote viliunga mkono slogan ya No Reforms No Election lakini si kuzuia.
Ni wakati viongozi wa Chadema, kuitisha vikao vya maamuzi kupitisha msimamo wa Chama kwa sababu hii ya kuzuia uchaguzi mkuu haukuwa msimamo wa chama na ninaamini hakuna nyaraka za No Reforms No Election zinaeleza hivyo.
Vikao hivyo vitumike kujadili mustakabali wa Chadema kama mamlaka zitashikilia msimamo wa kutoiruhusu Chadema kushiriki uchaguzi kwa kutosaini Kanuni za Maadili, ili washushe msimamo unaoeleweka kwa wanachama na wagombea.
Jambo lingine muhimu sana, tafuteni maridhiano ndani ya chama, uchaguzi umewagawanya na mkagawanyika, hata adui hamwezi kumkabili kwa sababu hamko wamoja, mnakosoana wenyewe kwa wenyewe mbele ya umma.
Nimeshawashtua mmekanyaga mdudu, ni uamuzi wenu kushtuka mnapotea, hata mambo ya kumsingizia Mbowe kwa kila jaribu mnalopitia halitawasaidia, huu ni wakati wa kukaa chini na kutafakari ikibidi kubadili gia angani badilini. Si dhambi.
Mfanye hivyo kwa jeuri mkitambue umma wa wapenda haki kwa sasa uko nyuma yenu, lakini msiingie mtego wa kuhamasisha kuzuia uchaguzi mkuu.
0656600900