Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Thamani ya kura yako ni sauti yako, nguvu yako

Nakaribia kutimiza umri wa miaka 60. Tangu uchaguzi wa mwaka 1990 hadi uchaguzi wa mwaka huu, nimepiga kura mara saba na uchaguzi ujao utakuwa wa nane.

Kwa zaidi ya miaka 40, nimekuwa nikitimiza wajibu wangu wa kidemokrasia kwa kupiga kura. Hata hivyo, katika kipindi chote hicho, sijawahi kufundishwa wala kuelezwa kwa kina kuhusu thamani halisi ya kura yangu.

Ninachokiona ni upungufu mkubwa wa elimu ya uraia kuhusu kura. Kinachosisitizwa zaidi ni kujiandikisha ili upate nafasi ya kupiga kura, lakini hakuna elimu inayofafanua kura ni nini na inamaanisha nini kwa mwananchi.

Mara nyingine tumeelezwa umuhimu wa kupiga kura ili tuwachague viongozi tunaowataka.

Lakini bado elimu hiyo haijagusia uzito na thamani ya kura yenyewe. Na hata pale tunapofundishwa jinsi ya kupiga kura, hakuna maelezo yanayoambatana na kujenga uelewa wa thamani ya kura yako kama raia.

Kwa muda mrefu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikikabiliana na changamoto ya wananchi kukwepa au kukataa kulipa kodi.

Mojawapo ya sababu kuu ilikuwa ni wananchi wengi kutofahamu thamani ya kodi wanayolipa.

Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya TRA kuanzisha elimu ya thamani ya kodi, wananchi wakaelewa jinsi kodi yao inavyowezesha huduma za kijamii na maendeleo ya taifa. Matokeo yake ni kwamba makusanyo ya kodi yameendelea kuongezeka kila mwaka.

Hii iwe funzo, kama tulivyofundishwa kuhusu thamani ya kodi, basi tunapaswa kufundishwa pia kuhusu thamani ya kura.

Tanzania kwa miaka mingi ilijitambulisha kama nchi ya siasa ya ujamaa na kujitegemea. Azimio la Arusha lilieleza wazi kuwa maendeleo yanahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Fedha siyo msingi, bali ni matokeo ya sera bora. Lakini leo hii, tunaishi katika mfumo wa soko huria. Fedha imekuwa msingi wa kila jambo. Katika hali hii, basi uongozi wa umma unapaswa kupimwa pia kwa kipimo cha uwajibikaji wa kifedha, hususan ulipaji kodi.

Wenzetu katika nchi zilizoendelea, mtu hawezi kugombea uongozi bila kuonesha historia yake ya kulipa kodi.

Mtu anayelipa kodi kubwa ana uwezo wa kuzalisha kipato kikubwa, hivyo ana nafasi nzuri ya kuleta maendeleo.

Ni wakati wa Tanzania kufikiria mabadiliko ya sheria za kodi, kila mtu, akiwamo Rais wa Jamhuri, alipe kodi.

Na taarifa za ulipaji kodi zitumike kama moja ya vigezo vya uadilifu kwa viongozi wa umma. Hii itasaidia siyo tu kuongeza mapato ya Serikali, bali pia kupata viongozi bora, si wapiga dili wanaoingia kwenye siasa kwa ajili ya maslahi binafsi.


Sasa, turejee kwenye thamani ya kura yako

Kura yako ni zaidi ya kipande cha karatasi, ni mamlaka.

Wewe ni mmiliki halali wa nchi hii, Katiba yake na sheria zake. Kwa kura yako, unamuajiri Rais, mbunge na diwani.

Kupitia kodi yako, unawalipa mishahara yao. Hii ina maana kwamba wewe ndiye bosi mkubwa, wao ni watumishi wako.

Kwa hiyo, kila unapopata nafasi ya kujiandikisha au kuboresha taarifa zako katika daftari la kudumu la wapigakura, usisite.

Kura yako ndiyo sauti yako. Usipojiandikisha au usipopiga kura, utakuwa umeacha wengine wakuamulie nani awe kiongozi wako, lakini bado utawajibika kwa kulipa kodi inayowalipa viongozi uliokosa nafasi ya kuwachagua.


Kura ni hiari, lakini kodi ni wajibu

Kupiga kura ni hiari. Kugombea nafasi yoyote ya uongozi ni hiari. Lakini kulipa kodi ni wajibu wa lazima kwa kila Mtanzania.

Hii ina maana kwamba, hata usipopiga kura, bado utakatwa kodi kwa ajili ya kuwalipa viongozi waliopo madarakani.

Na kama hawakufai, basi ulichangia kuwaleta kwa kukosa kuchagua. Kwa hiyo, ukimkosa kiongozi bora kwa sababu hukupiga kura, wewe ndiyo unapata hasara ya kwanza.


Uhuru wa kushiriki na kutokushiriki

Katika mazingira ya kisiasa, mtu binafsi, chama au taasisi yoyote ina haki ya kuchagua kushiriki au kutoshiriki uchaguzi. Lakini ni kosa la jinai kuzuia au kushawishi wengine wasishiriki.

Kauli ya No reforms, No election ya Chadema ni hoja ya msingi inayodai maboresho ya kikatiba, lakini haipaswi kutumika kama kigezo cha kuzuia uchaguzi au kuwazuia wanaotaka kushiriki.

Kwa mujibu wa Ibara ya 5 na 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kushiriki katika uchaguzi ni haki ya msingi ya kila raia si ya chama chochote cha siasa.

Kura yako ni mali yako. Ni silaha yako ya kidemokrasia. Usikubali kuburuzwa na mtu, chama au kiongozi yeyote kuachana na haki yako hii ya msingi.

Tanzania inahitaji raia wanaojitambua, wanaotumia haki zao kwa umakini, na wanaojua kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kuletwa na wanasiasa pekee, bali na wananchi wenyewe kwa kushiriki mchakato wa maamuzi.

Mungu ibariki Tanzania.