Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SUK bado kugumu, imebaki CCM na Serikali

Muktasari:

  • Uamuzi wa kupatikana kwa mwafaka wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa upo mikononi mwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.



Dar es Salaam. Licha ya kuwepo madai kwamba mazungumzo kuhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo yamekamilika, ngoma inaonekana bado mbichi.

Vyama hivyo vilikuwa katika mazungumzo ya takriban miezi sita kukubaliana mambo yanayopaswa kujumuishwa katika SUK. Katika mazungumzo hayo, ACT Wazalendo ilitoa masharti yanayopaswa kutekelezwa ili iingie.

Miongoni mwa masharti ambayo ACT Wazalendo ilitoa ni SUK isiishie ngazi za kitaifa, iende hadi mikoa na wilaya, pia mamlaka ya Makamu wa Kwanza wa Rais yaongezwe ili awe na nguvu ya kuamua na kuelekeza.

Mazungumzo yakafanyika. Kila upande ukapewa muda wa kwenda kujadili, kukubaliana na kupeleka mezani ili liandaliwe tamko la pamoja. ACT Wazalendo inasema imeshamaliza, mtihani umebaki kwa CCM.

Uongozi wa ACT Wazalendo unasema kila kitu kipo sawa kwa upande wao, kwa sababu wametoa masharti, na wanachosubiri ni makubaliano ya utekelezaji kutoka upande wa pili, yaani Serikali na CCM.

Upande wa CCM haujawa wazi kama umekubaliana na masharti yaliyotolewa na ACT Wazalendo au imeamua vipi. Hata vikao vya kujadili ama utekelezaji wa masharti hayo au vinginevyo havijaanza kufanyika.

Mei mwaka huu, Rais Mwinyi alisema mazungumzo ya kuunda SUK kati ya CCM na ACT Wazalendo yanaendelea vizuri, huku chama chake kikiweka mbele maslahi ya taifa, Serikali, na chama hicho kwa ujumla.

“Mazungumzo hatutoyakataa. Tutaendelea, lakini wasidhani kama watatuburuza katika mazungumzo hayo. Tupo tayari kwa mambo yote ambayo yana maslahi na nchi yetu na tupo tayari kushirikiana,” alisema.


ACT Wazalendo

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Juni 29, 2026, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita, amesema hatua iliyofikiwa ni kila upande kwenda kukubaliana kuhusu mambo ya utekelezaji yaliyokubaliwa.


Amesema CCM ndiyo yenye mambo ya kutekeleza, wakati ACT Wazalendo yenyewe imeweka masharti kwamba ili iingie SUK lazima mambo hayo yatekelezwe.

Hatua hiyo, ameeleza, itapaswa kufuatiwa na tamko la pamoja litakalofafanua kwamba SUK imeundwa chini ya makubaliano kadhaa yanayopaswa kuzingatiwa.

“Hivi navyozungumza bado hakuna tamko la pamoja, na wenzetu sijui kama wameshakaa na kukubaliana kuhusu utekelezaji wa mambo tuliyokubaliana, maana yanawahusu wao,” amesema.

Mwafaka wa SUK, amesema, utatokana na upande wa CCM kupitia vikao vyake kueleza kama umekubali kutekeleza masharti, na kisha ACT Wazalendo itaingia.

“Kwenye masharti hayo mwenye mambo ya kutekeleza zaidi ni CCM kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka. Sisi tumeweka masharti yetu tu kwamba hatuwezi kuingia bila hayo,” amesema.

Amesema kwa sasa kinachosubiriwa ni pande zote mbili kukutana kwa ajili ya tamko la pamoja baada ya kukubaliana na utekelezaji wa masharti yaliyowekwa. Kila ambacho bado hakijaitishwa wala kupangwa lini kitafanyika.

Alipoulizwa kinachoendelea na hatua iliyofikiwa kuhusu SUK, mmoja wa wajumbe wa kamati inayoshiriki mazungumzo ya SUK, Juma Duni Haji, amesema: “Mtaelewa soon (hivi karibuni), hapa najiandaa naenda kwenye kikao.”

Hata hivyo, alipoulizwa zaidi kuhusu kikao hicho na lini pengine watafikia mwafaka, amesema upande wao hauna tatizo, wenye mamlaka ndio waliobaki kwa sababu wana jukumu la kutekeleza.

“Sisi sio tatizo, mwenye hatamu za dola ni Hussein (Dk Mwinyi – Rais wa Zanzibar), sisi tulishakubaliana kila kitu, lakini yeye ndiye mtekelezaji,” amesema Duni.


CCM bado bado

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema yuko nje ya nchi, lakini hatua ya mwisho anayoikumbuka ni kwamba chama kiliridhia mazungumzo ya ndani.

“Yaani Makamu Mwenyekiti (Dk Mwinyi) alishatoa taarifa kwa chama kuhusu mazungumzo na chama kikabariki, lakini sikuwahi kuona kikao chochote, na sasa nipo nje huku sijui zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, amesema bado hajapokea taarifa yoyote ofisini kwake kuhusu kukamilika kwa mazungumzo hayo.

“Mimi sina taarifa hizo kamili kwa sababu chama hakijatangaza, kwa hiyo siwezi kusema kama yamekamilika na yamefikia kiwango gani, au kitu gani kimefikiwa, na hata yale madai yao kama yamefikia kiwango gani,” amesema.


Serikali: Vinazungumza vyama

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma, amesema mazungumzo hayapo serikalini bali kwenye vyama, lakini uamuzi utatolewa kwa pamoja.

“Uamuzi wa vyama utatolewa kwa pamoja, mpaka sasa sijasikia taarifa yoyote kuhusu makubaliano yoyote ambayo wamekubaliana,” amesema Hamza.

Hata hivyo, amesema hayupo katika nafasi nzuri ya kuitolea maelezo kwa sababu chama (CCM) ndicho kinaweza kuongelea, akielekeza atafutwe Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, ikiwa na yeye atakuwa na ruhusa ya kutoa taarifa.

“Maana chama kikisema watatoa taarifa ya pamoja, ukianza kutoa taarifa moja moja unaharibu mpaka mazungumzo,” amesema.

Amesema: “Kwa kuwa wenzetu wameanza kuvujisha yaliyozungumzwa, basi mtafute na wa kwetu (CCM) usikie atasemaje.”

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Nassor Ahmed Mazrui, amesema mazungumzo ya kuondoa mkwamo wa kisiasa yamekamilika na kinachosubiriwa sasa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.

Mazrui, aliyekuwa Waziri wa Afya katika kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi, ametoa kauli hiyo Juni 28, 2026 wakati akifungua mkutano mkuu wa jimbo la Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kwa sasa wanasubiri viongozi wakuu wa pande zote mbili kutoa tamko rasmi kueleza hatua iliyofikiwa.

“Kwa kweli mazungumzo yamekamilika na muda wowote viongozi wetu watatoa tamko,” alisema Mazrui.