Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia: Tumetimiza ndoto za Mwalimu Nyerere

Muktasari:

  • Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Wilaya ya Butiama mkoani Mara leo, mgombea huyo ametaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na kuahidi Serikali yake kukamilisha mchakato wa katiba mpya.

Mara. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imefanikiwa kutimiza ndoto za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP).

Amesema Serikali ya chama hicho imeendeleza na kukamilisha miradi hiyo ambayo ilikuwa ni ndoto za Mwalimu Nyerere pamoja na kumuenzi kwa misingi ya utawala bora.

Samia ametaja miradi mingine kuwa ni makao makuu ya nchi kuhamishiwa Dodoma, mradi wa maji Same-Mwanga, Bwawa la Mkomazi (Korogwe) ambalo kwa sasa limefikia asilimia 50 na Bwawa la Kidunda ambalo litasaidia kutatua kero ya maji kwa mikoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro (kidogo), sasa ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 50.

Amesema Baba wa Taifa aliliachia Taifa misingi mizuri ya kifalsafa, kisera na kisiasa na kuwa kazi yao kutafsiri misingi hiyo na fikra hizo katika mazingira ya sasa na kuwa dira, mipango na ilani zao zinatafsiri fikra hizo kwa kujenga Taifa linalojitegemea, jumuishi na lenye ustawi kwa watu wote na sekta za uchumi.

Samia ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2025 katika uwanja wa Mwenge uliopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara akiendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kwa kipindi cha pili cha miaka mitano ijayo.

“Tunapomzungumzia Baba wa Taifa, hatuwezi kumtenganisha na misingi ya kiitikadi na kifalsafa aliyoijengea nchi yetu ambayo ilibebwa na dhana kama vile uhuru, umoja, kujitegemea, uhuru na kazi pamoja na dhana nyingine muhimu za kiitikadi ambazo alikuwa akitoa kila baada ya muda kujenga nchi yetu na kuleta umoja na mshikamano wa nchi,” amesema Samia.

Kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo, amesema wameweza kutekeleza miradi mikubwa ya utawala bora inayotoa msukumo mkubwa kwenye sekta za uzalishaji ambazo ni sehemu za ndoto za Mwalimu Nyerere.

Ametaja miradi (ndoto) ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa akitamani ifanyike kuwa ni pamoja na ndoto kubwa ya makao makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

“Hili ni suala la utawala bora, tuliamua miaka ile kwamba makao makuu yetu ya nchi yatakuwa Dodoma, tumechelewa kidogo lakini kuanzia awamu ya tano na hii ya sita tumekamilisha uhamiaji na mihimili yote mitatu ya Serikali iko Dodoma. Bunge lilitangulia, Serikali tukafuata na Mahakama mwishoni mwa mwaka jana imehamia Dodoma,” ameongeza Samia.

Mgombea huyo ametaja mambo mengine ambayo ilikiwa ni ndoto ya Mwalimu Nyerere ni ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambapo alitamani lijengwe lakini hali haikuruhusu lakini sasa limekamilishwa na bwawa linazalisha umeme.

Ametaja mradi mwingine ni mradi wa maji wa eneo la Same-Mwanga ambapo Mwalimu Nyerere alijenga bwawa eneo la Nyumba ya Mungu lakini hakuweza kuendeleza mradi huo na kuwa kwa sasa umeendelezwa wananchi wa Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe wanaenda kunufaika na mradi huo.

“Kwa ufupi zile ndoto za Mwalimu za utawala bora, sekta za uwezeshaji watu kiuchumi, maendeleo ya jamii ndiyo haya ambayo tunaendelea kutekeleza ndugu zangu,” amesema.

Amesisitiza kwamba wanaendelea kudumisha tunu zetu za amani umoja na mshikamano kitaifa pamoja na muungano adhimu. CCM inatambua umuhimu wa kuimarisha zaidi mshikamano wa Watanzania kwa kukamilisha mchakato wa katiba mpya kama ilivyoelezwa kwenye ilani yetu,” amesema Samia.

Kuhusu Katiba mpya mgombea huyo amesema kutokana na suala hilo kuwa matakwa ya makundi mbalimbali ya Watanzania kwa nyakati tofauti serikali yake itauendeleza.

“Haya ni matakwa ya makundi mbalimbali ya Watanzania kwa nyakati tofauti tulijaribu wakati wa awamu ya nne mchakato haukukamilika awamu ya sita tunakwenda kuuendeleza mchakato huo. Kama walivyofanya waasisi wetu na wazee wetu sisi tunaendelea kulinda nafasi ya CCM kuyasimamia yote haya maslahi mapana ya Watanzania,” amesema na kuongeza:

“Baba wa Taifa aliwahi kusema bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba na hatukubali nchi yetu iyumbe kwa kisingizio chochote.”