Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wakumbushwa kulinda amani, maisha baada ya uchaguzi

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Butiama,mkoani Mara wakiwa katika uwanja wa Mwenge wilayani humo wakisubiri kuanza kwa mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM,Samia Suluhu Hassan,leo Ijumaa Oktoba 10,2025

Muktasari:

  • Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara wakati wakizungumza na Mwananchi kabla ya mkutano wa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan wilayani humo.

Butiama. Vijana nchini wamekumbushwa kudumisha amani na utulivu kipindi cha uchaguzi na kutambua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Aidha wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ili kuchagua viongozi watakaowawakilisha katika ngazi mbalimbali za uamuzi.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara wakati wakizungumza na Mwananchi kabla ya mkutano wa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan wilayani humo.

Warioba Nyantori, mkazi wa Kijiji cha Mwibagi, amesema ni muhimu Watanzania wakiwemo vijana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo ili kupata wawakilishi watakaowawakilisha katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika ngazi mbalimbali za uamuzi.

“Tunaomba vijana wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu na kuhakikisha wanadumisha amani kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema na kuongeza:

“Tusihamasike kufanya vurugu kwa Taifa letu kipindi cha uchaguzi mkuu kwani Tanzania ni nchi iliyojengwa kwa misingi ya upendo, amani na utulivu, tulinde sana amani yetu.”

Miriam Makubu amesema kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo ni muhimu kudumisha, amani na utulivu katika kipindi hicho.

“Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu tunapaswa kutambua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo tushiriki uchaguzi kwa amani bila vurugu za aina yoyote, tunahamasisha jamii hasa vijana kujitokeza kuchagua viongozi wanaowataka wawawakilishe,” amesema.

Rahel Stanslaus kutoka Kata ya Mirwa wilayani humo amesema kwa kipindi cha miaka minne sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya na kuwa ni muhimu wananchi kujitokeza kuchagua viongozi kwa ajili ya maendeleo.

“Ni muhimu wananchi tusisusie uchaguzi na badala yake tushiriki kuchagua viongozi, sisi wanawake tujitokeze kuchagua wawakilishi wetu ili tuendelee kupata huduma bora za afya ambapo kwa sasa vifo vya mama na mtoto vimepungua katika wilaya yetu kwani huduma za afya zimesogezwa karibu,” amesema.

Samia anaendelea na kampeni kuomba ridhaa ya wananchi kumchagua ili awatumikie kwa kipindi cha miaka mitano, kwa sasa yuko mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo leo anatarajiwa kufanya mikutano Butiama, Serengeti (Mara) na Bariadi Mjini, Mkoa wa Simiyu.

Butiama ni nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye amezikwa nyumbani kwake Kijiji cha Mwitongo wilayani humo.

Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28, 2025 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), idadi ya Watanzania waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpigakura ni 37,647,235 ambao wataamua nani awe diwani, mbunge na Rais.

Kwa mujibu wa taarifa ya INEC iliyotolewa Oktoba 7, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima orodha hiyo inaonyesha wapigakura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na 996,303 wapo Zanzibar.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa jumla ya vituo vya kupigia kura 99,895 vitatumika.