Prime
Sababu Traoré kuwa kivutio ulimwenguni

Dar es Salaam. Ukiacha kina Julius Nyerere, Nelson Mandela, Kwame Nkurumah na Eduardo Mondlane walionasibishwa na jina la 'Mtoto wa Afrika' hatimaye linaibuka tena katika karne ya 21 kwa mkuu wa nchi mdogo zaidi kiumri duniani, Ibrahim Traoré.
Traoré mwenye umri wa miaka 37, ndiye Rais wa Burkina Faso, tangu Septemba mwaka 2022 alipompindua, Luteni Kanali Paul Henry-Damiba, ikiwa ni jaribio la pili kuelekea utawala wa kiraia katika Taifa hilo.

Jina Mtoto wa Afrika, limekuwa likitumiwa kumuenzi kiongozi au mtu mashuhuri barani Afrika aliyeonesha uzalendo, mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi, au aliyetetea maslahi ya Waafrika.
Ingawa utawala wa kiraia ndilo lililokuwa hitaji la wananchi wa Burkina Faso, mwelekeo wa utendaji wa Traoré unaonekana kuwanogea wengi ndani na nje ya nchi yake, kiasi cha kupewa jina la Mtoto wa Afrika.
Kwa mtazamo wa wataalamu wa siasa za Afrika na ulimwengu, mvuto wa Traoré, unachochewa na uthubutu wake wa kuonyesha upinzani wa wazi dhidi ya sera za kimagharibi, ingawa wanashuku aghalabu viongozi wa hivyo hukosa mwisho mwema.
Mashaka yao yanatokana na rejea za kihistoria kwa viongozi wa kaliba ya Traoré, akiwemo Muammar Gaddafi wa Libya, walioangukia kifo kwa misimamo na uthubutu wa kupingana na sera za kimagharibi.
Ikiwa ni sehemu ya mageuzi ndani ya Taifa lake, Traoré amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha Burkina Faso inanufaika na utajiri wake wa madini.
Serikali ya kijeshi, inajenga kiwanda cha kusafisha dhahabu na kuanzisha akiba ya dhahabu ya Taifa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.
Hata hivyo, kampuni zinazomilikiwa na mataifa ya Magharibi zinaonekana kukumbwa na wakati mgumu, ikiwemo Kampuni ya Sarama Resources yenye makao makuu yake, Australia ilianzisha mchakato wa mazungumzo na Burkina Faso mwishoni mwa mwaka 2024 baada ya leseni yake ya utafiti wa madini kufutwa.

Serikali hiyo ya kijeshi chini ya Traoré, pia imetaifisha migodi miwili ya dhahabu iliyokuwa inamilikiwa na kampuni iliyoorodheshwa katika soko la hisa la London, na ilisema mwezi uliopita kuwa inapanga kuchukua udhibiti wa migodi mingine inayomilikiwa na wageni.
Mwanadiplomasia na Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa, Balozi Benson Bana anasema mageuzi na uthubutu wa Traoré kupingana na sera za kimagharibi ndiyo sababu ya kuwavutia wengi ulimwenguni.
Makucha ya ukoloni
Mafanikio ya kiuongozi, ujasiri, kukosa woga dhidi Taifa lililokita mizizi ya utawala ndani ya Burkina Faso ni miongoni mwa mambo yanayomwongezea ushawishi kiongozi huyo kwa mujibu wa Balozi Bana.
Anasema mataifa mengi yaliyotawaliwa na Ufaransa yameshindwa kujinasua kutoka kwenye makucha ya ukoloni, imefikia hatua yanaamuliwa hata nani awe Rais wake, lakini Traore ameinasua Burkina Faso kutoka kwenye hilo.

Kwa sababu nchi nyingi Afrika zimetawaliwa na mataifa yenye itikadi za kimagharibi kama za Ufaransa, anasema kila mmoja anaujua uchungu na mateso yake na anapotokea kiongozi mwenye uthubutu wa kupinga atapendwa, ndio msingi wa kupendwa kwa Traore.
Balozi Bana anaweka wazi kuwa, Burkina Faso kwa miongo kadhaa tangu uhuru wake, limekuwa Taifa linaloendeshwa kwa matakwa ya Ufaransa na linapangiwa cha kufanya, lakini Traore amelikataa hilo na anasimamia uhuru kamili wa nchi yake.
“Katika hali kama hiyo, kiongozi huyo pamoja na kwamba atakuwa katika hatari ya kugombana na mataifa yenye nguvu, lakini ataungwa mkono na wananchi wake, pia mataifa yote yanayoumizwa na makucha ya ukoloni na itikadi za kimagharibi,” anasema.
Balozi Bana aliyewahi kuhudumu katika Taifa la Nigeria, akiiwakilisha Tanzania pia katika nchi ya Burkina Faso, anamwona Traore kuwa aina ya kiongozi aliyesubiriwa kwa muda mrefu na Taifa lake na nchi nyingine za Afrika zinazoteswa na ukoloni mamboleo.
Kinachostaajabisha zaidi ni kile alichoeleza, ujasiri na weledi wa Traore ni matokeo ya mafunzo kutoka Ufaransa, hivyo ni kama mzimu uliolelewa na kukuzwa kijasiri, umemgeuka mlezi.
Anaongeza mapenzi zaidi kwa Traore, anasema yanachochewa na mageuzi anayoyafanya kwa Taifa lake, ukizingatia yalitamaniwa kwa muda mrefu na wananchi wake.
Chuki dhidi ya umagharibi
Kama anavyoona Balozi Bana, Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Ibrahim Rabbi anasema ulimwengu umetengenezwa zaidi na sera za magharibi zinazochukiwa sehemu kubwa duniani anapotokea kiongozi mwenye uthubutu wa kuzipinga atasifiwa na kupendwa.

“Anaonekana shujaa kwa sababu ameamua kuzikwepa sera za Magharibi na imekuwa njia ya Traoré, amekuwa miongoni wa viongozi wachache wenye uthubutu na ikizingatiwa Magharibi mwa Afrika kuna rekodi mbaya ya viongozi wenye upinzani na mkoloni wao Mfaransa,” anasema.
Upinzani dhidi ya mkoloni wao huyo, anaeleza aghalabu husabanisha viongozi husika wasiwe na mwisho mwema, akimtolea mfano, Thomas Senkara aliyeuawa akiwa na umri wa miaka 35.
“Ndani ya Traoré, unamuona Sankara lakini unamuona kijana mwingine aliyeamua kwenda mbali zaidi kufikiria kubadili hali ya maisha ya Burkina Faso moja ya nchi yenye umasikini mkubwa na migogoro mingi,” anasema.
Traoré, anaonekana kuwa mpinzani dhidi ya Magharibi lakini waliowengi wanasahau ndani yake, kuna kiongozi mwingine Muammar Gaddafi aliyekuwa Rais wa Libya.
“Gaddafi alikuwa na upinzani mkali na Magharibi na hata alitumia pesa na raslimali za Libya kupambana na Magharibi kujaribu kuibadilisha Afrika na Libya na kuamsha watu mwisho wake kila mmoja anajua waliomsaliti hawakuwa wazungu isipokuwa wao walichochea na akamalizwa na watu wake,” anasema.
Rabbi anasema Traore ni kiongozi wa kijeshi na nchi yoyote inayoongozwa kwa mfumo huo huwa inavutia zaidi raia wa nchi nyingine.
“Unapokuwa kwenye utawala wa kijeshi wewe unakuwa chini ya amri ya kijeshi na huwezi kuvutiwa nazo labda kama unafaidika moja kwa moja lakini utaona sifa za kiongozi wa namna hiyo zinatoka nje,” anasema.
Mtihani unaomkabili
Rabbi anamuelezea Traore kama kiongozi aliyebadili mwelekeo wa Burkina Faso kwa kuitoa kwenye msingi wa ukoloni kutoka kwenye makucha ya Ufaransa na kuipeleka kwa Urusi.
“Mtihani alionao na hauzungumzwi na wengi na ukizungumza wengi wanakasirika bado Burkina Faso inamatatizo mengi ya kiusalama ndani ya nchi karibu ya nusu ya nchi haiko mikononi mwa jeshi,” anasema.
Changamoto hiyo, ilimshinda kiongozi aliyepita katika Taifa hilo, Bado inamkabili Traore pia.
“Suala lingine la mabadiliko nchi nyingi duniani zinaweza kujiendesha kwa kutumia rasilimali zilizopo bila mikopo na amekuwa akilionyesha hilo hataki kujiingiza kwenye mikopo mipya itakayoiweka nchi yake kwenye shida,” anasema.
Urusi ni salama au yaleyale
Rabbi anasema kuna wanaoamini Urusi na Marekani ni maadui lakini wanasahau kuwa hizo zote ni dola kubwa zinazofanya mambo kwa maslahi yao popote walipo wanajiangalia wao kwanza.
“Labda kama tunapaswa kujifunza twende Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako Urusi aliingia kabla tangu mwaka 2010 hakuna chochote cha mfano wanachoweza kujivunia hawawezi kutoka barabarani hata kumpinga kiongozi aliyepo madarakani,” anasema Rabbi.

Anasema alichokifanya Traore ni kuwaonyesha viongozi wa Afrika lazima wakubali kubadilika kwamba wanaweza kuishi bila kutegemea sera za Magharibi lakini katumbukia mikono ya Mashariki.
“Mashariki hatuna rekodi yeyote ya kuonyesha nchi moja iliendelea kupitia wao. Urusi ilikuwa miongoni mwa mataifa ya G8 yaliyopiga hatua katika uwekezaji wa viwanda 2014, wenzake walimtoa ikabaki G7 lakini Rais wa Marekani, Donald Trump anazungumza naye kutaka kumrudisha kwenye njia,” anasema.
Rabbi anasema ndiyo maana hata sasa hakuna kelele za wanachama wa kundi la BRICS ni kama wametega mtego ukipita huku na kule unanasa na njia pekee ni kubaki.
“Russia wanampa ulinzi Traore lakini lazima wakubali hakutakuwa na suala la mabadiliko, Afrika ya Kati wamebadili hadi ukomo wa Rais kukaa madarakani kutoka mitano hadi sasa hakuna anayehoji,” anasema.
Traoré aliingia madarakani akiwa na umri wa miaka 36 Septemba 2022, ndiye Rais mdogo zaidi duniani aliyezaliwa Machi 14, 1988.
Umri wake umemuondoa katika kasumba ya wazee waliozoea kuongoza Bara la Afrika na hivyo kuwavutia wengi duniani.