Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rwanda yatoa saa 48 wanadiplomasia wa Ubelgiji waondoke nchini humo, yataja sababu

Muktasari:

  • Ubelgiji ni miongoni mwa mataifa yaliyotangaza kusimamisha baadhi ya misaada na ufadhili kwa Serikali ya Rwanda ikiituhumu kuchochea mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kigali. “Ukoloni mambo leo.” Ndiyo sababu inayotajwa na Serikali ya Rwanda kufikia uamuzi wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Serikali ya Ubelgiji, uamuzi ambao umeanza utekelezaji wake jana Machi 17, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda, uamuzi huo umefikiwa baada ya Rwanda kutafakari sababu kadhaa, zote zikiwa na uhusiano na juhudi za kusikitisha za Ubelgiji za kudumisha dhana zake za ukoloni mamboleo.

“Ubelgiji imeendelea kuidhoofisha Rwanda, si tu kabla ya mgogoro unaoendelea, bali pia wakati wa mgogoro huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako Ubelgiji ina historia ndefu na yenye ghasia katika eneo hilo, hasa kwa vitendo vyake dhidi ya Rwanda,” imesema taarifa hiyo.

Rwanda imeishutumu Ubelgiji kwa kuchagua upande katika mzozo unaoendelea nchini DRC, ambapo imekuwa ikituhumiwa na Jumuiya za Kimataifa kuwa inawafadhili wapiganaji wa kundi la M23 wanaoshikilia maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

“Ubelgiji imechagua upande katika mzozo huu na inaendelea kuhamasisha ubaya dhidi ya Rwanda katika majukwaa mbalimbali. Inatumia uongo na upotoshaji ili kuimarisha mtazamo hasi dhidi ya Rwanda, kwa lengo la kuidhoofisha Rwanda na ukanda mzima,” inasomeka taarifa hiyo.


Imeenda mbali na kusema Serikali ya Ubelgiji imekuwa ikiendeleza siasa za ukabila uliokithiri zilizochochea ubaguzi, mateso na mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.


Pia, imeituhumu Ubelgiji kuruhusu ardhi yake kutumiwa na makundi yanayokanusha mauaji ya kimbari na kuendeleza itikadi za kinyama.


“Uamuzi wa leo unadhihirisha dhamira ya Rwanda ya kulinda masilahi ya taifa letu, heshima ya Wanyarwanda, pamoja na kushikilia misingi ya uhuru wa taifa, amani na kuheshimiana,” imeeleza taarifa.

Kutokana na uamuzi huo, Rwanda imewataka wanadiplomasia wote wa Ubelgiji walioko Rwanda kuondoka nchini humo ndani ya saa 48.

“Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna, Rwanda itahakikisha kuna ulinzi wa majengo, mali na nyaraka za ubalozi wa Ubelgiji mjini Kigali,” imesema.

Hadi sasa Serikali ya Ubelgiji haijazungumza chochote wala kutoa taarifa kuhusiana na taarifa hiyo ya Rwanda.


Uamuzi huo umefikiwa wakati ambao Serikali ya Angola imejitwika jukumu la kutafuta ufumbuzi wa mzozo unaendelea mashariki mwa DRC kati ya vikosi vya jeshi la Rais Felix Tshisekedi vya FARDC dhidi ya wapiganaji wa M23.

M23 tangu waanze mapigano na FARDC wameiteka miji mikuu ya mashariki mwa DRC hususan mji wa kiuchumi wa Goma, Jimbo la Kivu Kaskazini na Bukavu ambao ni makao makuu ya Kivu Kusini, huku taarifa zikidai wanaendelea kusonga mbele kuelekea Uvira.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.