Prime
NIKWAMBIE MAMA: Vita ya Iran isiwe kisingizio
Wakati tukisoma katika Shule za Bweni, wanafunzi tulijigawa katika makundi madogo madogo ya watu watatu hadi sita kutokana na jinsi tulivyoendana. Kuna makundi yalivyopenda sana kusoma, mengine yalipenda michezo na sanaa.
Kadhalika kulikuwa na makundi ya watoto waliopenda sana kujirusha na kula bata. Makundi haya hayakukosa madisko ya mwishoni mwa wiki na sherehe nyinginezo za mijini.
Pamoja na kula na kutibiwa hapo hapo shuleni, tulikuwa tukipewa fedha ya kujikimu na wazazi wetu. Kwa kawaida hela ilitumika kwenye muhula mzima hadi tuliporudi makwetu kwa ajili ya likizo. Lakini kwa wenzetu waliochagua kula bata, hela yao haikutosha kuwakidhi muhula mzima. Labda kama walikuwa na wanachama waliokuwa watoto wa mabosi au wa wafanyabiashara wakubwa ndio angalau ingewasogeza.
Walikuwa wakiishiwa kwenye juma la kwanza tangu muhula ulipoanza. Wanafunzi tulikuwa na kawaida ya kusomeana barua zilizoingia na kutoka tukiwa mabwenini. Mara nyingi tulikuwa tukiwacheka sana wenzetu walivyokuwa wakibembeleza kutumiwa mafao na wazazi wao.
Mwanzoni ilisingiziwa zahanati ya shule kuishiwa dawa, lakini wazazi walipata majibu sahihi kwa uongozi wa shule.
Sasa vilitafutwa visingizio ambavyo havikuwa na mahusiano hata kidogo na mazingira ya shule. Mmoja wetu aliandika barua kwa mzazi: “Mama, vita ya Bosnia inaikaribia shule, naomba hela ya kujikinga na moshi.”
Tulimnyang’anya na kuichana barua hiyo. mwingine aliandika: “Baba, Idi Amin amekuja kujificha bwenini kwetu. Naomba hela nihamie Hosteli”. Kadhalika tukaitia moto barua yake.
Lakini kumbe hiyo ndio tabia ya Watanzania. Ni wepesi sana kuanzisha visingizio pale wanapotaka faida zaidi. Marekani walipoanza kunyosheana vidole na Iran, “wanarejareja” walianza kujaza maduka yao kimkakati wakiota faida. Lakini Serikali ya Tanzania ilitoa tamko la kutuliza wananchi, ikisema hakuna tishio la upungufu wa mafuta hata kama vita ya Mashariki ya Kati itapiganwa.
Kabla wananchi hawajamaliza kushukuru, wafanyabiashara tayari walikuwa wamepandisha bei ya bidhaa za matumizi ya kila siku, hata zile walizotengeneza wenyewe. Kwa mujibu wa kauli za maafisa wa nishati, akiba ya mafuta ilikuwapo na usambazaji haukuvurugika.
Lakini sokoni hali ni tofauti kidogo: bei ya sukari, unga, sabuni na hata mafungu ya mchicha zimeanza kupanda kwa kasi ya mwizi.
Huku mtaani tumezoea hali ya bei hupanda kwa sababu tatu; kwanza mafuta yakipanda, pili mafuta yakishuka na tatu mafuta yasipopanda wala kushuka. Kwetu ni kawaida, na hii ndio historia ya biashara. Wengi wanakumbuka wakati wa Vita ya Ghuba ya mwaka 1990–1991, ambapo hofu ya mafuta ilienea duniani. Ingawa nchi nyingi zilikuwa bado na akiba, baadhi ya masoko yalionyesha dalili zile zile: bei zilipanda haraka kuliko taarifa rasmi.
Miaka kadhaa baadaye, wakati wa msukosuko kidunia wa fedha mwaka 2008, kulikuwa na hadithi kama hiyo. Habari ya kuyumba kwa uchumi ilifanya baadhi ya bidhaa kupanda bei hata kabla wananchi hawajaelewa vizuri kilichotokea. Wengine wanakumbuka kipindi cha janga la Uviko-19. Mara tu uvumi ulipoanza kusambaa, bei ya bidhaa ilipaa kama puto. Pengine walisahau kutueleza kuwa virusi vinapoigusa noti, vinaishusha thamani.
Au pengine ni kutoelewa vizuri elimu ya fedha. Tunavyojua sisi, bei hupanda pale gharama za uzalishaji au usafirishaji zinapoongezeka. Kwa mfano pale inapokosekana mvua kwa maana ya ukame, mashamba yanaposhambuliwa na wadudu waharibifu kama nzige au uhaba wa mafuta unaosababisha ongezeko la bei yake. Ni lazima nguvu ya ziada itumike kupambana na hali hizo. Lakini katika masoko yetu, bei hupanda pia pale uvumi unapoongezeka.
Hivyo wakati Serikali inahakikisha hakuna upungufu wa mafuta, uthibitisho uwafikie wafanyabiashara na walaji kwa uzito unaofanana. Ninaposema wafanyabiashara namaainisha ni pamoja na wale wanaohusika na mafuta. Wenzetu wanaonekana kuwa na tahadhari ya kivyao, wanapandisha bei mapema ili “kupambana na magumu yanayokuja”. Sasa sisi walaji tufanyeje? Maana hata tukipunguza kula bei zitatufuata humohumo kwenye “mfungo”.
Faraja yetu inabaki kuwa mafuta bado tunayo, vita iko mbali na bidhaa bado zinapatikana. Lakini faraja hii inauawa na changamoto ya bei zake zinazokwenda kasi kuliko mafuta yenyewe. Labda siku moja tutaandika kitabu kinafofanana na njozi, kinachoelezea nadharia ya bei kupanda kwa hofu ya kitu ambacho bado hakijatokea. Ni kama kupandisha bei ya mayai mara jogoo anaposalimiana na mtetea.
Tungependa sana wahusika wakiwemo Tume ya Bei (sijui kama bado ipo), wawe wakifanya ziara za mara kwa mara hasa yanapotokea haya yanayotokea sasa. Au ikiwezekana iundwe “Tume ya Walaji” itakayobeba wajumbe kama sisi ili nasi tupate silaha ya kujihami. Maana katika msururu mzima wa wahitaji, ni walaji pekee wanaokosa mtetezi. Labda waamue wenyewe kususia manunuzi, lakini je, matumbo yao yatawaunga mkono?
Usije ukashangaa Tume ya Walaji ikabeba uzito wa wengi wakiwemo wafanyabiashara wenyewe. Hili linaeleweka vizuri, wala haina haja ya kutumia nguvu nyingi kulifafanua. Ndio maana nyoka ukishamuwahi kichwani tu, kazi yake huwa imekwisha.