Prime
NIKWAMBIE MAMA: Uchaguzi si ngoma ya lelemama

Muda unakwenda bila kurudi nyuma. Hili ni jambo mahususi kwa Watanzania kukumbuka hasa katika kipindi hiki tunachouelekea uchaguzi mkuu. Uchaguzi si lelemama, ni mchakato unaoweza kutupatia viongozi au kutubadilishia kabisa maisha yetu kama Watanzania.
Kuna baadhi ya majirani zetu wanaomba muda ungejirudia kabla hawajafanya chaguzi ili warekebishe mambo, lakini maziwa yakishamwagika huwa hayazoleki.
Wenzetu wanajutia baada ya kufanya uchaguzi na kupata matokeo yaliyopelekea simanzi. Mifano michache ya nchi hizo ni Ivory Coast walipopiga kura mwaka 2010.
Uchaguzi wao ulisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya mgombea aliyekuwa madarakani, Laurent Gbagbo, kukataa kukubali kushindwa na Alassane Ouattara.
Hali hii ilisababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha vifo vya maelfu na kuleta maafa makubwa ya kibinadamu.
Ikaja kutokea kwa jirani zetu wa karibu, Kenya mwaka 2007. Uchaguzi wao uliishia katika mgogoro mkubwa baada ya matokeo kutangazwa kuwa Rais Mwai Kibaki alikuwa mshindi, huku upande wa upinzani ukidai uchaguzi uliibwa.
Hali hii ilisababisha machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya 1,000 na kuwahamisha maelfu. Kenya ilijipiga mhuri ambao unadumu mpaka hivi leo.
Zimbabwe nako yalitokea mwaka 2008. Uchaguzi huu ulikuwa na dosari kubwa ukihusisha vurugu, vitisho na hila dhidi ya upinzani, hasa dhidi ya Morgan Tsvangirai.
Raia wengi walihisi kwamba uchaguzi huo uliwapelekea kwenye utawala wa kiimla zaidi na kushuka zaidi kwa hali ya kiuchumi na kijamii.
Walikutana na hali ngumu hasa baada ya thamani ya pesa yao kushuka zaidi ya pesa ya Uganda katika kipindi cha Idi Amin.
Burundi yaliwatokea mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu kinyume na matakwa ya wengi. Kuliibuka maandamano, machafuko na ghasia kubwa.
Kabla ya mabadiliko, Katiba ya Burundi ya mwaka 2005 (iliyotokana na Mkataba wa Amani wa Arusha) ilieleza wazi kuwa rais anaweza kuhudumu mihula miwili ya miaka mitano mitano bila nyongeza.
Lakini Rais Nkurunziza alidai kuwa muhula wake wa kwanza (2005–2010) haukupaswa kuhesabiwa kwa sababu hakuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, bali alichaguliwa na bunge kama sehemu ya makubaliano ya amani ya Arusha.
Kwa hiyo, alidai kuwa ana haki ya kugombea tena mwaka 2015 kwa kuwa amehudumu mihula miwili tu kwa uchaguzi wa moja kwa moja.
Mahakama ya Katiba ya Burundi iliidhinisha uamuzi wake, ikisema kuwa muhula wake wa kwanza hauhesabiki, jambo lililopingwa vikali na wapinzani na baadhi ya wananchi waliodai kuwa hiyo ni dhuluma.
Rais hakuwa tayari kurudi nyuma na matokeo yake kukazuka maandamano makubwa ya kupinga uamuzi huo, jaribio la mapinduzi, maelfu waliikimbia nchi kutokana na machafuko na baadaye matokeo ya uchaguzi yaliyogomewa na wapinzani.
Mwaka 2018 ikawa zamu ya DR Congo. Uchaguzi wa mwaka 2018 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ulikuwa wa kihistoria kwa sababu ulikuwa fursa ya kwanza ya kukabidhiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu nchi ipate uhuru mwaka 1960.
Uchaguzi wao ulitarajiwa kuwa fursa ya mabadiliko, lakini matokeo yake yalipingwa na wengi kuhisi kuwa uchaguzi haukuleta mabadiliko yaliyotarajiwa.
Tatizo kubwa lililoonekana hapa ni kitendo cha Rais Joseph Kabila alikuwa ameongoza tangu mwaka 2001 baada ya kifo cha baba yake Laurent Kabila kuhisiwa kufanya figisu.
Awamu yake ya uongozi ilipaswa kuisha mwaka 2016, lakini alisemekana kuchelewesha uchaguzi mara kadhaa, jambo lililosababisha maandamano ya upinzani na jumuiya ya kimataifa kushinikiza aondoke madarakani.
Baada ya uchaguzi wa 2018, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) ilimtangaza Félix Tshisekedi kuwa mshindi. Lakini mpinzani mwenzake, Martin Fayulu alidai kuwa matokeo hayo yalichakachuliwa na kwamba yeye ndiye aliyeshinda kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura.
Ripoti ya Kanisa Katoliki ambalo lilikuwa na maelfu ya waangalizi wa uchaguzi, pia ilionesha matokeo yalipingana na yaliyochapishwa rasmi.
Martin Fayulu aliwasilisha pingamizi katika Mahakama ya Katiba, lakini mahakama ilithibitisha ushindi wa Tshisekedi.
Hata hivyo kulikuwa na madai ya makubaliano ya kisiri kati ya Tshisekedi na Kabila ili kuhakikisha Kabila na chama chake wanadumisha ushawishi serikalini kupitia bunge na taasisi za usalama. Yaani kama “uchawa” fulani hivi.
Jumuiya za Kimataifa pamoja na Umoja wa Afrika zilieleza mashaka yao, lakini baadaye walikubali matokeo.
Kama kawaida, makovu huja baada ya vidonda. Kulitokea mgawanyiko wa kisiasa kati ya urais wa Tshisekedi na bunge lililodhibitiwa na chama cha Kabila.
Kongo ikaendeleza matatizo ya kiusalama, changamoto za kiuchumi, ufisadi, na huduma duni za kijamii.
Hayo yanalifanya Taifa hilo lenye utajiri wa madini kutokuwa sehemu salama hata kidogo ya kuishi.
Watanzania tujihadhari na uchaguzi usio wa haki unaoweza kupelekea machafuko na umwagaji damu.
Ni sisi tu na hakuna mwingine wa kuamua hatma yetu. Huu ni mtihani mkubwa, tuelewe kuwa dunia nzima na vizazi vyetu vinatutazama jinsi tunavyoufanya.