Prime
NIKWAMBIE MAMA: Acheni siasa za mchelea mwana kulia...

Malezi yana athari ya kudumu maishani mwa mwanadamu. Tofauti ya watu inayoonekana leo inasababishwa kwa kiasi kikubwa na malezi yao tangu utotoni.
Kwa jinsi hii unaweza kuwatofautisha watu wa jamii tofauti, lakini pia hata wa jamii moja waliolelewa tofauti.
Chukulia mmoja alilelewa kwa kufuatana na mila na desturi za kabila lake, na mwingine akalelewa kuendana na mabadiliko ya wakati na makuzi ya teknolojia.
Tofauti zao zinajidhihirisha bayana ukubwani pasi na kutumia visaidizi katika kuwatofautisha.
Hakuna asiyejua kuwa kumdekeza mtoto ni kumharibu. Wazee wetu waliotutangulia walifuata malezi yaliyotokana na mila na desturi za kikabila.
Hawakuruhusu mtoto adekezwe bila sababu za msingi. Wazazi waliwakataza walimu kudekeza watoto mashuleni, na walimu waliwakataza wazazi kuwafanyia hivyo majumbani. Kulikuwa na mfumo uliomweka mtoto kuwa wa jamii; alisimamiwa na wote kwa manufaa ya jamii nzima.
Mtoto alipomkosea mtu mzima kwa makusudi aliadabishwa na yeyote, na alijitahidi kufuta alama, kwani mzazi wake angegundua tukio hilo angempa nyongeza ya adhabu.
Lakini tunaona tofauti kubwa kwenye malezi ya kisasa majumbani hadi mashuleni. Huku uswahilini ukimtuma mtoto wa mtu akuchukulie kitu dukani, mama yake atakuja juu. Kadhalika ukimnyoshea mkono ukitaka kumnyosha mtoto, utaambiwa “zaa wako umdunde kama ngoma."
Walimu wa huku mtaani wanalazimishwa kufuata mitalaa ya wazazi katika malezi ya watoto. Jirani alimpeleka mwanaye kwenye shule bora ya kisasa. Mtoto alikaa huko mwaka mzima, na alirudi likizo katika mwaka uliofuata.
Mtoto huyu alirudi akiwa si yeye kabisa. Hakuweza tena kunywa chai ya mkandaa wala kula muhogo wa kuchemshwa. Hakujumuika na wenzake shambani wala michezoni, na mbaya zaidi alishindwa kuwasiliana na wenzake.
Aliwaambia kuwa alikatazwa kutumia lugha yoyote zaidi ya lugha za kimataifa, hususan Kiingereza na Kifaransa.
Hadi hivi tunavyoongea, ndugu zake waliokosa bahati ya kusoma ndio wanaowasaidia wazazi kwa kazi za ujasiriamali.
Yeye kutwa kucha yupo na kompyuta mpakato akitafuta kazi mitandaoni.
Kama jinsi familia zetu zinavyolelewa katika kizazi hiki, ndivyo wanachama, viongozi, wafuasi na wagombea kutoka kwenye vyama wanavyolelewa na vyama vyao. Ukizingatia kuwa dunia imetupeleka umbali mrefu kutoka kwenye tamaduni zetu kuelekea kwenye ulimwengu wa kidijitali, malezi ya mila na desturi yanaelekea kufutwa kabisa.
Matokeo yake hayatofautiani na yale ya malezi ya mtoto aliyepelekwa shule akasahau kuwaamkia wazazi kwa lugha yake mama.
Kabla na baada ya uhuru, Tanganyika ilikuwa na mfumo wa vyama vingi. Chaguzi za 1958 – 1959, na ule wa kumchagua Rais baada ya uhuru (1962) ni mifano inayokumbukwa. Vyama vya wazungu, Wahindi, Waafrika na kadhalika vilichuana kugombea viti bungeni na hatimaye urais kwa mbinde na sarakasi nyingi. Hizi figisu za vyama na wagombea tunaowaona leo, si ngeni kabisa machoni pa wazee walioshiriki chaguzi zile.
Uzuri wake hakukuwa na malezi ya dijitali. Ukiyatimbanga huko mtaani utamalizana nao huko huko.
Walikuwepo wagombea wachache walioanzisha ugomvi kwa kutegemea mbio, vyama vyao viliweza kuwasaidia kuwaficha kwenye nyumba za wanachama hadi pale upepo ulipopita.
Lakini hakukuwa na mgombea aliyethubutu kutunisha msuli wake, wa chama, wa Serikali au wa wafadhili mbele ya wenzie.
Sasa hivi malezi ya kidijitali kwa wagombea yanatutoa njiani. Mgombea anakuja kuwatukana wenzake mtaani huku akiwa amesimamisha tumbo kama kiongozi wa bendi ya shule.
Mkimgusa tu, hizo kelele zitakazofuata nyuma yake mtaomba ardhi ipasuke. Wanasema “ukitaka kujua nguvu ya mlevi mwaga pombe yake", sasa picha ninayoiona hapa ni mgombea kubeba taswira ya pombe; mlevi mwenyewe ni nani hasa? Inanikumbusha enzi zetu wakati tulipokuwa tukicheza na mjukuu wa aliyekuwa mgambo wa manispaa wa enzi za ukoloni.
Mzee huyu hakuwa ameacha kunyoa denge, kupiga ‘way' na kuvuta kiko au mtemba. Siku alipolianzisha, hakukuwa na mmoja katika wazazi wetu aliyethubutu kutoka ndani kwake.
Basi nakumbuka hadi leo tulipocheza na mjukuu wake, tulimhami sana asilie kwa kuwa tulimwogopa sana babu yake.
Kwa kulijua hilo, mwenzetu alikuwa akisusa na kuvimbisha mashavu kila mara. Nasi tulimchangia mpaka hela ili kumridhisha na amani iendelee kuwapo. Hii ndiyo taswira ya wagombea wetu.
Mzimu wa kudharau mila na desturi zetu unatupeleka kila siku kushinda kwenye korido za Mahakama tukishtakiana.
Tunaacha kufanya mambo muhimu kama kunadi sera za vyama vyetu, kueleza mustakabali wa siasa zetu na kupambanua dira ya uongozi wetu mara tutakapoaminika kuendesha nchi.
Katika uchaguzi wa kisasa, vyama vinachukua picha ya majibwa makubwa yanayoamrishwa na watoto ambao ndio wagombea.
Sekunde yoyote kitaumana kwa sababu majibwa haya hayawezi kuongea kistaarabu, ila kila moja lipo kwa maslahi ya mtu wake. Ndivyo isivyo bahati, kwani vyama vinadhani kuwapambania wagombea wake hata kama hawana sera ni kuvipaisha vyama vyao katika medani za siasa.
Vyama viache kuendekeza wagombea kwa kudhani ndio wanaovipandisha daraja, bali viwekeze kwenye sera.