Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Msingi wa ghorofa upo chini, wa maji upo juu

Lipo tatizo kubwa lakini sijui kwa nini hawa jamaa zetu wanaogopa kukwambia. Wao kila siku wanakalia mapambio tu utadhani hawayaoni.

Kama kweli hawayaoni, basi ni lazima tujiulize sababu zinazowafanya waendelee kuishi hapo mjengoni. Matatizo ni bwawa kubwa, huanza na chemchemi moja, hivyo haiwezekani kulikausha bila kuifuta hiyo chemchemi isipeleke mikondo bwawani.

Hakuna jambo lisilowezekana. Mkondo wa maji ukiamua kuuhamisha mtaa inawezekana. Lakini mtaa pia unaweza kuhamisha mkondo wa maji ili mradi vyote viwili vikubaliane na uhalisia wa mazingira.

Haijatokea mtu kuamua kuyapeleka maji mlimani pasipo na nguvu nyingine za kisayansi. Msingi wa maji unatokea juu kisha matokeo yake yanaonekana bondeni, lakini msingi wa mtaa wenye maghorofa huwa chini.

Hivi sasa Serikali nzima imehamishia macho na masikio yake mabondeni. Kelele za mabondeni zimekuwa endelevu zikipita katika hatua za maombi (yaani kuwaomba waathirika wahamie sehemu salama walizotayarishiwa), mafukuzo pale Serikali ilipobidi kutumia msuli ili kuepusha madhara, “kelele za chura” ambapo vilio vya wahanga havikusikilizwa kwa sababu ya ubishi wao.

Kilikuwepo kipindi cha maombi ya waathirika kurudi maeneo yao hatarishi.

Kuyumba kwa jengo kunatokana kwa kiasi kikubwa na tatizo la msingi. Hivyo Taifa linaweza kuwa legelege na lisilo na maana lisipokuwa na misingi imara. Mara nyingi kutokuwa na uhakika wa pamoja katika jambo linalohitaji usimamizi wa pamoja kunaweza kuzitenga mamlaka baada ya ajali. Ni sawa na haya tunayoyaona kwa mamlaka kubwa zinazofikia kutishiana hatua za kisheria kwa yale yaliyofanyika kabla. Huku kwenye barabara tumesikia jinsi washauri wa ujenzi wa wakati huo wanavyohemea machungu baada ya kitisho cha kuburuzwa mahakamani.

Kadhalika baadhi ya wenye nyumba za mabondeni wanapishana kwenye vyombo vya sheria kutaka zichukuliwe hatua kali za kinidhamu dhidi ya viongozi wao wa mitaa. Wao wanadai taratibu za kisheria zilitumika kuwaweka katika hatari hiyo ya kupoteza mali na maisha.

Viongozi wanakiri kufanya makosa katika kuidhinisha ujenzi wa mabondeni. Wengine wanadhani “kama kusingekuwa na watenda dhambi, wachungaji wa kondoo za bwana wangelifanya kazi gani?” Yaani waliyajua makosa yao ambayo mwendelezo wake ni kwenda kutoa misaada na hotuba za kuwasihi waathirika kuondoka kwenye maeneo hayo. Wanafanana na mganga anayekuroga ili akutibu.

Bila shaka unakumbuka kuwa ujenzi wa mabondeni ulipigwa marufuku tangu miaka mingi iliyopita, lakini ukitaka kuamini kuwa hawa si watu, angalia hati za waliouziwa maeneo hayo juzi na jana utakuta saini na mihuri ya haohao viongozi wao. Nyuma ya pazia wapo viongozi wanaoendelea kuhalalisha makosa ili wapite humohumo kudai fadhila. Wakati mwingine wamekuwa wakitumia kivuli cha Serikali yako tukufu kuendeleza dhambi hiyo bila huruma.

Iwapo kungelikuwa na msingi wa kutoruhusu upungufu wa aina hii, kusingelitokea mabalaa yanayoishughulisha Serikali kuu kuacha kutekeleza miradi ya maendeleo na kurudia yale iliyoyawekea uamuzi tangu mwanzo.

Wakati mwingine najiuliza maswali yasiyo na majibu; iwapo kosa ni la kisheria ama ni la kiongozi kama binadamu. Najiuliza hivyo nikizingatia kiapo na kanuni za uongozi.

Ninavyoelewa mtu akifanya kosa kama hilo bila ya uthibitisho wa ofisi yake anastahili kulibeba jumba bovu mgongoni mwake. Akifanya makosa akiwa nyuma ya meza ya ofisi kama kiongozi, tena akapigia na mihuri aliyokabidhiwa baada ya viapo, kosa huwa kubwa maradufu kwa sababu anaibebesha mzigo Serikali yako inayoaminiwa na wananchi wake. Kwa lugha nyepesi “anakubebesha mzigo wewe akiwa mwakilishi wako”.

Ukae ukitambua kuwa huku uswahilini, viongozi wetu ni Miungu-watu. Yaani ni wenye nguvu zaidi ya chochote hata kile kilicho juu yao. Walisema “pesa huvunja milima na kujaza mabonde”, hivyo kigezo hiki huenda kilitumika kulijaza bonde la Msimbazi. Ndiyo, bila shaka wakazi waliokutana na udhia walipenyeza rupia na kuyafanya mambo kuwa mepesi. Lakini wepesi wa mzigo huweza kusababisha punda asimalize kazi yake mapema.

Kwa jinsi ninavyodhani, hawa washauri wa ujenzi wanaotishiwa kuburuzwa Mahakamani wala hawakutakiwa kufanyiwa hayo. Tatizo ni viongozi wanaotaka ushauri waupendao.

Kwa mfano daktari anayeshauri mgonjwa afanyiwe upasuaji hulazimika kuchukua saini ya mgonjwa au msimamizi wake ili wasije kulaumiana baadaye. Ndivyo viongozi wetu waliotaka ushauri wa ujenzi wa barabara: si ajabu mtindo uliotumika ni uleule.

Utamwambia nini kiongozi anayetaka muarubaini wa ghafla kwa wapigakura wake? Utamwambia kwamba “wahamishe” wakati yeye hazioni roho zao, bali karatasi za kupigia kura? Nadhani umejionea wazi jinsi kiongozi mdogo anavyoweza kuwapa notisi wakubwa wake, tena hata “kuwatrotisha” mchakamchaka hadharani. Ndivyo yanavyotendeka uswahilini: Mtaalamu hana la kusema mbele ya kiongozi wake!

Natamani sana kuunganisha somo hili na jinsi tunavyowajenga watoto wetu kama misingi ya Taifa lao. Wao wanajifunza kutokea kwetu, lakini kwa kadiri dhambi inavyozaa laana, wakienda kwa mfano wetu watalipoteza Taifa lao. Ni heri tukemeane na kuzifuta dhambi hizi ili nao wajifunze kwa mifano hai. Kwa sasa nikuachie hayo wakati najiandaa na misingi bora ya Taifa kwa wenetu.