Prime
NIKWAMBIE MAMA: Kosa la pili halifuti la kwanza

Katika kila jamii kuna mambo yanayostahili kupongezwa na kuungwa mkono, na yapo pia yanayostahili kulaumiwa au kulaaniwa.
Jamii yoyote ile, iwe inaongozwa kwa misingi ya demokrasia, kifalme au hata udikteta, kuna vitendo vinapofanyika huwa havikubaliki na jamii husika.
Lakini pale jamii inaposhindwa kupaza sauti, kukosoa au kulaani maovu hayo, hujikuta ikibaki na masikitiko, ikiguna pembeni na kutikisa kichwa kwa uchungu na unyonge.
Katika hali hiyo, wanajamii huanza kusaka mtu wa kuwasemea, kwa sababu wao hawasikilizwi. Hofu hutawala nafsi zao, wakiogopa matokeo ya kusema ukweli au kuhoji uonevu na hivyo kubaki kimya huku wakimuachia Mungu aamue.
Hali hii hutokea mara nyingi katika jamii ambazo kuna kundi dogo la watu wanaojiona kuwa wao ndio wenye kauli ya mwisho.
Watu hawa hujihisi kuwa wako juu ya sheria, na wengine hawana haki ya kuuliza au kupinga maamuzi yao, hata kama yanawaumiza watu kiakili au kimaisha.
Baadhi yao huendelea kupanda ngazi hadi kuwa na kiburi na jeuri ya hali ya juu, hawasikilizi mtu yeyote, hata kama maamuzi yao ni ya kiholela, yenye sura ya dhulma, ujanja au hata wizi wa kisheria.
Katika Mji Mkongwe wa Zanzibar, hasa eneo la biashara la Darajani, yapo mambo mengi yanayofanyika ambayo yanaiumiza jamii. Yanatia huzuni na yanaonekana kuwa ni maonevu yanayozidi kuwakandamiza walioko katika hali ya umasikini.
Mambo haya yanalalamikiwa si mara moja au mara mbili, bali mimi mwenyewe nimeyaona kwa macho yangu mara nyingi.
Wanaoumia zaidi ni wafanyabiashara wadogo, wengi wao wakiwa ni watu kutoka Pemba. Najua baadhi ya watu hawatapenda kusikia hili, lakini kama hawataki jambo lijadiliwe hadharani, wasingefanya hayo maovu. Ukweli hausemwi kwa kumfurahisha mtu, bali kwa ajili ya haki.
Vitendo vinavyofanyiwa wafanyabiashara hawa haviendani na taswira ya Zanzibar kuwa ni jamii inayopendana na kuhurumiana.
Kinyume chake, vinaonesha dhulma na ubaguzi wa wazi. Hebu tazama mfano huu:
Baada ya sikukuu ya Idd el Fitr, kundi la vijana walioajiriwa na Mamlaka ya Mji Mkongwe, wakiwa na virungu na magongo, walivamia eneo maarufu la kuuza kofia Darajani. Waliwabomolea wafanyabiashara waliokuwa wamepanga kofia zao katika meza sita tofauti, wakazichukua zote.
Cha kushangaza, wafanyabiashara wengine waliokuwa jirani, wanaouza mikate, tende, sigara na vocha hawakuguswa hata kidogo.
Hili eneo limekuwa maarufu kwa zaidi ya nusu karne kwa kuuza kofia za mkono, na ni sehemu ambayo hata wageni huitembelea kutafuta kofia.
Wauzaji hao wana leseni halali za biashara, na mamlaka inajua wazi kuwa hawana maduka – biashara zao zinafanyika pembezoni mwa barabara.
Kila siku hulipa ada ya usafi wa mazingira, hata kama biashara yao haihusiani na uchafuzi wa mazingira.
Swali ni: Kwa nini ni wauza kofia tu walilengwa na wengine wakaachwa? Na zile kofia walizochukuliwa zilipelekwa wapi? Kama zilikamatwa kwa mujibu wa sheria, je, ni sheria ipi hiyo? Na kama zililenga tozo au faini, kwa nini hazikuhifadhiwa kwa njia itakayowezesha mmiliki kuzikuta tena?
Je, ni kigezo gani kilitumika kuamua kwamba hawa wauzaji wa kofia ndio pekee waliokiuka taratibu, ilhali wamekuwepo hapo kwa miaka mingi bila kuonywa au kuelezwa kuwa wanakiuka sheria?
Hii si mara ya kwanza. Kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu uvamizi wa bidhaa na kuvunjwa kwa meza za wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kama simu, dagaa, mikate na maandazi.
Wengi wao hawajawahi kurudishiwa mali zao, ambazo thamani yake hufikia maelfu ya shilingi.
Mamlaka ya Mji Mkongwe inapaswa kueleza wazi ni kwa nini vitendo hivi vinaendelea kufanyika.
Wapi zinapelekwa bidhaa zinazochukuliwa kwa nguvu? Na kama biashara ya wazi hairuhusiwi, kwa nini wanapokea ada ya leseni na usafi wa mazingira kila siku?
Hakuna ubishi kuwa ukusanyaji wa mapato ni muhimu kwa uendeshaji wa shughuli za Mamlaka na kwa hifadhi ya Mji Mkongwe, lakini namna ukusanyaji huu unavyofanyika hauonyeshi haki wala uadilifu.
Uonevu huu hauleti taswira nzuri, siyo kwa Mamlaka pekee, bali hata kwa Serikali nzima, Serikali ambayo imeahidi kuwaunga mkono wajasiriamali wanaofanya biashara halali ili kujikimu kimaisha.
Ni wakati sasa kwa viongozi wa Mamlaka kujitathmini. Wanapaswa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa vijana wanaopewa jukumu la kusimamia mazingira.
Haiwezekani mali za watu ziporwe kana kwamba wamezipata kwa njia ya wizi au uhalifu, ilhali wanachofanya ni kujitafutia riziki halali.