Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Gari ikigongwa na treni imekosea

Kuna hekaya zingine za utotoni tulizigundua ukubwani kuwa zilikuwa za kufikirika. Lakini zingine hadi leo zimetuachia maswali bila majibu. Kwa mfano hii inayodai kuwa treni ikigonga gari, gari ndiyo itakayoadhibiwa. Inaweza kuwa kweli kwa sababu reni haiwezi kutumia njia ingine zaidi ya reli, na reli haiwezi kutumika na chombo kingine cha usafirishaji.

Iwapo njia hiyo itatumika tofauti, basi itakuwa imeingiliwa na hatua ni lazima zitachukuliwa kwa chombo kilichoiingilia.

Hali hii ndiyo inayoonekana kwenye Hifadhi za Taifa. Haijalishi iwapo wakulima na wawindaji walifanya makazi hapo kabla ya msitu huo kutangazwa kuwa hifadhi, lakini wanatakiwa kukaa mbali sana ili kuwapisha viumbe wengine wanaopewa makazi hapo. Ni jambo jema kwa sababu shughuli za kibinadamu ndizo zinazoharibu mazingira kwa kiasi kikubwa na kutishia kutoweka kwa ikolojia katika sura ya nchi.

Kwa sheria ya nchini mwetu, ardhi ni mali ya Serikali. Hivyo Serikali ina mamlaka ya kubadili matumizi ya ardhi kwa jinsi inavyoona inafaa. Hivyo uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kimkakati lililoundiwa mamlaka zinazosimamia matumizi sahihi ya ardhi, kwani sisi sote tunayategemea mazingira bora katika maisha yetu na ya vizazi vyetu vinavyokuja.

Lakini kwa upande mwingine, ardhi inayohitajika kwa matumizi ya Serikali haiwafukuzi wenyeji. Hawa wanahamishwa au kutafutiwa makazi mengine kuyapisha matumizi mapya ya ardhi hiyo. Serikali kwa kushirikiana na mamlaka zake ina jukumu la kuhakikisha raia wanapata makazi bora na kuhakikishiwa usalama wao katika makazi yao mapya.

Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya wananchi wanaoishi jirani na hifadhi za Taifa kuingiliwa na viumbe waliopishwa kwenye hifadhi. Tembo wamekuwa mstari wa mbele kuhatarisha maisha ya wanavijiji, kuharibu mashamba hivyo kupelekea hatari ya janga la njaa. Wanafunzi wanaoishi katika maeneo hayo wanashindwa kwenda shule kwa kuhofia usalama wao. Watoto wakitoka ndani wanakutana na tembo milangoni.

Hili ni tatizo kubwa kwani binadamu na wanyama wa mwituni hawaelewani lugha. Watu wanaweza kuelewa wanapoambiwa kuwapisha wanyama, lakini wanyama hawawezi kuelewa wakiambiwa waachane na mashamba ya binadamu. Shida inakuwa kubwa kwa wanakijiji kwani wakulima wanakopa ili kuendeleza mashamba. Wanategemea kulipa mara wavunapo. Lakini tembo wanavuruga mashamba na kukatiza ndoto zao.

Mamlaka za hifadhi wanyama zinaelekeza lawama kwa wakulima zikidai kuwa wanavamia maeneo ya hifadhi. Lakini inawezekana mamlaka hizi hazijafanya utafiti na jitihada za kutosha katika suala hili. Zinakuwa kama zilizolala kusubiri maafa na kujibu kwa kutangaza fidia. Fidia ina maana gani baada ya ajali iliyosababisha ulemavu wa kudumu au upotevu wa maisha kwa ujumla?

Katika nyakati zilizopita tulisikia jinsi mababu zetu walivyokuwa wakiishi na wanyama wa msituni. Mababu hawa waliwalinda tembo na faru dhidi ya majangili waliojishughulisha na biashara haramu. Wenyewe walijua nyakati za kuongezeka au kupungua kwa wanyama, pengine mamlaka nazo zingejifunza mbinu za wazee hawa. Inawazekana mamlaka zetu zinashindwa kuhimili ongezeko la wanyama hawa.

Nilipokuwa mdogo nilimuuliza mwalimu wa Jiografia ni kwa nini simba na chui wanaruhusiwa kuwala wanyama adhimu kama twiga na pundamilia. Jibu alilonipa mwalimu lilinishangaza sana. Mwalimu aliniambia kuwa mnyama mmoja anapoliwa hufanya mwendelezo wa maisha mapya kwao. Kila wanapovamiwa hutawanyika kwenda kuanzisha familia mpya au kuchanganyika na jamii zingine na kufanya uzao mpya.

Inaonesha tembo wanajikuta wakiongezeka maradufu kwenye maeneo yao bila kudhibitiwa. Pengine ongezeko la wanyama hawa linasababisha upungufu wa mahitaji yao hifadhini. Hivyo wanalazimika kuyatafuta mahitaji kwa huvamia mashamba ya wanavijiji. Kwa wabongo treni ikigonga gari hutafsiriwa kuwa gari imegonga treni, hivyo tembo hawavamii kijiji bali wanavamiwa na wanakijiji.

Wakati fulani tulishuhudia wafugaji wakimla simba aliyekuwa na tabia ya kuvamia mazizi ya ng’ombe. Kwa akili ya haraka tukio la aina hiyo ni kama kutuma ujumbe kwa makundi ya simba. Na si ajabu wanyama hao wakali wakasogea mbali kwa woga wa kutendwa kama mwenzao. Wavuvi nao wameshawahi kuwala mamba na viboko waliowadhuru wavuvi wenzao kwenye harakati. Sababu ilikuwa kama ile; kutuma ujumbe.

Tatizo la tembo na wakulima sio chuki na uadui, bali kutoelewana tabia. Huku uswahilini watu humpeleka mwenzao kwenye vyombo vya sheria ili kumrekebisha tabia. Si kwamba hawampendi, bali wanahitaji arekebishwe ili waendelee kuishi naye. Lakini hutokea mara chache wahalifu (hasa walio kwenye makundi) wanagoma kurekebika. Hapa nasikitika kusema ndipo wanapoibuka “wananchi wenye hasira kali”, wakalimaliza tatizo kwa njia zao.

Kwenye hadithi moja niliyoipata wakati nikiwa mdogo, babu yangu mmoja aliyekuwa mwindaji alikuwa akigawana mawindo yake na fisi. Mwanzoni fisi hawa walikuwa na kawaida ya kuvamia mbuzi wa wafugaji pale kijijini. Lakini wakajenga tabia ya kumsubiri mzee alipotoka mawindoni, akawarushia pande la mnyama aliyempata. Fisi waliacha kuvamia mifugo na wafugaji wakawa na amani.

Nadhani mamlaka zingeruhusu wanakijiji kumla mmoja kati ya tembo waharibifu, pengine wengine wangepata ujumbe. Wanyama wana hisia za ndani sana, wanajua kuwa mwenzetu hapa ametowezwa. Hivyo wanaweza kuusoma ujumbe haraka na wakaufanyia kazi.