Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nafasi ya Afrika, wanawake kiti cha Katibu Mkuu wa UN

Mchakato wa kumtafuta Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa (UN), unaotarajiwa kukamilika mwaka 2026, tayari umeanza.

Kwa kuwa tuliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Machi 8, 2025, ulikuwa ni wakati mwafaka kutafakari juu ya ukweli kwamba katika kipindi cha miaka 80 ya uwepo wa Umoja wa Mataifa, hakuna mwanamke aliyewahi kuongoza taasisi hiyo kubwa duniani.

Ingawa kiongozi ajaye wa Umoja wa Mataifa atateuliwa mwaka 2026, ni muhimu kuanza kufikiria kuhusu aina ya uongozi utakaokuwa na uwezo wa kuendeleza misingi ya usawa, haki, pamoja na kukuza zaidi diplomasia duniani.

Katika kipindi hiki cha maandalizi, je, Afrika itatumia fursa hii kuonyesha nguvu yake ya umoja, au itaruhusu mgawanyiko na hatimaye kudhoofisha ushawishi wake?

Ingawa mada hii inaweza kutoendana na vipaumbele vya kisiasa vya sasa, athari zake ni bayana. Ni matumaini ya wengi kuwa kiongozi atakayechaguliwa ataleta mabadiliko chanya katika diplomasia ya kimataifa, kuongeza ushirikiano na kushughulikia changamoto kuu za wakati huu.

Ikumbukwe kwamba, mwaka 2014, kampeni ya “1 kwa bilioni 7” ilifanikiwa kushinikiza uwazi katika mchakato wa uteuzi wa Katibu Mkuu wa UN, na hivyo kufungua fursa ya mijadala ya umma.

Kampeni hiyo ilikuja baada ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuandika barua kwa wanachama wa Umoja wa Mataifa wakiomba kuwe na uwazi na mchakato shirikishi kwa wanachama wote ili kuwezesha utekelezaji wa mamlaka ya umoja huo.

Hali kadhalika, kampeni ya mrithi wake ya “1 kwa bilioni 8” inalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya kaulimbiu ya “Ni wakati sasa wa kuwa na Katibu Mkuu wa kwanza mwanamke mwenye mtazamo jumuishi wa kijinsia, anayewakilisha misingi ya haki na usawa.

“Kiongozi anayetambua changamoto za kisera na kimfumo dhidi ya wanawake, pamoja na uhusiano baguzi unaotokana na jinsia, rangi, tabaka na mambo mengine.”

Nafasi ya Afrika katika wakati huu muhimu haiwezi kupuuzwa. Ikiwa na mataifa 54, bara hili linawakilisha kundi kubwa zaidi la wapigakura katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).

Katika miaka ya hivi karibuni, Afrika imeonyesha nguvu yake ya pamoja, hasa kwa kufanikisha kupata kiti katika kundi la nchi za G20 kama Umoja wa Afrika. Hakuna bara lingine linalotarajiwa kushuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu kama Afrika katika miongo ijayo.

Hata hivyo, bara hili bado limeachwa nje ya uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa—kiashiria cha ukosefu wa usawa katika utawala wa dunia.

Mataifa wanachama wenyewe yameangazia suala hili kupitia Mkataba wa Mustakabali wa Dunia. Hii inafanya msimamo wa Afrika katika uchaguzi ujao kuwa wa umuhimu mkubwa zaidi.

Kwa kuungana na kumuunga mkono mgombea mmoja wa kike, viongozi wa Afrika wana nafasi ya kihistoria. Wanaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa mienendo ya mchakato huu.

Huu ni wakati wa bara hili kujidhihirisha kama nguvu yenye mshikamano, likiwa mfano wa mshikamano wa kweli. Tayari mataifa 10 ya Afrika yamesaini tamko la pamoja kuhusu uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi wa Umoja wa Mataifa.

Ni dhahiri kwamba, mataifa yaliyobaki yameashiria kutoa uungaji mkono kwa wazo la mwanamke kuwa Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa.

Huu ni wakati mwafaka, pia, kuanza kufikiria kuwa muhula wa Katibu Mkuu ajaye uambatane na mchakato wa mabadiliko na mageuzi ya sera muhimu, yakiwemo maboresho yaliyocheleweshwa kwa muda mrefu ya Baraza la Usalama na hatua za mwisho za kufufua Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.

Pia, atalazimika kushughulikia ukosefu wa usawa wa kimfumo ambao kwa muda mrefu umepuuza sauti za nchi maskini duniani.

Ni rai ya wengi kwamba kiongozi ajaye wa Umoja wa Mataifa aweke kipaumbele katika masuala haya.

Kwa miongo mingi, UN imekuwa ikiwahimiza wanachama wake kuweka mbele usawa wa kijinsia na kuhimiza uongozi wa wanawake.

Hata hivyo, licha ya kufanikisha usawa wa kijinsia katika ngazi za juu za Umoja wa Mataifa, bado nchi wanachama hawajawahi kumteua mwanamke kuwa kiongozi mkuu wa taasisi hiyo.

Ikiwa mataifa yote ya Afrika yataungana kumuunga mkono kiongozi mwanamke mwenye sifa stahiki, yanaweza kuonyesha kwa vitendo misingi ya haki, ujumuishi na usawa inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Kumchagua mwanamke kuchukua majukumu ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa itakuwa hatua muhimu kuelekea usawa wa kijinsia ndani ya taasisi hiyo na alama yenye nguvu kwa uongozi wa wanawake duniani.

Viongozi wa kike huleta mtazamo wa kipekee, wakipinga vikwazo vya kimfumo na kukuza sera jumuishi katika sekta mbalimbali, hatua ambayo hatimaye inanufaisha pande zote.

Kiongozi mwanamke ataimarisha mamlaka ya kimaadili ya Umoja wa Mataifa katika masuala kama haki za wanawake, usawa wa kijinsia, na haki za kijamii.

Katika kipindi hiki cha changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinawaathiri zaidi wanawake, na migogoro inayoendelea kuongezeka, unahitajika mshikamano, ubunifu, na Umoja wa Mataifa wenye ufanisi zaidi.

Wakati Marekani na Ulaya zikijikita zaidi katika siasa za kitaifa na kujitazama kibinafsi, majukumu ya kuendesha mchakato wa mageuzi ya taasisi za kimataifa yatahitaji kuongozwa na maeneo mengine ya dunia, hususan Afrika.

Zaidi ya hayo, hatua hii itazipa motisha kanda nyingine duniani kutathmini upya umuhimu wa kuwa na wagombea wanaotanguliza mbele usawa na ushirikiano wa kimataifa badala ya maslahi ya kitaifa.

Pia, itatoa ujumbe mzito kuwa Afrika, ambayo mara nyingi huelezwa kama mpokeaji wa uamuzi wa kimataifa, sasa ni chombo cha mabadiliko katika usimamizi wa dunia.

Haya yote yanahitaji dhamira ya kisiasa na mshikamano. Viongozi wa Afrika wanapaswa kuweka kando tofauti zao na maslahi binafsi na kuungana katika kumuunga mkono mgombea mwanamke mwenye maono anayewakilisha matarajio ya bara hili na malengo mapana ya nchi maskini na zinazoendelea.

Ni imani yetu kuwa mchakato huu wa uchaguzi kwa ngazi ya Umoja wa Mataifa utaimarisha zaidi ushawishi wa Afrika unaokua katika siasa za kimataifa.

Zaidi ya yote, Katibu Mkuu ajaye wa kike anaweza kuongoza kwa mtazamo mpya na jumuishi, unaoakisi mahitaji ya watu zaidi ya bilioni nane duniani. Uamuzi ni dhahiri. Viongozi wa Afrika wanapaswa kuchukua hatua sasa kwa mshikamano, ujasiri na mtazamo wa maendeleo.

Imeandikwa na mjumbe wa kamati ya uongozi ya kampeni ya “1 kwa bilioni 8”, Gabriela Keseberg Dávalos, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Fortunata Makene na mtafiti wa taasisi hiyo, Richard Ngilangwa.