Mwalimu aahidi mageuzi miundombinu ya masoko Dar
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Salum Mwalimu akimwaga sera kwa wananchi wa Msasani jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Mgombea huyo amesema hali ya sasa ya masoko ya bidhaa za vyakula na magulio jijini humo ni ya kusikitisha, akiahidi kuyageuza kuwa ya kisasa na yenye mazingira bora ya biashara ili kulinda usalama wa wafanyabiashara na walaji.
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kufanya mageuzi makubwa ya miundombinu na masoko jijini Dar es Salaam endapo atachaguliwa kuwa Rais, Oktoba 29, 2025.
Amesema hali ya sasa ya masoko ya bidhaa za vyakula na magulio jijini humo ni ya kusikitisha, akiahidi kuyageuza kuwa ya kisasa na yenye mazingira bora ya biashara ili kulinda usalama wa wafanyabiashara na walaji.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Msasani Sokoni, leo Oktoba 10, 2025 wa kushawishi umma kuchagua kushika wadhifa huo, Mwalimu ameeleza kusikitishwa kwake na hali ya sasa ya masoko na magulio jijini humo, akisema:
“Dar es Salaam inakuwaje na soko la namna hii kama hili la Msasani? Alafu kinauzwa bidhaa za chakula, katika utawala wangu sitakubali, nikichaguliwa, naenda kujenga upya. Naona Dar es Salaam kuna magulio mengi, mbona ni uchafu? Nikiingia madarakani nitajenga masoko ya kisasa na miundombinu inayofikika haraka kama barabara safi za kutoka na kuingia,” amesema.
Mwalimu amesema kuwa kwa hadhi ya Dar es Salaam inapaswa kuwa jiji la fursa na kwamba ni muhimu wananchi kuchagua viongozi wenye sera mbadala, makini na wenye maono ya kubadilisha na kujenga taswira ya kweli.
“Maisha ya sasa yanapaswa kuongozwa na vijana wenye kasi na morali ya kutosha, haiwezekani masoko mengi hayana hadhi halafu kila uchwao masoko yanaripotiwa kuungua moto hii haikubaliki, tupeni Serikali Chaumma tukafanye mageuzi,” amesema.
Dorcus Francis, mgombea ubunge wa Kawe kupitia Chaumma, ameahidi kuwainua vijana kiuchumi kwa kutoa mikopo ya riba nafuu, pamoja na kuboresha soko la samaki la Msasani kwa kutumia mapato yanayokusanywa na halmashauri.
“Nahitaji kuona soko hili linakuwa safi na miundombinu bora inayofikika kirahisi,” amesema Dorcus.
Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema amesema chama hicho kimejipanga vema kuleta mabadiliko ya kweli nchini kwa kuwasilisha mgombea wa urais kijana, mwenye sifa, na maono makubwa kwa taifa.
Mrema amesema kuwa licha ya kuwa na mgombea kijana, chama pia imekuja na sera makini na thabiti zinazolenga kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini na kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
“Tuna sera nzuri zenye kujibu changamoto za Watanzania, kazi iliyobakia ni Watanzania kupiga kura kwa wingi ili Mwalimu achaguliwe,” amesisitiza Mrema, akimaanisha mgombea wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Mrema, chama hicho kinaamini kuwa mustakabali wa taifa uko mikononi mwa vijana na viongozi waadilifu na kwamba chama hicho ni mbadala sahihi kwa Watanzania wanaotafuta mabadiliko ya kweli.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Masoud Mambo amesema chama hicho kimepitisha makada wenye uwezo, uadilifu na sifa zinazostahili ili kuwatumikia wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Mambo amesema hatua hiyo inalenga kuleta mabadiliko ya kweli kwa kutumia sanduku la kura kama chombo cha demokrasia.
“Kikubwa, wananchi tuungane kwa pamoja na kuwaunga mkono. Tukawawakikishe kwenye vyombo vya maamuzi. Wenzetu waliokuwa na dhamana kwa miongo sita sasa wameshindwa. Tunahitaji kutumia fursa hii ya kupiga kura ili kubadilisha maisha yetu,” amesema Mambo.
Amesisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika mageuzi ya kisiasa na kijamii na kwamba ni wakati wao sasa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono harakati za kuleta mabadiliko kupitia viongozi wapya waliopitishwa na chama hicho.
Amesema chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuwapa kipaumbele wagombea wanaotokana na makundi ya vijana na wanawake, kikieleza kuwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuleta usawa na maendeleo ya wote.