Mbunge akataa kura za kuongezewa kwenye sanduku

Mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodemus Maganga akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Serikali katika ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa Fedha wa 2025/2026 leo Jumanne Machi 15, 2025 bungeni, Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Ni joto la kuelekea uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM na kisha uchaguzi mkuu ambapo Mbunge Maganga anasema lazima haki itendeke ili waliochaguliwa kihalali watangazwe kwa wananchi.
Dodoma. Mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodemus Maganga amewataka wasimamizi wa uchaguzi mkuu kutenda haki ili watoe matokeo sahihi bila kuongeza kura wala kupunguza.
Maganga amesema mgombea akipewa kura sahihi kwenye uchaguzi itasaidia Taifa kuwa na viongozi sahihi wenye hofu ya Mungu kuliko kama watapatikana viongozi watakaopita kwa nguvu ya wasimamizi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 15, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu katika mwaka wa fedha 2025/26 ambayo inahitimishwa leo.
“Nawaomba wasimamizi wetu, kama kura zangu hazikutosha naomba uziache kama zilivyo, usiongeze ili niwe na nyingi na zikiwa nyingi naomba msipunguze bali tangazeni kama zilivyo ili tutende haki,” amesema Maganga na kuongeza,
“Maandiko yanasema kuwa, haki huinua Taifa, lazima tutende haki katika maeneo yote, wasimamizi wa kura nawaomba muwe makini na muwe na huruma na haki za watu msije kwenye kutenda kinyume,” amesema.
Amesema fomu zitachukuliwa na wananchi watachagua nani wanamtaka ambaye ana sifa za kuwatumikia na nani ambaye anajipeleka lakini akawataka vijana kujitokeza kwa wingi zaidi ili kuingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
Mbunge huyo ameonya pia suala la rushwa kwa wagombea akizitaka mamlaka zinazohusika ziendelee kuwafuatilia watu wanaotoa rushwa kwenye chaguzi zote ili waweze kuwashughulikia kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.
Kwa mujibu wa Maganga, kinachotakiwa ni haki kwenye suala zima la uchaguzi lakini akasisitiza kuwa wale ambao hawatapenda kutoa haki, atakuwa mstari wa mbele kuitafuta haki kwa namna yoyote ili baada ya kuipata ndipo suala la amani litafuata.
Katika hatua nyingine amewaomba wabunge wenzake kujipa moyo kwani Bunge likimaliza muda wake lazima watakwenda kwa wananchi kwa ajili ya kutetea nafasi zao akiwasihi wakapambane kikamilifu ili waweze kuzipata nafasi hizo.
Kauli ya mbunge huyo inafanana na kauli zilizowahi kutolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali wakidai kwamba kuna mbinu huwa zinafanyika kuwatangaza washindi wa uchaguzi, na siyo kwa kura zinazopigwa na wananchi.
Itakumbukwa kwamba Septemba Mosi, 2024, katika picha jongefu ya dakika 1.32, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marco Ng’umbi alisikika akiwaeleza watu aliowataja mara kadhaa kuwa ni madiwani kwamba ushindi wao katika uchaguzi huo si ujanja wao, bali ni nguvu ya Serikali.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza hata waliopita bila kupingwa ni kazi iliyofanywa na Serikali na sio ubora wa wagombea husika.
Alisema mazingira ya mwaka 2020 hayakuja yenyewe moja kwa moja kwa sababu wao walikuwa wagombea bora sana. Alidai kwamba Serikali ndiyo iliyoifanya kazi kwa baadhi yao kupita bila kupingwa. Alisisitiza kwamba na yeye alihusika majimbo fulani.
Vilevile, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akiwa Bukoba, alisikika kwenye kipande cha video kilichosambaa mitandaoni akisema matokeo ya kura siyo lazima yawe ya kwenye boksi, bali inategemea na anayetangaza matokeo.
Katika maneno yake, Nape alisema: “Kashai oyee! Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe yale ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza… na kuna mbinu nyingi, kuna halali, kuna nusu halali na haramu na zote zinaweza kutumika, ilimradi tu ukishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe.”
Wazungumzia kauli hiyo
Mwanazuoni wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Matrona Kabyemela amesema kauli ya mbunge huyo ni njema iliyojengwa kwenye muktadha wa demokrasia ya vyama vingi na kwenye imani za wananchi.
“Lakini kutenda haki au la kunaandamana na sheria za nchi na utekelezaji wake. Kwa Tanzania, Katiba yetu bado ina matundu ambayo yanaweza kupenyeza vitendo vya kukiuka haki za uchaguzi,” amesema.
“Kwa hiyo, kwa mtazamo wangu, kauli tu haiwezi kuleta mabadiliko yoyote, lakini aliyeongea kwa kuwa alipitia mchakato nadhani anatutafakarisha kuwa kuna muda vyombo vya uchaguzi huwa vinabadilisha matokeo bila kuionea jamii huruma,” amesema na kuongeza:
“Mabadiliko yanahitajika lakini yatumie busara ya kimazingira na tutafika kwani hata Roma haikujengwa siku moja,” amesema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza amesema kauli yake hiyo haina maana yeyote na haiwezi kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na walio wengi.
“Uchaguzi unaongozwa na sheria, kanuni, Katiba na mamlaka zilizowekwa chini ya Tume ya Uchaguzi, hayo ni maneno tu ya kukosa cha kusema, haiingii kwenye maandishi wala kubadilisha maandishi, sheria wala kanuni, kifupi haina maana,” amesema.
Kwa mujibu na Kaiza amesema haiwezi kuchagiza chochote ingekuwa jambo la maana iwapo angewasilisha muswada binafsi bungeni wa kufanya mabadiliko, zaidi ya hapo alikuwa anajifurahisha aonekane kazungumza.