Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapito ya miaka 48 CCM yenye majaribu ya nyakati

Kuelezea Chama cha Mapinduzi (CCM), kilivyoweza kutimiza umri wa miaka 48, kikiwa madarakani, inavutia kukopa kifungu cha maneno ya Kiingereza “stand the test of time” – “kuvuka majaribu ya nyakati.”

Hakika, bila ubishi, “CCM has stood the test of time” – “CCM imesimama imara kwenye mitihani yote ya nyakati.” Iwe kwa kuumiza wasio na hatia au kupitia matendo ya haki, CCM imemudu kubaki salama kwa miaka 48.

Kutoka mtihani wa Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi mwaka 1984 mpaka Edward Lowassa mwaka 2015. Makabidhiano ya madaraka kutoka Mwalimu Julius Nyerere kwenda Ali Hassan Mwinyi hadi Dk John Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan. Inatosheleza tafsiri kuwa chama kimevuka majaribu mengi ya nyakati.

Harakati za wana-CCM Zanzibar nyuma ya madai ya uwepo wa mpango wa kuuvunja Muungano na dhoruba la mpasuko visiwani mwaka 1988, lililosababisha aliyekuwa Waziri Kiongozi, Seif Sharif Hamad, kuvuliwa uanachama na kufungwa jela, mpaka vuguvugu la G55, ambalo lilihusisha wabunge wa Tanzania Bara, walioidai Tanganyika ndani ya Tanzania.

Kutoka Februari 5, 1977, CCM ilipozaliwa baada ya kuunganisha vyama vya Tanu na ASP hadi Februari 5, 2025, ni miaka 48 iliyotimia. Ni siku 17,532 zenye matukio makubwa ya kisiasa. Kuvunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, kisha kuiunda tena mwaka 2000.

Vita ya Kagera, Tanzania dhidi ya Idi Amin, Uganda, iliyoanza mwaka 1978 na kumalizika mwaka 1979. Mpango wa mapinduzi ya Serikali, kumwondoa madarakani Mwalimu Nyerere mwaka 1984, halafu wasiwasi mkubwa baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa.

Haikuwa rahisi mwaka 1984, Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) CCM, ilipomvua nyadhifa zote aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Aboud Jumbe. Sababu ilikuwa mapambano ya kuukabili uasi dhidi ya Muungano.

Jumbe, mwasisi mwenza wa CCM, alituhumiwa kisha akakutwa na hatia ya kukutwa na mapendekezo ya rasimu ya Katiba, yenye kutaka Muungano wa serikali tatu. Akavuliwa urais na umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, urais wa Zanzibar na uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, vilevile umakamu Mwenyekiti CCM.

Kumpata Ali Mwinyi, kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ulikuwa mtihani mwingine. Hata sababu ya Mwinyi kupewa nafasi ni kwa kuwa hakuwa na kundi. Zanzibar, hasa CCM, ilikuwa ikisumbuliwa na makundi kwa kiasi kikubwa.

Mwinyi alionekana kuituliza Zanzibar. Hata hivyo, alipoondoka, mchuano baina ya Rais wa Nne wa Zanzibar, Idris Abdulwakil, na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Maalim Seif, ulidhihirisha kwamba hali ya kisiasa ndani ya CCM, ilikuwa bado mbaya upande wa Zanzibar.

Mwalimu Nyerere alipokuwa anajiandaa kuachia madaraka ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1985, alikuwa na karata mkononi. Ni jina la Dk Salim Ahmed Salim. Alitaka ndiye awe mrithi wake wa kiti cha urais. Nec CCM walimgomea.

Wajumbe wa Nec CCM kwa sauti moja, walipinga Dk Salim kuwa Rais wa Tanzania mbele ya Mwinyi, kwa hoja ya uandamizi. Walisema, Mwinyi, kwa kuwa alikuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania, alikuwa mwandamizi kuliko Salim. Mwalimu Nyerere aliamua kuondoa karata yake, Nec ikashinda. CCM ikavuka salama.

Mwinyi, kupitia kitabu chake “Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha Yangu”, amesimulia kuwa baadhi ya wazee wa Zanzibar walimgomea Mwalimu Nyerere kumfanya Dk Salim kuwa Rais wa Tanzania kwa tuhuma kwamba alihusika na kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, na kwamba huwa hasemi “Mapinduzi Daima”.

Uchaguzi Mkuu 1995, CCM walikutana na joto kali. Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kigoma Malima, alijiengua kwenye chama hicho na kujiunga na chama cha NRA. Kada mashuhuri, aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, Augustino Mrema, alihamia NCCR-Mageuzi.

Haitoshi, Mrema alisimama kama mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi, hivyo kufanya mchuano kuwa mkali dhidi ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa. Hata kipindi cha uteuzi wa mgombea urais CCM, chama hicho kilipitia majaribu ya nyakati.

Kitendo cha kumkata Lowassa kwenye mbio za urais mwaka 1995, kilizua zogo, hadi Mwalimu Nyerere alilazimika kutoa ufafanuzi. Msimamo wa Mwalimu Nyerere wa kuondoa jina la John Malecela katika orodha ya wagombea wa CCM, ulisababisha mtafaruku.

Mwalimu Nyerere alilazimika kurudisha kadi ya uanachama CCM, baada ya kuona wajumbe wanamgomea kumwondoa Malecela. Ni Malecela aliyeamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro ili kunusuru Baba wa Taifa asijivue uanachama CCM. Hili pia CCM walilivuka salama.

Uchaguzi Mkuu 1995, uliipa CCM hekaheka nyingine kwenye hatua ya mwisho, ya Mkutano Mkuu, uliochagua jina la mgombea urais. Jakaya Kikwete aliongoza kwa kura dhidi ya Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya.

Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM, alitangaza kuwa Kikwete hakuvuka asilimia 50 ya kura, hivyo uchaguzi ungerudiwa dhidi yake na Mkapa aliyetoka wa pili, ili kumpata mgombea. Uchaguzi uliporudiwa, Mkapa alishinda.

Ushindi wa Mkapa ulisababisha kinyongo kwa timu ya Kikwete, iliyoamini ilishinda ila ilidhulumiwa. Kundi kubwa CCM lilimshawishi Kikwete kuhama chama. Ni Kikwete aliyesambaratisha mipango yote baada ya kutoa hotuba ya kihistoria kumuunga mkono Mkapa na kuomba timu yake yote iwe ya mgombea wao, Mkapa.

Mwaka 2010, mipango mingi iliratibiwa kuibomoa CCM. Aliyekuwa Mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe, alihamia kilichokuwa chama kipya, CCJ, kipindi cha mwisho cha ubunge wake. Halafu Mpendazoe alihamia Chadema na kugombea ubunge jimbo la Segerea, Uchaguzi Mkuu 2010.

Mpendazoe alitoboa siri kuwa uhamaji wake kutoka CCM, ulikuwa mpango mkubwa wa wabunge wengi CCM kuhamia CCJ, kisha Chadema. Alisema kuwa alisalitiwa na wenzake, akajikuta ni yeye tu aliyehama. Jaribio hili pia CCM walilivuka salama.

Uchaguzi Mkuu 2015, Lowassa aliibua hekaheka kwa sehemu kubwa, vilevile aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe. CCM iligawanyika. Kuelekea kumpata mgombea urais, Lowassa alikatwa. Nec CCM ilichafukwa. Wajumbe waliimba wana imani na Lowassa.

Pamoja na hivyo, CCM walifanikiwa kumsimika mgombea urais, Dk Magufuli. Lowassa alihamia Chadema, akafuatwa na wana-CCM waandamizi wengi, akiwemo Waziri Mkuu wa Saba wa Tanzania, Fredrick Sumaye.

Balozi Juma Mwapachu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Milton Makongoro Mahanga, Naibu Waziri wa Kilimo, Goodluck Ole Medeye, kutaja wachache, walihama CCM, kumfuata Lowass.

Wajumbe wa Kamati Kuu CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), walitangaza hadharani kujitenga na uamuzi wa CCM, kuelekea kumpata mgombea urais 2015.

CCM walivuka Uchaguzi Mkuu 2015. Magufuli alitangazwa mshindi wa kiti cha rais dhidi ya Lowassa, aliyegombea kwa tiketi ya Chadema. Baada ya uchaguzi, kuna wana-CCM waandamizi walifukuzwa uanachama kwa kukisaliti chama kwenye uchaguzi.

Waliofukuzwa uanachama ni Sophia Simba, waliokuwa wenyeviti wa CCM mikoa, Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Jessica Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara).

Nchimbi, Kimbisa na aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke, walisamehewa na kupewa onyo kali. Hili pia CCM walilivuka. Si miaka 48 ya lelemama. Chama kimevuka mabonde na milima.

Desemba 2019, CCM ilitikiswa na wazee wenye heshima kubwa, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, ambao wote, kwa nyakati tofauti, wamepata kutumikia ukatibu mkuu wa chama hicho. Kinana na Makamba, waliandika waraka wakikishutumu chama hicho kukaa kimya kipindi wao wakishambuliwa na mtu anayeitwa Cyprian Musiba.

Pamoja na kila kilichotokea, CCM ilivuka, kama ilivyoweza kumkabili Dk Mohammed Gharib Bilal, aliyetaka kumpa changamoto aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume, katika Uchaguzi Mkuu 2005, kisha Gharib akawa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Machafuko ya kisiasa Januari 26 na 27, 2001, Dar es Salaam na Zanzibar, yaliyosababisha vifo vya makumi na mamia kuwa wakimbizi, ni sehemu ya historia ya CCM kwa miaka 48, kwamba chama hicho kimevuka majaribu mengi ya nyakati.

Rais kufa madarakani, ilitokea mara ya kwanza baada ya Tangazo la Rais Samia Machi 17, 2021 kuwa aliyekuwa Rais, Dk Magufuli, alifariki dunia. Rais Samia, ambaye alikuwa Makamu wa Rais, alikula kiapo kuongoza nchi, kikatiba.



Kwa macho ya wengi, ilionekana Rais Samia aliingia ofisini kwa njia ya amani. Hata hivyo, Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo, baadaye alisimulia kuwa “kuna watu walisahau Katiba”, kwamba kulikuwa na kusita kumkabidhi Rais Samia ala ya uongozi wa nchi, mpaka yeye (akiwa mkuu wa majeshi), alipowakumbusha kufuata Katiba.

Hili pia CCM walivuka salama. CCM ni mtoto aliyezaliwa baada ya Tanu na ASP, ambavyo kila kimoja kina historia ya mitikisiko. Tanu, mapambano ya Oscar Kambona dhidi ya Mwalimu Nyerere, uasi wa jeshi mwaka 1964 na jaribio la mapinduzi mwaka 1969, wakati ASP, Aprili 7, 1972, Rais Karume aliuawa akiwa madarakani.

CCM, miaka 48, kimebaki kuwa chama kikongwe Afrika. Kinaongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ushirika. Lawama dhidi yake ni nyingi kuwa kinaminya demokrasia na kinashinda uchaguzi kwa nguvu ya dola, lakini mitihani mingi ni uthibitisho kuwa kimeonja majaribu ya nyakati na kuvuka salama.