Prime
KONA YA MALOTO: Muda wa kuyatazama matukio haya ya utekaji kwa jicho la sayansi kali

Kabla ya Novemba 2016, Tanzania haikuwa na historia endelevu ya utekaji na upotevu wa raia. Yalikuwepo matukio machache, na matumaini ya wananchi yalikuwa kwa polisi.
Ghafla, mwaka 2016 ukielekea ukingoni, hali ilibadilika. Tukio lilikuwa moja, yakafuata mengine. Miaka tisa baadaye, inakuwa mazoea, watu kupotea au kuuawa, kisha taifa linasahau.
Ni miaka minane na miezi sita tangu Ben Saanane atoweke. Hajulikani alipo. Yu hai au la! Waliohusika na kupotea kwake hawajakamatwa.
Hawajulikani. Ni watu wasiojulikana. Ni hadithi isiyo na hitimisho. Naweza kubet kuwa familia ilishakata tamaa.
Inawezekana, ikitokea Ben akarejea leo, familia yake badala ya kushangilia kumwona, watakimbia kwa kudhani ni mzimu. Inaumiza sana, mtu uliyempenda, atoweke bila maelezo. Unaanza kuishi kwa kuweweseka, usijue atarudi lini, au uweke matanga na kusahau.
Miaka saba na miezi sita imepita, tangu mwandishi Azory Gwanda atekwe. Hajulikani alipo. Waliomteka hawajakamatwa. Hawajulikani. Ni watu wasiojulikana. Kutoweka kwa Azory imekuwa sawa na riwaya za nyakati za ujima.
Miaka saba na miezi 10 imepita tangu aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye, atekwe. Hajulikani alipo. Waliomteka ni watu wasiojulikana.
Upatikanaji wake ni hadithi tu! Miaka minane imepita tangu mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzake watatu watekwe kisha kupatikana baada ya siku tatu. Waliowateka ni akina nani? Mpaka leo ni hadithi tu!
Miaka saba imepita tangu mfanyabiashara Mohammed Dewji “Mo” alipotekwa. Watekaji walimtelekeza Gymkana, Dar es Salaam.
Akina nani walimteka? Polisi walitoa ripoti ambazo hazikukidhi hata kidogo. Ilisababisha Rais wa Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli, aseme: "Watanzania siyo wajinga.” Kauli ya Magufuli haikufanya polisi warudi nyuma na kujibu maswali ya msingi kuhusu kupotea kwa Mo.
Mamia ya watu wamepotea Kibiti, Mkuranga, Rufiji na Kilwa. Aliyekuwa mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Bungara “Bwege”, alisema bungeni kuwa watu walichukuliwa na polisi lakini vituoni nchi nzima hawapo. Maiti nyingi zikaokotwa Mto Ruvu na fukwe za Bahari ya Hindi. Waliokufa na waliosababisha vifo ni watu wasiojulikana.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka, na wenzake, Jacob Mlay na Frank Mbise, wamebakiza miezi mitatu watimize mwaka mmoja.
Imebaki miezi minne utimie mwaka mmoja tangu aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao, ashushwe kwenye basi, eneo la Tegeta, Dar es Salaam, alipokuwa akisafiri kuelekea Tanga, kisha akakutwa ameuawa Ununio, Dar es Salaam.
Leo habari kubwa ni kutekwa au kuchukuliwa kwa nguvu kutoka nyumbani kwake, kada wa Chadema, Mdude Nyagali “Mdude Chadema”. Wasiwasi ni mkubwa kuhusu usalama wa Mdude. Je, atarudi au itakuwa hadithi kama ya Ben na Azory? Itakuwa kama Kibao? Mungu aepushe mbali.
Hii si mara ya kwanza kwa Mdude kutekwa. Ilitokea Mei 2019. Alichukuliwa na watu wenye bunduki. Baadaye iligundulika alikuwa kwenye mikono ya polisi.
Miaka sita baadaye, hadithi ni mpya. Je, yatajirudia ya Mei 2019 au ni mwanzo mpya wa msako usio na majibu wala usioeleweka? Tuombe Mungu Mdude apatikane.
Kipindi hiki cha wasiwasi mkubwa baada ya Mdude kutekwa, ni muda wa kutafakari mwanzo wa matukio ya utekaji na uelekeo wake.
Kwa nini yalianza na inakuwaje yanaendelea kutokea? Masilahi ya utekaji yalikuwa nini kipindi yanaanza, na sasa ni yapi?
Bahati mbaya waliomteka Ben, hawakuwahi kujulikana, kwa hiyo inawezekana ndiyo wanaohusika na kunyakuliwa Mdude. Kama ambavyo waliomuua Kibao ni kitendawili tata kukitegua, si ajabu ndiyo watekaji wa Mdude.
Usiku wa juzi nikiwa usingizini, niliota nazungumza na mtu mwenye kinyago. Mtu yule aliniuliza; zama zinabadilika, utawala unapishana, watendaji wanatoka na kuingia wapya lakini matukio ya utekaji yanaendelea. Sababu ni nini?
Nilichelewa kujibu kwa sababu sikuwa na jibu lililonyooka. Yule mtu aliniuliza tena; kama watekaji na wauaji walifanya kipindi cha utawala mmoja na hawakukamatwa wala kubainika, baada ya mabadiliko ya uongozi kama matukio hayo yangekoma, je, haitaonekana aliyepita ndiye mhusika na mpya ni mwema?
Nilijibu kwa kutikisa kichwa. Akaniuliza tena; watekaji na wauaji ambao hawakukamatwa, inashindikana vipi kuendeleza vitendo hivyo vya kinyama ili ionekane ndiyo tabia ya nchi, aingie mtawala mmoja au mwingine?
Maswali ya mtu yule yalitaka tutafakari sana nje ya sanduku. Ufumbuzi wa matukio ya utekaji unahitaji tafakuri ya kisayansi.
Huwezi kuwaza kawaida na kupata majibu ya uhakika kwa sababu watekaji wanatumia sayansi kufanya uhalifu wao.
Tazama watu wanaotekwa au kuuawa. Ni wale wakosoaji wa serikali au wenye nasaba za upinzani.
Kwa vyovyote, watekaji au wauaji hupiga hesabu za kisayansi na kuwagusa wale ambao ama hufanya umma uichukie dola au wananchi kukosa imani dhidi ya Serikali.
Agent provocateurs ni watu maalumu ambao hujituma au hukodiwa kutimiza lengo la uchochezi.
Kama lengo ni kutaka kuzionesha jamii za ndani na zile za kimataifa kuwa Serikali haina misingi ya haki za kibinadamu, inaua na kuteka watu, wanaweza kutumika kufanya utekaji na kutekeleza mauaji dhidi ya watu wanaoonekana ni kinyume na mamlaka za nchi.
Matokeo yake, anauawa Kibao, moja kwa moja Serikali inalaumiwa. Soka, Mbise na Mlay, mtuhumiwa mkuu inakuwa dola. Kama ilivyotokea alipotekwa Edgar Mwakabela “Sativa”, Dar es Salaam na kutupwa porini Katavi, umbali wa za zaidi ya kilomita 1,000. Serikali ililaumiwa tu.
Inahitajika sayansi kujua kiini cha utekaji na sababu za mauaji. Je, agent provocateurs wapo ndani ya Serikali, wakiwa na malengo ya kupanda vyeo au ni watu nje ya mfumo? Kama ni nje ya mfumo, je, walishakuwemo ndani kisha wakatupwa?
Yupo mtu anawaza, serikali inaposhutumiwa kila siku, je, taifa linaongozwa na chinjachinja? Mwingine anayeamini wauaji na watekaji ni watu nje ya serikali, je, ni raia wa Tanzania wanaoteka na kuua ndugu zao au watu wa mataifa mengine wanaishambulia nchi?