Kagame kuhitimisha kampeni leo, atabiriwa kushinda kwa kishindo

Muktasari:
- Kagame mwenye umri wa miaka 66, anagombea nafasi hiyo kwa mara ya nne. Kwa mara ya kwanza aliingia katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2000 na akaibuka na ushindi na baada ya hapo aligombea tena mwaka 2003, 2010 na 2017 na katika chaguzi zote hizo, Kagame amekuwa akiibuka na ushindi wa kishindo.
Kigali. Wakati Rwanda ikitarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu Jumatatu Julai 15, 2024 kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, mgombea wa chama cha FPR, Paul Kagame ambaye pia ni Rais wa nchi hiyo, anahitimisha kampeni zake leo Jumamosi, Julai 13, 2024 katika viwanja vya Kicukiro, Gahanga jijini Kigali.
Kagame mwenye umri wa miaka 66, anagombea nafasi hiyo kwa mara ya nne. Kwa mara ya kwanza aliingia katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2000 na akaibuka na ushindi na baada ya hapo aligombea tena mwaka 2003, 2010 na 2017 na katika chaguzi zote hizo, Kagame amekuwa akiibuka na ushindi wa kishindo.
Itakumbukwa Kagame kabla ya kuwa rais , alifanikiwa kuchukua mamlaka kama kiongozi wa kundi la waasi la nchi hiyo lililochukua mamlaka na kufanikiwa kumaliza mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Kipindi hicho, Kagame alikuwa makamu wa rais na kiongozi mkuu kutoka mwaka 1994 hadi 2000.
Jumatatu Wanyarwanda wanapiga kura katika uchaguzi ambao bila shaka Kagame ataibuka na ushindi kwa mujibu wa baadhi ya Wanyarwanda waliozungumza na Mwananchi leo Jumamosi akiwamo Emmanuel Gachume ambaye amesema; “Kagame hana upinzani, kila mtu hapa Rwanda bado anaamini katika uongozi wake.”
Wakati Gachume akiyasema hayo, Intozya Kugenzule amesema mabadiliko ya Katiba yanampa mgombea huyo nafasi ya kugombea kwa vipindi vingine vya miaka mitano.
“Mmm sijui kama wapinzani watamuweza, kwa sababu wananchi bado wana imani naye, ameifanyia nchi mambo mengi makubwa kwa muda mfupi na sasa Rwanda yetu tunajiona na sisi ni watu wengine, hasa vijana, anawapa nafasi sana za kujitafutia maendeleo,” amesema Kugenzule.
Katika uchaguzi huu, Kagame anapambana na Frank Habineza wa chama cha Democratic Green na mgombea huru, Philippe Mpayimana.
Akizungumza na vyombo vya habari jana jioni, Mpayimana alisema licha ya kuwa ni mara yake ya kwanza kugombea nafasi hiyo, amesema umefika muda kwa wananchi kuamua kubadili uongozi wa Rais Kagame.
“Sina wafuasi, lakini wafuasi ndiyo kama nyie waandishi wa habari, hawa wananchi mnaowaona hapa, ndiyo mtakaounda serikali, ifike mahali sasa na sisi wazawa tupewe nchi tuongoze, (bila kufafanua anamaanisha nini), hatuwezi kuongozwa miaka yote na watu kutoka mbali,” amesema Mpayimana.
Kaatika uchaguzi wa mwaka 2017, Rais Kagame alipata takribani asilimia 99 ya kura zote, hali ambayo inaelezewa huenda ikajirudia tena katika uchaguzi huu.
Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa habari zaidi.