Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jumuiya ya Wazazi CCM, yajitenga na kauli ya Simai kuhusu Yuda

Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM Taifa, Fadhili Maganya akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Juni 4, 2026 kuhusu maadhimisho ya siku ya wazazi yatakayofanyika mkoani Mwanza Julai 4, 2026. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa maoni ya mtu mmoja hayawezi kuwakilisha msimamo rasmi wa chama na kitaendelea kuwa imara licha ya kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya viongozi wake.

Dodoma. Kauli ya mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mohamed Simai Said mbungeu kudai kwamba serikalini kuna kina ‘Yuda’, imeiibua Jumuia ya Wazazi ya ya Chama cha Mapinduzi ambayo imejitenga na kauli hiyo.

Jumuiya hiyo  imeibuka ikiwa ni siku moja baada ya Simai kulieleza Bunge kuwa  kuna kiongozi ndani ya Serikali anafanya usaliti akimwita Yuda bila kumtaja jina, alipokuwa akichangia mjadala wa Wizara ya Fedha.

Katika hoja yake hiyo, alidai kiongozi huyo anazunguka makanisani na kutumia majina ya viongozi wastaafu kutafuta huruma ya wananchi na kufanya usaliti wake, kiasi cha kukwaza maendeleo.

Hoja hizo za Simai bungeni zimeibua mjadala hata nje ya muhimili huo. Wapo wanaohoji Yuda huyo ni nani? Wengine wanaonya hatari ya tuhuma, kadhalika wapo wanaosema kinachosemwa na mbunge huyo ni dalili ya upepo mchafu ndani ya CCM kuelekea urais wa 2030.

Leo Juni 4, 2026, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Fadhili Maganya amezungumzia kauli ya mbunge huyo wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya wiki ya wazazi itakayofanyika Julai 4, 2026 mkoani Mwanza.

Amesema CCM kitaendelea kuwa imara na salama wakati wote, na kuwa kauli zinazotolewa na mtu mmoja mmoja haziwezi kukiyumbisha wala kubadili mwelekeo wa chama hicho chenye wanachama zaidi ya milioni 13 nchini.

Maganya amesema mijadala inayoibuka kutokana na kauli za baadhi ya viongozi au wanachama haipaswi kutafsiriwa kama msimamo rasmi wa chama kwa kuwa CCM ina viongozi na wanachama wenye mitazamo tofauti, hivyo haiwezi kuyumbishwa kwa kauli ya mtu mmoja.

Amesema ukubwa wa CCM unaruhusu uwepo wa maoni mbalimbali, lakini msimamo wa chama hutolewa na viongozi wenye mamlaka ya kufanya hivyo na si kila mtu.

Mwenyekiti huyo amesema viongozi ambao wanaweza kutoa kauli ya chama ni Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu Wenyeviti wa chama wa Tanzania Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu pamoja na Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

“Chama cha Mapinduzi kina wanachama zaidi ya milioni 13. Miongoni mwao wapo makada, viongozi na wanachama wa kawaida wenye mitazamo tofauti. Mtu mmoja kutoa kauli yake haiwezi kufanya chama hiki kikose utulivu au kuonekana hakiko salama. CCM itabaki salama na imara siku zote,” amesema Maganya na kuongeza:

“Kauli hiyo haikutolewa na msemaji rasmi wa chama. Ilikuwa ni maoni ya mtu binafsi katika nafasi yake ya kisiasa, lakini siyo msimamo wa Chama cha Mapinduzi.”

Kwa mujibu wa Maganya, kauli iliyoibua mjadala inapaswa kutazamwa kama maoni binafsi ya mhusika na si msimamo wa CCM. Pamoja na kufuatilia kauli hizo zilizotolewa hadharani, amesema hali hiyo haiathiri uimara, mshikamano na umoja wa chama hicho.


Maadili kwa watoto

Katika hatua nyingine, Maganya amesema Jumuiya hiyo inaandaa mwongozo maalumu wa kuimarisha malezi na makuzi ya watoto kwa kuzingatia maadili, mila na desturi za Kitanzania.

Mganya amesema suala la malezi ni jukumu la jamii nzima na si la wazazi pekee, akieleza kuwa mila na desturi za Kitanzania na Kiafrika zimekuwa msingi muhimu wa kujenga maadili kwa watoto na vijana.

Amesema baadhi ya masuala yanayojadiliwa duniani kuhusu haki za binadamu yanapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia mazingira, tamaduni na maadili ya Tanzania.

Aidha, amebainisha kuwa katika kongamano lijalo la Jumuiya ya Wazazi kutakuwa na mjadala maalumu kuhusu changamoto za malezi na makuzi ya watoto, ambapo wadau watatoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha maadili katika jamii.

Amesema jumuiya hiyo tayari imeanza kuandaa waraka maalumu utakaotoa mwongozo wa kuboresha malezi na makuzi ya watoto kwa kuzingatia mazingira ya Kitanzania, kwa lengo la kujenga kizazi chenye maadili mema na uzalendo.

“Jukumu la malezi si la Jumuiya ya Wazazi pekee. Ni jukumu la jamii nzima. Tunazo mila na desturi zetu za Kitanzania na Kiafrika ambazo zimekuwa msingi wa malezi bora kwa vizazi vyetu.

“Sisi kama Jumuiya ya Wazazi yenye dhamana ya malezi tumeliona tatizo hili na sasa tunaandaa waraka utakaosaidia kuboresha makuzi na malezi ya Kitanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, mwenyekiti huyo amesema shughuli za wiki hiyo zitajikita katika maeneo matano muhimu ambayo ni elimu, malezi na maadili, mazingira, afya na utamaduni.

Amesema katika kipindi chote cha wiki hiyo kutakuwa na shughuli mbalimbali za kijamii na kielimu zitakazofanyika Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika kujenga kizazi chenye maadili na uzalendo.

“Kwanza ni elimu, pili malezi yanayobeba maadili, tatu mazingira, nne afya na tano utamaduni. Haya ndiyo maeneo makuu yatakayoongoza shughuli zote za wiki hii maalumu,” amesema.

Ameeleza kwamba kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho hayo, kutafanyika kongamano kubwa la kitaifa litakalowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya malezi, maadili na ustawi wa jamii nchini.

"Tutakuwa na kongamano kubwa la kitaifa linalohusu malezi, maadili na ustawi wa nchi yetu. Hili ni jukwaa muhimu la kujadili namna bora ya kuimarisha maadili na makuzi ya watoto na vijana wa Tanzania," amesema.