Prime
Ilikojificha siri ya mageuzi kisiasa

Dar es Salaam. Mageuzi ya mfumo wa kisiasa yatakayohusisha mabadiliko ya kisheria, sera na Katiba kwa ujumla wake, limekuwa hitaji la muda mrefu kwa baadhi ya wadau wa siasa na vyama vya upinzani.
Mitazamo ya vyama vya upinzani ni kuwa, mabadiliko hayo yatatoa uwanja sawa wa mapambano katika chaguzi na hivyo, kuwa turufu ya ushindi wa upinzani kwenye nafasi za juu, ikiwemo urais.
Lakini, baadhi ya wadau wa siasa, wanaona mabadiliko hayo, ndio utakaokuwa msingi wa kuimarika kwa demokrasia ya nchi na itazaa maendeleo, utulivu na mustakabali mwema wa taifa.
Kwa sababu ya mitazamo hiyo, kumekuwa na juhudi na harakati mbalimbali za kushinikiza mabadiliko, ndiko zilikozaliwa ajenda za kudai demokrasia na No Reforms No Election.
Haihitaji kurunzi kuona mkwamo wa mageuzi yote, licha ya harakati zilizowahi kufanywa. Yapo mageuzi yaliyoishia njiani na mengine kukaribia matumaini, lakini hatima ya kutimizwa kwake ilisubiri utashi wa ama Serikali, chama tawala au vyote kwa pamoja.
Lakini, wanazuoni waliobobea katika sayansi ya siasa, wanasema ipo siri ya mafanikio katika mageuzi ya kisasia nchini iliyojificha na haitatokana na harakati zinazoendelea.
Historia ya mikwamo ya mageuzi Tanzania
ageuzi katika mifumo na masuala ya kisiasa nchini, yana historia za mikwamo zaidi kuliko mafanikio.
Historia hiyo ya mageuzi inaanzia baada ya uhuru, mwaka 1961 hadi 1965, kipindi ilipoonekana haja ya kuondoa mfumo wa siasa za vyama vingi na kurudi chama kimoja.
Kufikia mwaka 1965, mfumo wa chama kimoja ulianzishwa rasmi kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii ilitokana na hoja kuwa vyama vingi vingeweza kusababisha mgawanyiko wa kitaifa.
Mkwamo wa vyama vingi, ulitokana na hofu ya kugawanyika kwa taifa jipya wakati huo, muelekeo wa kisiasa za ujamaa na kujitegemea uliohitaji mshikamano wa kitaifa, pia kukosekana kwa vyama vya upinzani vyenye nguvu.
Mwaka 1980 hadi 1992, kukaibuka shinikizo la mageuzi ya kisiasa, ukihitajika mfumo wa siasa za vyama vingi, hata hivyo hadi kufikia mwaka 1990, Serikali bado ilikuwa inashikilia mfumo wa chama kimoja.
Mwaka 1991, tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini iliweka bayana kuwa Watanzania wengi bado walikuwa na mashaka kuhusu mfumo huo.
Hatimaye, mwaka 1992, Katiba ilifanyiwa marekebisho kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
Ndiyo, yalifanyika mageuzi lakini hayakuwa kamili kwa sababu ya ukosefu wa taasisi imara za kidemokrasia, pia kulikuwa na hofu ya machafuko ya kisiasa.
Ulipofika mwaka 1995 hadi 2005, kukaibuka changamoto za uchaguzi huru na haki, pia vyama vya upinzani vilionekana dhaifu kutokana na ukosefu wa usawa wa vyama vya siasa katika kugawa rasilimali.
Pia, mfumo wa uchaguzi ulilalamikiwa kwa kutokuwa huru na wa haki na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kuibeba CCM.
Katika chaguzi zilizofuata, mabadiliko madogo yalifanyika, lakini bado vyama vya upinzani vilikosa nguvu ya kushinda.
Hii ni kwa sababu ya mfumo wa kisheria uliokuwa unatoa nafasi kubwa kwa chama tawala kudhibiti taasisi muhimu kama Tume ya Uchaguzi na vyombo vya usalama.
Mwaka 2010 hadi 2015, msukumo wa mageuzi uliongezeka na kulikuwa na harakati kubwa za kutaka Katiba mpya chini ya Rais Jakaya Kikwete. Mchakato wa Katiba ulianza na Tume ya Jaji Joseph Warioba mwaka 2011, ilipendekeza mabadiliko kadhaa.
Miongoni mwayo ni mfumo wa serikali tatu, yaani Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais na kuimarisha demokrasia na uwajibikaji wa Serikali.
Hata hivyo, mwaka 2014, mchakato huu ulikwama kutokana na upinzani mkali kutoka kwa CCM, iliyopinga mfumo wa serikali tatu, mivutano kati ya chama tawala na upinzani kuhusu maudhui ya Katiba mpya na kuahirishwa kwa kura ya maoni ya Katiba kutokana na ukosefu wa maridhiano.
Mwaka 2015 hadi 2021, mkwamo wa mageuzi ulishuhudiwa vilivyo, baada ya demokrasia kukandamizwa na kuzorota.
Chini ya utawala wa Rais John Magufuli wa wakati huo, hali ya kisiasa ilizidi kuwa ngumu kwa mageuzi ya kidemokrasia. Serikali yake ilijulikana kwa kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani.
Pia, ilitunga sheria kali kama Sheria ya Vyombo vya Habari na Sheria ya Makosa ya Mtandao na kubana uhuru wa kujieleza na kuendesha siasa.
Katika kipindi hiki, juhudi za mageuzi ya kisiasa zilikwama kutokana na udhibiti mkali wa Serikali dhidi ya taasisi za kiraia na vyombo vya habari.
Pia, udhaifu wa vyama vya upinzani kushikamana katika kupigania mabadiliko na hofu ya wananchi kujihusisha na siasa kutokana na mazingira ya ukandamizaji.
Siri ya mageuzi
wa mtazamo wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, mbinu yoyote inayolenga kuleta mageuzi hutegemea wakati na mazingira halisi.
Anaeleza mbinu zinazotumika sasa na wadau wa siasa na baadhi ya vyama kushinikiza mageuzi, ingekuwa katika mataifa mengine zingezaa matunda.
Lakini kwa Tanzania ni vigumu kwa wakati huu, akitaja sababu bado wananchi wameridhika na maisha wanayoishi na wanaamini mambo yao yanaweza kwenda bila siasa.
"Kuna vitu viwili, maisha yetu bado yanahimilika, kwa hiyo, hatuoni kama siasa inaweza kuamua hatima yetu. Katika mazingira haya vuguvugu la mageuzi ya Katiba linakosa nguvu ya wananchi kwa sababu hawaoni umuhimu wake," anafafanua.
Anasema ukifika wakati siasa zikachafuka na watu wakashindwa kuendelea na shughuli zao, ndipo utakapoiona hata nguvu ya umma ikidai mageuzi na hapo ndipo yatakapopatikana.
Mwanazuoni huyo anasema jambo kama hilo, lilishuhudiwa nchini Algeria na hata Singapore.
Anasema wananchi hawahamasiki kwa sababu bado hali yao ni nzuri, hawajui hata hayo mageuzi yatawasaidiaje.
"Lakini ukifika wakati wa tabu, mageuzi yenyewe yatakuja, kwa sababu kile ambacho wananchi walikuwa wanaogopa hakitakuwepo tena, woga utaisha," anasisitiza.
Kwa mtazamo wake, hakuna mbinu inayoweza kutumika sasa ikafanikisha mageuzi kutokana na uhalisia huo, zaidi ya kusubiri nyakati ambazo wananchi wamekerwa.
"Kwa kawaida mageuzi na hata historia inaonyesha hivyo, kwamba huwa yanakuja ghafla. Linatokea jambo linaamsha hasira za wengi, katikati ya hali hiyo, ndipo mageuzi pia yanafanywa," anasema.
Hata hivyo, Dk Masabo anasema hajajua ni lini hali hiyo inaweza kutokea kwa sababu si kitu kinachotabirika.
"Nakupa mfano wa vita ya ubaguzi wa rangi Marekani, baada ya kuuawa kwa yule George Floyd Mmarekani mweusi, ilimsha hisia za wananchi wengi na mageuzi mengi yakapitia njia hiyo," anasema.
Kwa kawaida, anasema sababu haitengenezwi, badala yake ni kitu kinachotokea kutoka kusikojulikana na hatimaye kinaamsha hisia za watu na ndipo mageuzi yanakopenya.
Mageuzi ni 'automatic'
chambuzi wa Masuala ya Siasa, Prince Mwambipile anasema kihistoria mageuzi ya kisiasa katika mataifa mengi, yametokea baada ya juhudi za muda mrefu za wadau bila mafanikio.
Anaeleza kwa sehemu kubwa kulitokea machafuko ndio baadaye yakafuata mageuzi hasa yale yanayogusa Katiba kwa ujumla wake.
Anasisitiza mbinu zinazotumika kudai mageuzi bado zitakwama kwa sababu hatima ya kufanyika kwake inabaki mikononi mwa mamlaka.
"Wananchi kwa ujumla wao ndio mara zote wanaokuwa sababu ya mageuzi, haikuwahi kutokea mwanasiasa akasababisha mageuzi jukwaani. Wananchi wanaposema wanataka ndio inatokea," anasema.
Hata hivyo, anasema hakuna wa kuwashawishi wananchi waamue, zaidi ya shida zao na changamoto zinazowakabili.
"Ukiona unashinikiza mageuzi na huungwi mkono na wananchi, ujue bado hawana tatizo na hali iliyopo. Siku wakitatizika wenyewe bila kuambiwa itawaona wanadai," anaeleza.
Anasisitiza siri ya mageuzi ipo ndani ya changamoto za wananchi, watakapoona wanapata shida watadai.
"Kwa kukaa jukwaani ukasema wananchi hakikisheni mnafanya mageuzi, huwezi kufanikiwa. Mwananchi hasikilizi, mara nyingi anajiangalia yeye binafsi na maisha yake, alikutana na vikwazo kwenye eneo hilo, utamuona anadai mageuzi," anasema.
Anasisitiza pengine hata juhudi zinazoendelea na kudai Katiba Mpya na Sheria nyingine, hazitafanikiwa kwa majukwaa ya kisiasa, usipokuwa itakapofika siku wananchi wanaumizwa ndipo vuguvugu litaonekana.
Tafasiri ya mageuzi
Mageuzi ya kisiasa yanahusisha marekebisho ya vipengele vya katiba vinavyoonekana kuwa kikwazo kwa demokrasia, kama vile muda wa uongozi wa viongozi wa kisiasa au mamlaka ya vyombo vya uchaguzi.
Mabadiliko ya sheria za uchaguzi ni maana nyingine ya mageuzi ya kisiasa, ikilenga kuhakikisha kuwa uchaguzi ni huru na wa haki kwa kuweka taratibu zinazozuia upendeleo na udhibiti wa vyombo vya dola katika siasa.
Kuboresha uhuru wa taasisi za kisiasa ni maana nyingine ya mageuzi ya kisiasa kama vile Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyombo vya usimamizi wa haki, na vyombo vya habari ili viwe huru na visifanye kazi kwa shinikizo la serikali au chama tawala.
Ugatuzi wa madaraka, kugawa mamlaka kutoka serikali kuu kwenda kwa serikali za mitaa ili wananchi washiriki zaidi katika maamuzi yanayowahusu.
Uimarishaji wa Haki za Kidemokrasia, kama uhuru wa vyama vya siasa, haki ya kujieleza na uhuru wa maandamano ya amani.
Lengo kuu la mageuzi ya kisiasa ni kuimarisha utawala wa sheria, kujenga uwanja wa kisiasa ulio sawa kwa wote na kuhakikisha kuwa sauti za wananchi zinasikika katika kuendesha nchi.