Hivi ndivyo Ruto anavyopachikwa majina na Gen-Z

Rais wa Kenya, William Ruto.
Muktasari:
- Tangu ameingia madarakani, Rais Ruto amepewa majina mbalimbali ya utani kiasi ambacho hata yeye anashangaa ni kwa nini Wakenya wamekuwa wakimpa majina hayo.
Dar es Salaam. Tangu ameingia madarakani, Rais wa Kenya, William Ruto amepewa majina mbalimbali ya utani kiasi ambacho hata yeye anashangaa ni kwa nini Wakenya wamekuwa wakimpa majina hayo.
Ruto aliingia madarakani mwaka 2022, akapata misukosuko ya maandamano ya vijana maarufu Gen-Z, akaonyesha ustahimilivu akaishi nao.
Maandamano hayakutosha akaanza kupachikwa majina ya utani ikiwemo Kasongo, El Chapo pamoja na vibonzo na michoro mitandaoni, hivi hivyo unaweza kusema ukitazama maisha ya Rais wa Kenya William Ruto kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Gen-Z wanampachika majina
Awali, Wakenya walimuita Zakayo, wakiwa na maana ya mtoza ushuru na hatimaye Kasongo jina lililojipatia umaarufu si Kenya tu bali Afrika Mashariki.
Ruto aliwahi kusema: “Nataka niwaulize nyie watu wa Nairobi si mtaniua kwa majina mapya, mlianza kwa kunipa jina la Hustler, halafu mkaniita Survivor. Halafu nyie mkanipa jina la Zakayo sasa nasikia mnaniita Kasongo. Hivi nyie mtaniongeza majina au mmemaliza? Mko na maneno. Sasa mnataka niwe na majina 10?”
Mfano, jina kama El-Chapo lilianza baada ya Rais Ruto kuahidi Serikali ya Kaunti ya Nairobi mashine ya kutengeneza chapati. Jumanne, Machi 11, 2025, Gavana Johnson Sakaja alimwomba Ruto kuunga mkono mpango wake wa kuilisha Kaunti.
Akijibu ombi la Sakaja, Rais aliahidi kupata mashine yenye uwezo wa kutengeneza chapati milioni moja kwa siku.
Babu Owino alimkosoa Sakaja kwa kuomba mashine ya kutengeneza chapati kutoka kwa Rais. Owino alilitazama ombi hilo, lililotolewa baada ya Ruto kuahidi kununua mashine kama hiyo, kama kikwazo cha masuala muhimu zaidi jijini Nairobi.
Aina ya uongozi ya Ruto
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 5, 2025, Mchambuzi wa Siasa za Kimataifa, Abdallah Kanju amesema Rais Ruto amekuwa na mtindo wa kipekee wa kujibadilika kulingana na hali ya kisiasa na kijamii nchini Kenya.
Anasema kukubali kwake utani na majina ya kejeli kama vile Zakayo, Kasongo, Yesu wa Sugoi, au Hustler, bila hasira ni sehemu ya mkakati mpana wa kisiasa.
Akitaja baadhi ya mbinu anazotumia kuishi na wananchi wake, Kanju amesema miongoni mwazo ni unyumbulifu wa kisiasa.
“Rais Ruto ni mwanasiasa anayeelewa nguvu ya kutobeba mambo binafsi. Kukubali utani au kejeli kunamwonyesha kuwa ni mtu wa watu (mwananchi wa kawaida), asiye na kinyongo. Hii inamsaidia kuepuka migogoro isiyo ya lazima na kudhibiti maoni ya umma kwa njia ya ucheshi.
“Kujenga taswira ya mtu wa kawaida, kwa kukubali kuitwa majina ya mtaani, Ruto anajenga picha ya kuwa si mtu wa tabaka la juu au wa mfumo bali ni mpambanaji aliyejitokeza kutoka kwa hali ya chini. Hii inamfanya aonekane kama kielelezo cha matumaini kwa wananchi wa kawaida,” amesema.
Kanju amesema Ruto anatumia kejeli kama zana ya mawasiliano badala ya kupuuza au kulalamikia kejeli, Ruto huzigeuza kuwa sehemu ya hotuba au mazungumzo yake ya kisiasa.
“Kwa mfano, alikubali jina Zakayo na kulitumia kueleza mpango wake wa ushuru. Hii ni mbinu ya “kuzigeuza risasi kuwa maua’ yaani kutumia maneno ya upinzani kama nyenzo ya kuimarisha ujumbe wake,” amesema.
Aidha, amesema ni hodari wa mawasiliano ya kisiasa kwa kuwa ni mzungumzaji mzuri ambaye hutumia lugha rahisi, mifano ya wazi na mbinu za kushawishi hadhira.
Amesema ana uwezo wa kuwasiliana moja kwa moja na wananchi kwa lugha wanayoelewa, iwe ni Kiswahili, Kiingereza au Sheng. Hii huongeza ukaribu na wananchi.
Mwisho, mchambuzi huyo amesema ni ujanja wa kuongoza uhusiano wake na umma kupitia timu yake ya mawasiliano, mitandao ya kijamii, na hotuba za hadhara, Ruto huzijibu kejeli kwa njia inayobadilisha maoni hasi kuwa chanya. Mbinu hii huimarisha ushawishi wake na kuleta umakini zaidi katika ajenda zake.