Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche ataka Watanzania waunganishe nguvu kupigania nchi

Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa (mwenye kofia nyeusi) John Heche akisalimiana na baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoani Mara baada ya kufika wilayani Bunda kwaajili ya harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya Chadema Wilaya ya Bunda. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Heche amesema kila Mtanzania anatakiwa kutambua kuwa ana wajibu wa kubadilisha nchi ili iwe sehemu salama kwao na kizazi kijacho kwa maelezo kuwa jukumu hilo ni la kikatiba na sio kosa kisheria.

Bunda. Watanzania wametakiwa kuunganisha nguvu zao pamoja ili kupigania nchi yao na hatimaye kunufaika kwa usawa na rasilimali zilizopo nchini, badala ya kuacha jukumu hilo kwa baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa wachache.

Wito huo umetolewa Mjini Bunda leo Jumapili Mei 10, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, John Heche kwenye harambee ya kuchangia ujezi wa ofisi ya Chadema Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Heche amesema kila Mtanzania anatakiwa kutambua kuwa ana wajibu wa kubadilisha nchi ili iwe sehemu salama kwao na kizazi kijacho kwa maelezo kuwa jukumu hilo ni la kikatiba na sio kosa kisheria.

Amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua mamlaka ya wananchi kwa viongozi na nchi yao kwa maelezo kuwa wananchi ndio wenye wajibu na jukumu la kuamua nani awe kiongozi kwa nafasi gani na kwa sifa zipi.

"Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mapungufu yake katika ibara ya nane inaeleza kuwa nchi yetu ni ya kijamhuri ambayo inafuata misingi ya kidemokarisia, kwa hiyo wananchi ndio msingi wa madaraka wa mamlaka yote kwa lugha nyingine hao viongozi wanaajiriwa na wananchi," amesema.

Amesema viongozi waliopo madarakani wamejisahau kuwa wao ni waajiriwa wa wananchi na ndio maana hawataki kukosolewa jambo ambalo ni kinyume cha Katiba, hivyo hali hiyo itakomeshwa endapo wananchi wataunga nguvu pamoja kwa kushirikiana na wale waliojitokeza kupambana kwa ajili ya haki za wananchi kikiwepo Chadema.

Heche amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kutokana na yale ambayo yamekuwa yakiwapata hasa wale walio mstari wa mbele katika mapambano hayo kwa maelezo kwamba, ni dhahiri kuwa kabla ya kufika katika mema yanayotarajiwa ni lazima wapite kwenye misukosuko.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa, John Heche akiangalia ramani ya ofisi ya chama hicho wilayani Bunda kabla ya kuanza kwa harambee kwaajili ya kufanikisha ujenzi huo. Picha na Beldina Nyakeke

"Tusiogope kupitishwa kwenye bonde la uvuli wa mauti,tujiandae kupita humo kabla ya kufika kwenye nchi ya ahadi, mimi binafsi nimeshasema na ninarudia kusema, sitakimbia nchi nitaendeleza mapambano na kama ni kufa waniue nikiwa hapa hapa nchini kwetu kwa sababu hii nchi ni ya kwetu sote na wao sio Mungu," amesema.

Amesema mashambulizi dhidi ya Chadema yanayoendelea yanadhihirsha kuwa chama hicho ndicho chama sahihi kwa ajili ya ukombozi wa Watanzania.

Katika harambee hiyo, Heche na marafiki zake wamechangia Sh11.5 milioni ili kukamilisha ujenzi huo.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa ofisi ya Wilaya ya Bunda, Kaimu Katibu wa Chadema Jimbo la Bunda Mjini, Zakayo Bwire amesema chama hicho kinahitaji zaidi ya Sh30 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

Ameeleza kuwa ujenzi wa ofisi hiyo ulianza Desemba 2021 walitumia  Sh16 milioni, ujenzi ambao hata hivyo ulishindwa kuendelea baada ya watu wasiojulikana kubomoa jengo hilo.

"Mwaka 2021 tulijenga hadi kufika hatua ya lenta lakini watu wasiojulikana walikuja wakabomoa jengo, kisha mwaka 2023 tukaendelea tena na ujenzi hadi kufikia hatua ya kupaua sasa tukiwa bado tunajikusanya kupata pesa kwaajili ya vifaa ya upauaji tena watu wasiojulikana walikuja wakaliangusha jengo hadi kuwa katika hali hii inayoonekana sasa," amesema.

Amesema ujenzi huo uliwekewe jiwe la msingi na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kiasi chote cha fedha kilichotumika kwa ajili ya ujenzi huo, kilitokana na michango ya wanachama ndani ya wilaya hiyo.

Bwire ameeleza kuwa baada ya kukamilika, jengo hilo litakuwa na ofisi mbalimbali zikiwamo za mwenyekiti na katibu pamoja na ukumbi wa mikutano utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 400.

Akitoa taarifa ya mkoa katika mkutano huo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Donald Mwembe amesema baraza la uongozi wa chama hicho mkoani humo limedhamiria kuhakikisha chama hicho kinapata ofisi katika majimbo yote yaliyopo ndani ya mkoa huo.

"Tumedhamiria kuwafanya viongozi wetu kutokuwa viongozi wa mitandaoni bali wawe na ofisi rasmi na tayari tumefanya harambee kwa ajili ya ujenzi kule Serengeti na leo tuko hapa Bunda, tuna ratiba kwa ajili ya wilaya zote ili kuhakikisha viongozi wanakuwa na sehemu sahihi na rasmi kwaajili ya kutekeleza wajibu na majukumu yao," amesema.

Mwembe pia amekiomba chama hicho makao makuu kutoa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa ngazi ya majimbo na mkoa ili waweze kufanya shughuli zao kwa weledi na tija zaidi.

Mwenyewekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche amesema baraza la uongozi mkoani humo limejiwekea malengo ya kuwa na ofisi za chama katika majimbo 10 ya mkoa wa Mara na wilaya sita za mkoa huo ifikapo mwaka 2029.

Amesema wameamua kufanya hivyo ili kuonesha kwa vitendo kuwa wana uwezo wa kuongoza nchi pale watakapopata ridhaa ya kuongoza kama ambavyo imekuwa dhamira yao tangu chama hicho kianzishwe.

"Kuna watu wamekuwa na tabia ya kututukana kuwa hatuna ofisi kana kwamba ofisi ndio akili, sasa tumeamua kwa kutumia nguvu za wananchi na wanachama wetu, kufika 2029 tutakuwa na ofisi zetu kwenye majengo yetu na sio majengo ya kukodi," amesema Heche.