Dk Nchimbi atoa maagizo kwa Serikali, amwita naibu waziri

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi
Muktasari:
- Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ametoa maagizo kwa Serikali kusimamia ipasavyo bei ya zao la Kahawa pamoja na kumtaka Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kwenda kuungana naye kwenye ziara yake inayoendelea.
Kyerwa. Kufuatia kupaa kwa bei ya Kahawa mkoani Kagera, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameipongeza Serikali kwa kusimamia jambo hilo kwa maslahi ya wakulima mkoani humo huku akiitaka iendelee kusimamia ili isishuke.
Dk Nchimbi ametoa pongezi hizo wakati wa mkutano wake uliofanyika leo Alhamisi Agosti 8, 2024 katika Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika mkoa huo.
Pongezi hizo zilifuata baada ya Mbunge wa Kyerwa (CCM), Innocent Bilakwate kueleza namna wakulima wanavyonufaika na zao la kahawa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza kahawa kuuzwa kwenye minada.
Amesema zao la kahawa lilikuwa linaporomoka lakini wakulima walipoanza kuuza kwenye minada, bei ya zao hilo imepanda kutoka Sh1,300 kwa kilo mwaka 2022, Sh2,300 mwaka 2023, hadi kufikia Sh5,000 mwaka huu.
"Wananchi wangu wa Kyerwa wanaishukuru Serikali kwa kuwasaidia kupandisha bei ya kahawa na sasa wakulima wanauza kahawa zao kwenye mnada kwa bei ya Sh5,000 kwa kilo, hii ni hatua kubwa," amesema Bilakwate.
Akizungumzia suala la kahawa, Dk Nchimbi ameeleza kuongezeka kwa bei ya kahawa ni matokeo mazuri ya usimamizi wa Serikali katika zao hilo ili iwanufaishe wakulima.
"Serikali iendelee kusimamia biashara ya kahawa ili bei iendelee kuwa nzuri," amesema Dk Nchimbi wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi.
Kuhusu kero za wananchi, Bilakwate amemweleza Dk Nchimbi kuhusu kero ya kutopatikana kwa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi katika jimbo lake, hivyo amemuomba wananchi hao wapatiwe vitambulisho ili wapate huduma.
Kero hiyo, pia imetolewa maeneo mengine yaliyotembelewa na Dk Nchimbi ikiwemo Kasulu, Kibondo na Ngara. Kufuatia malalamiko hayo, Katibu Mkuu amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo kuungana naye kwenye ziara yake ili aweze kutoa majibu mazuri kwa wananchi kuhusu mambo yanayohusu wizara yake.
"Natambua Waziri wa Mambo ya Ndani amesafiri. Naelekeza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani aje aungane nasi kwenye ziara hii ili aweze kusikia na kujibu kero za wananchi," amesema Dk Nchimbi.
Mkazi wa Kata ya Nkenda, Amon Kamala amesema changamoto yao kubwa ni ubovu wa barabara unaowakwamisha kufanya biashara kwa haraka na kuifungua wilaya hiyo kwa kuruhusu watu wengi kwenda kufanya biashara.
"Barabara yetu inayounganisha Wilaya za Kyerwa na Karagwe ni mbovu sana, tunaomba serikali itujengee barabara hii kwa kiwango cha lami ili maisha yetu yawe rahisi," amesema mwananchi huyo.
Akizungumzia barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa amesema mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika na mkandarasi amepatikana, kilichobaki ni kumkabidhi eneo ambalo ataweka makazi yake ya kuhifadhia vifaa.
"Ndugu Katibu Mkuu, nikuahidi kuwa baada ya ziara yako, nitarejea hapa Nkenda kwa ajili ya kumkabidhi mkandarasi eneo atakalojenga kambi yake ili aanze kazi," amesema Bashungwa.