Dk Nchimbi ‘amkaba koo’ Waziri wa Fedha kisa changamoto mbili Musoma

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza baada ya kukagua ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Musoma mkoani Mara, katika mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.
Muktasari:
- Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ametaka mambo mawili yafanyike kutatua mkwamo wa kukamilika kwa miradi miwili wilayani Musoma.
Mara. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, ameagiza hatua muhimu zichukuliwe kutatua changamoto ya umeme katika Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere na kukamilishwa kwa Uwanja wa ndege Musoma.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere, inayoandaliwa kutoa huduma na mafunzo ya matibabu, ametaka kabla ya Bunge kuvunjwa, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, awe ameshazitoa fedha za kumlipa mkandarasi.
Kwa upande wa Uwanja wa ndege Musoma, unaotarajiwa kufungua soko la utalii katika Hifadhi ya Serengeti na maeneo ya jirani, Dk Nchimbi amemtaka waziri huyo afanikishe upatikanaji wa fedha kuhakikisha mradi huo unakamilika Septemba kama ilivyopangwa.
Kiasi cha fedha alichoagiza Dk Nchimbi kitolewe kufanikisha miradi yote miwili ni Sh4 bilioni, kati ya hizo, Sh2.5 bilioni ni kwa ajili ya uwanja wa ndege na Sh1.5 bilioni kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere.

Hatua ya Dk Nchimbi kutoa maelekezo kuhusu changamoto ya umeme hafifu katika hospitali hiyo imetokana na kilichoelezwa na Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, aliyesema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya umeme na hivyo kukwaza huduma za X-Ray.
Changamoto hiyo, amesema, inatokana na kuchelewa kwa ukamilishaji wa ujenzi wa mradi wa jenereta litakaloongeza kiwango cha umeme, kwa kuwa umeme uliopo haukidhi mahitaji ya huduma hospitalini hapo.
"Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), amepeleka madai ya Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo tangu mwaka jana, lakini hajalipwa," amesema Mathayo.
Dk Nchimbi ametoa maelekezo hayo leo, Jumatano, Aprili 23, 2025, kwa nyakati tofauti alipotembelea miradi hiyo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Mara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amesema kwa ukubwa wa hospitali hiyo na idadi ya watu wanaotibiwa kutoka ndani na nje ya nchi, changamoto ya umeme haipaswi kuendelea.

"Kwa kuwa mbunge amesema ahadi hiyo ilitolewa tangu mwaka jana mwishoni na sasa ni Aprili, kwa hiyo nitoe wito kwa Waziri wa Fedha (Dk Mwigulu Nchemba) kulipa kipaumbele cha pekee suala la jenereta katika hospitali hii," amesema.
Amemtaka waziri huyo kuhakikisha anatumia muda huu kabla ya Bunge halijaisha kukamilisha upatikanaji wa fedha hizo ili ujenzi ukamilike.
"Ajue (Dk Nchemba) kuwa wakati Bunge linaendelea katika wiki hizi mbili tatu, ahakikishe fedha zinafika na nitakupigia simu mkuu wa mkoa kukuuliza kama fedha zimefika. Kama hazijafika, nitamuita waziri ofisini kwangu kumhoji kwa nini fedha hazijafika," amesema.
Awali, akizungumzia hospitali hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, amesema mbali na wagonjwa kutoka ndani, hata wa nje ya nchi wanatibiwa hapo.
Kwa mujibu wa Dk Mollel, wagonjwa 161 wamevuka mpaka kutoka Kenya kwenda katika hospitali hiyo kupatiwa huduma.
Uwanja wa ndege Musoma
Akiwa katika uwanja wa ndege Musoma, Dk Nchimbi ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ishirikiane na Wizara ya Fedha kuratibu haraka ukamilishaji wa malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha eneo litakapojengwa jengo la abiria la uwanja huo.
Katika maelekezo yake hayo, amesema ni muhimu ifanyike hivyo ili kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kuende sambamba na jengo la abiria.
"TAA mshirikiane na Hazina kuona namna ya kufanyia kazi tathmini zilizokamilika, ili wananchi walipwe na ujenzi wa uwanja wa ndege uende sambamba na jengo la abiria."
Maelekezo ya Dk Nchimbi kuhusu fidia hizo ni taarifa ya hoja iliyotolewa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Vedastus Maribe, aliyeomba kuharakishwa kwa malipo ya fidia hizo.
Maribe amesema malipo hayo ni Sh5.2 bilioni kwa wananchi 58 ili kuhakikisha jengo hilo linajengwa haraka na huduma zinatolewa sambamba na eneo la abiria kukaa.
Amesema uwanja huo utahudumia mikoa ya Mara na Simiyu, pamoja nan chi jirani za Rwanda na Uganda.

Hata hivyo, amesema, pamoja na maboresho yanayofanywa, uwanja huo wa ndege haukuwahi kufungwa.
Ameeleza wanachokifanya ni kukarabati njia ya kuruka na kutua ndege, njia ya maungio, maegesho ya ndege, mifereji, ununuzi na usimikaji wa vifaa vya kuongozea ndege.
Utekelezaji wa mradi huo, amesema, umefikia asilimia 58 na Septemba mwaka huu wanatarajia ukamilike, huku Sh8.2 bilioni zimeshalipwa na Sh2.5 bilioni bado mkandarasi hajalipwa.
Katika msisitizo wake, Dk Nchimbi amemtaka Dk Nchemba kuhakikisha anaharakisha upatikanaji wa fedha za kukamilisha ujenzi wa uwanja huo kama ilivyopangwa.
Ameitaka TAA, kwa kushirikiana na Hazina, waone namna ya kufanyia kazi tathmini zilizokamilika.

"Uwanja wa ndege hautakuwa na maana iwapo utakamilika na jengo la abiria hakuna," amesema.