Dk Mwinyi aonya mgawanyiko ndani ya CCM

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwa anazungumza katika moja ya tukio la chama hicho.

Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameonya mfarakano na mgawanyiko ndani ya chama na kuwataka wanachama wawe kitu kimoja ili kuongeza nguvu ya chama chao.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 6, 2023 katikia ziara yake wakati akizungumza na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mashina, majimbo, wilaya, hadi mkoa kwenye Ukumbi wa Piccadilly Kombeni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Amesema wakati wa chaguzi zote huibuka makundi mbalimbali yenye dhamira na maslahi tofauti hivyo, amewataka wana CCM kurejesha umoja na mshikamano baada ya uchaguzi kukamilika.

“Kamati za maadili chukueni hatua kali za kinidhamu kuhakikisha nidhamu na mshikamano ndani ya chama unarejea pindi inapotokea mgawanyiko na makundi,” amesema.

Akizungumzia suala la uhai wa chama, Dk Mwinyi amewataka viongozi wenye dhamana kwa mujibu wa nafasi zao ndani ya chama hicho, kutekeleza jukumu na kuongeza wanachama wapya ili kuendelea kukipa uhai chama hicho kiendelee kushika dola.

“Mtaji wa chama chetu ni kuongezeka wanachama wepya, kadi ziwepo za kutosha,” amesisitiza Makamu Mwenyekiti huyo.

Vilevile, amewahimiza wana CCM kulipa michango kwa wakati badala ya kusubiri hadi vipindi vya uchaguzi vikaribie.

Katika hatua nyingine, Rais Dk, Mwinyi, ameagiza chama kuwapa mafunzo ya uongozi watendaji wa ngazi zote walioshinda kwenye uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana pamoja na kujipanga tena kwaajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Naibu Katibu mkuu CCM, Zanzibar Dk Muhamed Said Dimwa aMEsema CCM haitajibu maneno wanayorushiwa na wapinzani badala yake wataendelea kuitekeleza Ilani ya chama na kuahidi kutowafumbia macho wenye dhamira ya kuwakwamisha.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Tanzania Zainab Khamis Shomari, alieleza ahadi ya wanawake na kinamama Tanzania bado ipo palepale ya kurejesha ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Pia aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwajengea heshima wanawake kwa kuwapa fursa ya uongozi kwenye sekta mbalimbali.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi, Muhamed Rajab Soud, alishukuru Serikali kuendelea kuufungua kimaendeleo mkoa huo kwa kuwepo na wawekezaji mbalimbali hivyo kujenga heshima ya mkoa.

Huo, ulikua mkutano wa kwanza wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk Mwinyi na viongozi wa chama hicho kwa ngazi za mashina, majimbo, wilaya, hadi Mkoa, tangu kumalizika wa chaguzi za chama hicho, mwishoni mwa mwaka jana.