Chaumma kuwapata waombea urais, Mzee wa Ubwabwa asema…

Muktasari:
- Juni 27-28, 2025 Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kitafanya mkutano mkuu wa kuwapata wagombea urais wa Tanzania na Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.
Dar es Salaam. Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kinatarajiwa kuingia kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mkutano wa kuwapata wapeperusha bendera hao wa urais wa Tanzania na Zanzibar utafanyika Juni 27 hadi 28, 2025 kwa wajumbe 400 wa mkutano mkuu kuketi na kupiga kura, huku mwenyekiti wa chama hicho, Hashima Rungwe, maarufu ‘Mzee wa Ubwabwa’ akiwaambia wanaomuuliza kama atawania wawe na subira.
Kabla ya mkutano huo, utatanguliwa na mkutano wa kufanya maandalizi wa wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho utakaofanyika siku mbili kuanzia Mei 10 hadi 11, 2025 jijini Dar es Salaam.

Chaumma pamoja na vyama vya ACT – Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), bado vipo kwenye hatua za mwisho kuwapata wagombea wao.
Huku vyama vya CCM, SAU, AAFP, UPDP, NLD na NCCR- Mageuzi tayari vilishakamilisha hatua ya kuwajua wagombea wao.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Machi 6, 2025, Katibu Mkuu wa Chaumma, Mohamed Masoud amesema maandalizi ya kuelekea kuwapata wagombea wao yanaenda vizuri.
"Tunafanya maandalizi na Mei 10 na 11 tutakuwa na vikao vya wajumbe wa kamati kuu pamoja na kujadili maendeleo ya chama, lakini tunategemea tutafanya maandalizi ya kupata wagombea kwenye mkutano mkuu wa wajumbe utakaofanyika Juni 27 na 28 mwaka huu," amesema Masoud.

Masoud amesema ni lazima mkutano wa kuwapata wagombea wao katika uchaguzi mkuu maandalizi yake yafanyike mapema na kikamilifu kwani utakusanya wajumbe 400 kutoka nchi nzima.
"Wajumbe wote ni muhimu katika kupiga kura lakini katiba yetu inasema wakifikia walau thelusi moja ili akidi akidi ya wajumbe wanaoweza kupiga kura itimie," amesema Masoud
Masoud ametoa rai kwa wajumbe wa kamati kuu kujitokeza kwa wingi ili kufanya maandalizi mazuri ya kupata wagombea wenye sifa na watakaokuwa na uwezo wa kukubalika kwa Watanzania muda ukiwadia.
Mwenyekiti wa chama hicho, Hashimu Rungwe amesema kuwapata wagombea wao Juni 2025 wanakuwa ndani ya muda na wala hawajachelewa.
"Kikubwa nawasihi wanachama wetu na Watanzania wenye kiu na Mzee wa Ubwabwa wawe watulivu tunapika mambo wakati ukifika tutawasogezea wagombea," amesema.
Alipoulizwa iwapo atajitosa kuomba ridhaa hiyo ameanza kwa kucheka huku akibainisha: "Si wakati wakusema ila itajulikana kwenye mkutano baada ya wajumbe kufanya uamuzi wenye masilahi mapana kwa chama."
Kulingana na Rungwe amesema wamejipanga kusimamisha wabunge na madiwani nchi nzima.

Katika uchaguzi mkuu wa 2020, Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa aliwania nafasi ya urais na alipata kura 32,878 kati ya kura 15,091,950 zilizopigwa ambapo mgombea urais wa CCM aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, hayati John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4.