Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema Serengeti yaibua madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu Shinyanga

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto amedai zipo taarifa za wananchi kunyang'anywa pikipiki na vyombo vingine vya usafiri, huku zaidi ya watu 200 wakidaiwa kushikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi, wakati huo Jeshi la Polisi limethibitisha kushikiria watuhumiwa 75.

Dar/Shinyanga. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti kimeeleza wasiwasi wake kuhusu kile ilichodai kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Maeneo yaliyotajwa ni Kijiji cha Idukilo kilichopo Kata ya Idukilo, Kijiji cha Kabila kilichopo Kata ya Mondo, Kijiji cha Magazo katika Kata ya Magazo pamoja na Kijiji cha Mabambasi kilichopo Kata ya Mwadui Ruhumbo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 5, 2026 na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto, chama hicho kinafuatilia kwa karibu taarifa za wananchi katika maeneo hayo kuhusu matukio yanayodaiwa kuhusisha operesheni za Polisi.

“Kwa mujibu wa taarifa tunazozipokea kutoka kwa wananchi, kuna madai ya polisi kuzuia shughuli za kijamii, kufunga kwa nguvu maduka, kuvamia nyumba za wananchi na kusababisha uharibifu wa mali mbalimbali ikiwemo fedha na bidhaa,” amedai Ngoto kupitia taarifa yake.

Ngoto amedai zipo taarifa za wananchi kunyang'anywa pikipiki na vyombo vingine vya usafiri, huku zaidi ya watu 200 wakidaiwa kushikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

“Vilevile, tumepokea madai ya wananchi kupigwa na kuteswa, pamoja na matumizi ya Shule ya Msingi Idukilo kama kituo cha polisi, jambo ambalo linaongeza taharuki katika jamii,” amedai.

Kutokana na hali hiyo, Chadema imetoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kishapu kuchukua hatua za haraka kusitisha operesheni hiyo inayolalamikiwa na wananchi.

Aidha, chama hicho imezitaka taasisi huru za kutetea haki za binadamu kufuatilia kwa karibu kinachoendelea katika maeneo hayo ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

Ngoto amesema chama hicho kitaweka hadharani msimamo wake rasmi kuhusu matukio hayo kesho huku kikitoa rai kwa wananchi kuendelea kukusanya na kuhifadhi ushahidi wa matukio yote wanayodai yametokea.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa na Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kuwashikilia watu 75 waliohusika katika matukio mawili ya kusababisha vurugu katika Kijiji cha Sanjo, kata ya Idukilo wilayani Kishapu,

Amesema Jeshi la Polisi limekamata watuhumiwa 75 waliohusika katika matukio mawili tofauti, tukio la kwanza lilitokea Mei 28, 2026 katika kijiji cha Sanjo kata ya Idukilo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Amesema mtendaji wa Kata ya Idukilo, Masembe Msele (50) akiwa na Ofisa Maendeleo wa Kata ya Mwadui Luhumbo aitwaye Rose Shayo (38), mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo pamoja na wajumbe watatu wa serikali ya kijiji, wakiwa katika shughuli ya kuingiza kaya masikini katika mfumo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), walivamiwa na watu waliokuwa kwenye pikipiki mbili,” amesema Magomi.

“Watu hao walianza kuwapiga na kuwanyang’anya nyaraka hizo zilizokuwa na baadhi ya majina na kuondoka wakidai hawataki kuona kiongozi yeyote wa Serikali akifanya kazi ndani ya kata ya Idukilo. Vurugu hizo zilisababishwa na wananchi kumkataa diwani wa kata hiyo, ambaye alikimbia eneo hilo.

“Tukio la pili lilitokea Juni Mosi, 2026 saa 6:30 usiku katika kata hiyo ambapo, kuna baadhi ya wanakijiji walipigwa kwa madai kuwa ndio wanatoa siri kwa polisi na kwa Mkuu wa Wilaya kwa kupeleka majina ya wanaofanya fujo,” amesema.

Magomi ameongeza kuwa: “Katika vurugu hizo walifanya uharibifu wa pikipiki na kuvunja baadhi ya maduka ya wafanyabiashara ambapo Jeshi la Polisi lilifika na kuwakamata waharifu hao.”

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linakemea vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya wananchi wa kata hiyo ya Idukilo na halitasita kuwachukulia hatua za kisheria ambao wataendelea kujihusisha na vitendo hivyo.