Chadema kujifungia siku mbili wakijadili usalama

Muktasari:
- Kikao hicho kitafanyika wakati wameshapanga kufanya maandamano jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 23, 2024 kuishinikiza Serikali kueleza hatua iliyofikia juu ya matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa kwa wananchi na makada wake.
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inatarajia kufanya kikao cha kawaida kitakachofanyika jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na mengine, wajumbe watajikita kujadili hali ya usalama nchini.
Kikao hicho kinakuja wakati tayari chama hicho kimeshapanga kufanya maandamano jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 23, 2024 kuishinikiza Serikali kueleza hatua iliyofikia juu ya matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa kwa wananchi na pamoja na makada wake.
Akizungumzia maazimio ya vikao vya chama hicho Septemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe aliwataka wanachama waliopo mikoani kujiandaa kufika jijini humo kwa ajili ya maandamano hayo.
Hata hivyo, tayari Jeshi la Polisi limeshatangaza kupiga marufuku maandamabo hayo, likisema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa agizo la kufanyika kwa uchunguzi wa suala hilo.
Miongoni mwa makada wa chama hicho waliotoweka na kuuawa ni pamoja na Ali Kibao, aliyechukuliwa ndani ya basi la Tashriff wakati akisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Tanga, Septemba 7, 2024 na kesho yake kukutwa ameuawa eneo la Ununio.
Wengine ambao wametoweka ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise.
Leo Jumatatu Septemba 16, 2024, Chadema imetoa taarifa ikieleza miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa kwenye kikao cha siku mbili, yaani Septemba 17 hadi 18, 2024 ni hali ya usalama wa nchi.
Mbali na usalama wa nchi, kikao hicho pia kinatarajia kufanya usaili na kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Kanda tatu za Pwani, Kusini na Pemba.
Chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa ndani mwisho wa mwaka huu, baada ya kukamilisha chaguzi za ngazi za chini.