Prime
Chadema chaanza vibaya kesi ya mgogoro wa mgawanyo raslimali

Muktasari:
- Wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chama hicho kutoka Zanzibar na makamu mwenyekiti mstaafu wanalalamikia mgawanyo wa raslimali za chama usio sawa kati ya Bara na Zanzibar na upendeleo na ubaguzi. Chadema kiliweka pingamizi kesi itupwe lakini Mahakama imewakatalia.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza vibaya katika kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa raslimali za chama hicho, baada ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi lake dhidi ya kesi hiyo.
Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Zanzibar na wenzake wawili, Ahmed Rashid Khamis Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama hicho kutokea upande wa Zanzibar.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema, akiwa mdaiwa wa pili.
Sambamba na kesi hiyo pia wadai wamefungua maombi ya zuio dhidi ya chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za Chama mpaka kesi yao ya msingi itakapoamuliwa.
Hata hivyo, Chadema kiliweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo, huku kikitoa sababu tisa za kutaka kesi hiyo itupwe bila kusikilizwa madai ya msingi ya wadai.
Katika sababu hizo Chadema kilidai kuwa wadai hawajaonyesha kiwango cha fedha kinachodaiwa, wadai kutokutumia taratibu za ndani ya chama kabla ya kwenda Mahakamani, na viapo vya mdai wa pili na wa tatu kutokuambatanishwa kwenye hati ya madai.
Sababu nyingine walidai kuwa ni wadai kutokuwa na mamlaka ya kumshtaki mdaiwa wa kwanza (Bodi ya Wadhamini) kwa madai kuwa nao ni sehemu ya bodi ya wadhamini.
Vilevile walidai kuwa wadai hawana haki ya kisheria kufungua kesi hiyo mahakamani na wadai hawana mamlaka ya kumshtaki mshitakiwa namba mbili, Katibu Mkuu wa Chadema na mwisho kesi kufunguliwa bila kutaka kifungu cha Sheria kinachoipa Mahakama mamlaka kusikiliza kesi hiyo.
Pingamizi hilo lililosikilizwa kwa njia ya maandishi limetolewa uamuzi leo Jumanne, Juni 10, 2025, ambalo Mahakama imelitupilia mbali.
Jaji Mwanga katika uamuzi wake amechambua sababu mojamoja na hatimaye akahitimisha kuwa pingamizi hilo la Chadema halina mashiko ya kisheria.
"Kwa kuzingatia uchambuzi huo nimejiridhisha kuwa pingamizi hili halina mashiko na kinatupiliwa mbali. Ninaamuru kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa Juni 24, 2025," amesema Jaji Mwanga.
Mbali na kesi hiyo msingi, vilevile chama hicho kimeweka pingamizi dhidi ya shauri la maombi ya zuio la muda, huku kikitoa sababu kama hizohizo kilichozitoa dhidi ya kesi ya msingi.
Waombaji (wadai) nao kwa upande wao wameibua pingamizi la awali dhidi ya kiapo kinzani cha wadaiwa kinachojibu kiapo cha wadai kinachounga mkono maombi hayo ya zuio la muda wameibua hoja tano pamoja na mambo mengine kuhusiana na kasoro za kisheria kwenye kiapo hicho.
Katika amri yake ya mwisho, Jaji Mwanga alielekeza mapingamizi yote, yaani pingamizi la Chadema dhidi ya maombi hayo ya zuio na pingamizi la Wadai dhidi ya kiapo kinzani cha Chadema pamoja na shauri lenye la maombi ya zuio yasikilizwe Juni 10, 2025 kwa mdomo.
Usikilizwaji wa mapingamizi hayo dhidi ya maombi ya zuio la muda pamoja na maombi hayo yenyewe leo ulikuwa unategemea uamuzi wa pingamizi hilo la Chadema dhidi ya kesi ya msingi.
Kama Chadema wangeweza kuishawishi mahakama ikakubalina na pingamizi lao, basi kesi hiyo ya msingi ingetupiliwa mbali na huo ndio ingekuwa mwisho wa kila kitu, kwani hata maombi ya zuio la muda yasingeweza kusimamia.
Lakini kwa uamuzi huo ambao Mahakama imehalalisha kesi ya msingi kuwepo mahakamani, sasa inaendelea na usikilizwaji pingamizi la Chadema dhidi maombi ya zuio, pingamizi la wadai dhidi ya kiapo cha Chadema na maombi yenyewe ya zuio la muda.
Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru mri za kutamka kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.
Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msingi huo, walalamikaji hao wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaiomba Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Amri nyingine wanazoIomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Mbali na amri hizo Vilevile wanaiomba Mahakama iamuru, wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.