Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM kutia mguu kila eneo walilopita Chadema, wakidai kutenganisha maji na mafuta

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema baada ya ziara yake mkoani Morogoro atakwenda kanda ya ziwa ili kuwaambia wananchi yaliyofanywa na Serikali.

Morogoro. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema maeneo yote ambayo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamepita kufanya mikutano nao watapita humohumo.

Makalla alieleza hayo leo Alhamisi Mei 15,2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Kilosa Town ikiwa ni sehemu ya kumalizia kiporo cha ziara yake mkoani Morogoro aliyoisitisha Mei 9, 2025 ili kupisha mazishi ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya.

Kauli ya Makalla imekuja wakati viongozi wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche na Katibu Mkuu wake, John Mnyika wanaendelea na mikutano ya No reforms, no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi katika kanda ya Victoria na Serengeti.

Kanda ya Victoria inaundwa na mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza ambako tayari wamekwishamaliza na sasa wako Serengeti yenye mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga.

"Nimerudi kumalizia kiporo, nilikibakiza baada ya kutokea msiba wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya, nimekuja leo Kilosa kesho Gairo, niwape salamu kwamba tutaanza na kanda ambazo wenzetu wamekwenda hasa mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga,".

"Popote walipopita tutapita kwa sababu tunayo mambo ya kujivunia, ukweli na uongo ni sawa na mafuta na maji, lazima vijitenge. Niseme tu WanaCCM tuendelee kukipigania chama kuna mambo makubwa yamefanyika na tuendelee kuyalinda mafanikio yaliyopatikana kwa wivu," amesema Makalla.

Makalla amefafanua kuwa chama hicho tawala kina mambo ya kuwaeleza wananchi tofauti na wengine.

Amesema changamoto zote zitatatuliwa na CCM kwa sababu ndio chama kilichopewa ridhaa ya kuongoza nchi, hivyo amewataka wananchi wa Kilosa kutokuwa na wasiwasi kuhusu changamoto zao ikiwamo suala la mafuriko.

Kuhusu Kilosa, Makalla amesema imebadilika kutokana na maendeleo yaliyofanyika katika sekta za afya, elimu, nishati na miundombinu ya barabara, reli na madaraja.

"Kuona ni kuamini watu walizoea kupanda mabasi kwenda Dar es Salaam au Dodoma, leo unatumia muda mchache kutoka Dar es Salaam hadi Kilosa haya ni maendeleo. Kulikuwa na shida ya umeme sasa hivi vijiji 82 vimefikiwa bado kuusambaza kwenye vitongoji," amesema Makalla.


Agusia hamahama makada wa Chadema

Katika mkutano huo, Makalla amedai Chadema inapitia wakati mgumu kutokana na wimbi la hamahama la makada na viongozi waandamizi wa chama hicho, wanaotimka kila kukicha kutafuta jukwaa jingine la kuendeleza harakati za siasa.

"Leo nimesikia mjumbe wa kamati kuu ( Devotha Minja aliyekuwa pia mwenyekiti wa Chadema kanda ya kati), jana sijui ilikuwa viongozi wa Kinondoni, kila kona wanahama,"

"Mwambie jirani yako adui muombee njaa, tuliwaambia kwamba kuna mgogoro wakakataa leo wanakwenda kusambaratika, watu wanahama kila kukicha sijui viongozi wa mikoa mara kanda," amedai Makalla.

Mei 9, 2025 Naibu Katibu wa Chadema (Bara), Amani Golugwa alisema chama hicho hakina muda wa kulumbana kwa sasa badala yake kinajijenga upya na wanaoondoka wanawatakia kila la kheri wanakoenda na wanatambua mchango wao walipokuwa ndani ya chama hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema wilaya hiyo, imepiga hatua za maendeleo hasa katika sekta za mifugo na kilimo ambapo Serikali imewekeza fedha nyingi ili kuiboresha.

Mbali na hilo, Shaka amesema changamoto za migogoro kati ya wakulima na wafugaji zilizokuwa zikisababisha mauaji zimepungua tofauti na miaka iliyopita.

" Hapo nyuma sifa kubwa ya Kilosa ni migogoro, mapigano na mauaji ya wakulima na wafugaji, leo hii sifa ya wilaya hii ni kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na miongozo yake ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji na makundi haya kuyaweka pamoja," amesema Shaka.

Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ndani ya miaka minne jimbo hilo limepiga hatua za maendeleo zilizotatua changamoto za miundombinu ya barabara, madaraja sambamba na uboreshaji wa upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote 82.