CCM: Hatutaangalia cheo wala umaarufu kwa wazembe
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, akizungumza nje ya Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, leo Ijumaa Mei 29, 2026.
Muktasari:
- Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, ameanza ziara yake mkoani Kilimanjaro akisisitiza kuwa chama hakitavumilia mtumishi yeyote wa chama na serikali atakayekwamisha utekelezaji wa miradi.
Siha. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitamvumilia mtumishi wake au wa Serikali yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika utekelezaji wa hilo, kimesema hakitaangalia cheo cha mtu, umaarufu wake wala umri, wote watachukuliwa hatua kulingana na kiwango cha makosa yao.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Mei 29, 2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi wakati wa ziara yake katika Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema CCM imeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika hospitali hiyo, akieleza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Amesema tangu mwaka 2023, zaidi ya Sh38 bilioni zimewekezwa katika hospitali hiyo, zikiwamo Sh22.5 bilioni zilizotumika kujenga maabara ya kisasa na ununuzi wa vifaa tiba na ujenzi wa jengo la utawala ambalo bado linaendelea kukamilishwa.
“Katika utekelezaji wa ilani tumeridhika kwa asilimia 100. Huduma zinazotolewa hapa ni nzuri na wananchi wanapata huduma bora. Lakini endapo kutakuwa na mtu anayekwamisha utekelezaji wa ilani, wananchi watatuhukumu na sisi kama chama hatutakubali hali hiyo,” amesema Kihongosi.
Amesisitiza kuwa kila mtumishi wa chama au Serikali anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu na kuwahudumia wananchi ipasavyo.
“Mtumishi yeyote wa chama au Serikali atakayekwamisha juhudi za Serikali katika kuwapelekea wananchi huduma bora tutachukua hatua bila kuangalia umaarufu, umri wala cheo. Kila mmoja lazima asimame kwenye nafasi yake na kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania,” amesema.
Katika ziara hiyo, Kihongosi amepongeza Serikali kwa maboresho yaliyofanyika hospitalini hapo, akisema yamepunguza gharama kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za muda mrefu.
Amesema hapo awali wagonjwa waliokuwa wanatumia oksijeni walilazimika kulipa zaidi ya Sh35,000 kwa mtungi mmoja, lakini sasa wanachangia Sh5,000 pekee huku wakiendelea kupata huduma bora.
“Kwa kweli Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana hapa. Tumeshuhudia wagonjwa wanaotumia oksijeni kwa muda mrefu wakipata huduma kwa gharama nafuu zaidi tofauti na zamani,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi wa Siha kulinda miundombinu ya hospitali hiyo kwa kuwa imegharimu fedha nyingi za Serikali na inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Tuilinde miundombinu ya Serikali. Serikali imewekeza fedha nyingi ili wananchi msitoke hapa kwenda Muhimbili au KCMC kutafuta huduma. Huduma zote zipatikane hapa Siha,” amesema.
Kihongosi, amesema Hospitali ya Kibong’oto ina historia kubwa nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1926 na kwamba mwaka huu inatimiza miaka 100 ikiwa imeendelea kutoa huduma muhimu kwa jamii.
Awali, Meneja wa Maabara ya Afya ya Jamii Kibong’oto, Shaban Mziray, amesema maabara hiyo ilianza kutumika mwaka 2023 na imekuwa na mchango katika ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko pamoja na tafiti mbalimbali za afya.
Amesema miongoni mwa kazi zinazofanyika ni kufuatilia usugu wa vimelea dhidi ya dawa, kubaini magonjwa ya kuambukiza katika jamii yakiwamo kifua kikuu cha kawaida na kifua kikuu sugu, pamoja na kufanya tafiti za kimkakati za kuboresha tiba.
“Tumehusika katika tafiti zilizosaidia kupunguza muda wa matibabu ya kifua kikuu sugu kutoka zaidi ya miezi 20 hadi miezi sita,” amesema.
Mziray, amesema maabara hiyo yenye ukubwa wa nusu hekari ni miongoni mwa maabara kubwa zaidi nchini kwa kiwango cha uwekezaji na ina uwezo mkubwa wa kuhifadhi sampuli kwa muda mrefu.
“Hapa tuna benki ya sampuli yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita 47,000 za sampuli kwa ajili ya tafiti na ufuatiliaji wa magonjwa kwa zaidi ya miaka 50,” amesema.