Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM kufuatilia mradi wa maji unaosuasua Bunda

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kenani Kihongosi, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Bunda ikiwa ni sehemu ya mwisho ya zaira yake mkoani Mara

Muktasari:

  • Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni ambapo ukikamilika utahudumia watu zaidi ya 51,000, ulianza kutekelezwa Aprili 2025 na ulitarajiwa kukamilika Januari 2026.

Bunda. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha fedha za utekelezaji wa mradi wa maji safi Nyamuswa, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, zinatolewa ili mradi huo uweze kukamilika baada ya kushindwa kukamilika kwa wakati.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni ulitarajiwa kukamilika Januari 2026, lakini hadi sasa haujakamilika sababu ikielezwa kuwa ni kuchelewa kwa fedha za malipo kwa mkadarasi anayetekeleza mradi.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, leo Jumapili 17, 2026, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amesema ili kufikia dhamira ya chama hicho ya kumtua mama ndoo kichwani, ni lazima miradi ya maji itekelezwe na kukamilika.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kenani Kihongosi, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Bunda ikiwa ni sehemu ya mwisho ya zaira yake mkoani Mara

“Mama Samia ana dhamira ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani na hilo litawezekana miradi ya maji kama huu wa Nyamuswa ikitekelezwa na kukamilika, hivyo niwaahidi nakwenda kukutana na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na watu wake kwani najua hili halimshindi,” amesema.

Amesema Serikali ina dhamira njema ya kutekeleza miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa CCM kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (Buwssa),Esther Gilyoma amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili 2025 na ulitarajiwa kukamilika Januari 2026.

Gilyoma amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya jitihada ya mamlaka yake katika kufikia lengo la kusambaza maji safi na salama kwa wakazi wa mji wa Bunda ambapo hivi sasa upatikanaji wa huduma hiyo katika eneo hilo ni asilimia 87.

Amefafanua kuwa mradi wa maji Nyamuswa ukikamilika utatoa huduma kwa watu zaidi ya 51,000 katika kata ya Nyamuswa na mji wa Bunda.

Amesema kutokana na ucheleweshaji wa fedha, mkandarasi wa mradi huo aliomba kuongezewa muda ambapo uliongezwa hadi Juni 2026 lakini kutokana na maendeleo ya mradi kuna uwezekano wa mradi huo kutokukamilika ndani ya muda huo wa nyongeza.

“Hadi sasa mradi umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake na mkandarasi amekwishalipwa Sh2 bilioni na anadai Sh2.5 bilioni kulingana na kazi ambayo amefanya,” amesema.

Baadhi ya wananchi wakiwa katika ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kenani Kihongosi, mjini Bunda ikiwa ni sehemu ya mwisho ya zaira yake mkoani Mara

Ameomba Serikali kuharakisha upatikanaji wa fedha ili mradi huo uweze kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo imekusudiwa.

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Nyamuswa wameomba mradi huo ukamilike kwa wakati ili waweze kuwa na chanzo cha uhakika cha maji safi na salama tofauti na sasa ambapo wanatumia maji yasiyokuwa salama kwao.

“Mbali na kuwa maji sio salama lakini pia kuyapata ni kazi kubwa hasa kipindi cha kiangazi, lakini huu mradi ukikamilika, changamoto hiyo itakuwa ni historia,” amesema Anna Nyamseba.

Joyce Martin amesema ili miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali iweze kukamilika kwa wakati ni vema kuwe na ziara za mara kwa kara za viongozi wa CCM kubaini changamoto za miradi hiyo ili ifanyiwe kazi.