Wananchi wataka utaratibu mpya mikopo ya halmashauri
Baadhi ya wananchi wakihudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika eneo la Nyamwaga, wilayani Tarime, na kuhutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi.
Muktasari:
- Mikopo hiyo hutolewa kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji.
Mara. Wakazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara wameiomba Serikali kuboresha utaratibu wa utoaji wa mikopo isiyo na riba inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, wakisema masharti yaliyopo yanawanyima wengi fursa ya kunufaika.
Wananchi hao walitoa maoni hayo Mei 16, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Nyamwaga wilayani Tarime na kuhutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi, Kenani Kihongosi.
Mikopo hiyo hutolewa kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji.
Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Sirari, Juma Chacha amesema licha ya maboresho yaliyofanyika katika utoaji wa mikopo hiyo, bado wananchi wengi wanashindwa kuifikia kutokana na masharti mengi, hususan hitaji la kuunda vikundi.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Nyamwaga, wilayani Tarime.
Amesema wananchi wengi wanaishia kukimbilia mikopo ya riba kubwa maarufu kama “kausha damu” kwa kuwa upatikanaji wake ni rahisi ukilinganisha na mikopo ya halmashauri.
“Watu wengi bado wanateseka na mikopo ya kausha damu kwa sababu kule hakuna masharti mengi. Huku halmashauri kuna mlolongo mrefu na taratibu nyingi, hivyo wengine wanaamua kwenda kwenye mikopo hiyo ya riba kubwa,” amesema Chacha.
Ameishauri Serikali kuruhusu wananchi kupata mikopo hiyo mmoja mmoja badala ya mfumo wa sasa unaotaka vikundi vya watu wasiopungua watano, akisema matumizi ya vitambulisho vya Taifa yanaweza kusaidia kurahisisha mfumo huo.
Naye mkazi mwingine, Rhobi Michael amesema wanawake wengi wenye biashara ndogo wanashindwa kunufaika kwa sababu ya masharti ya mikopo kutolewa kwa vikundi badala ya mtu mmoja mmoja.
“Kuna wanawake wana biashara zao binafsi lakini wanashindwa kupata mikopo kwa sababu ya masharti ya vikundi. Serikali iliangalie uwezekano wa kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja au vikundi,” amesema Rhobi.
Baadhi ya wananchi wakihudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika eneo la Nyamwaga, wilayani Tarime, na kuhutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita halmashauri mbili za wilaya hiyo zimetoa zaidi ya Sh8 bilioni kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa makundi maalumu.
Amesema mbali na mikopo hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani ya halmashauri, hali iliyochangia kuboresha huduma za kijamii katika wilaya hiyo.
“Miradi mingi imetekelezwa na mikopo kwa makundi mbalimbali imetolewa kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi na kuwasaidia kujitegemea,” amesema.
Akijibu hoja za wananchi, Kihongosi amesema amepokea maoni hayo na ataifikisha Serikali ili yafanyiwe kazi.
Amesema ilani ya uchaguzi ya CCM imeweka mkazo katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo mikopo kwa makundi maalum.
Kihongosi amesema Serikali imeendelea kupeleka fedha nyingi za maendeleo wilayani Tarime, hatua ambayo imechangia kuboresha sekta mbalimbali za huduma kwa wananchi.
“Leo nimekagua shule mpya ya sekondari iliyojengwa kwa zaidi ya Sh1.6 bilioni. Hii inaonyesha dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kujali eneo walipo,” amesema.
Ameongeza kuwa wilaya hiyo imepokea zaidi ya Sh60 bilioni katika kipindi cha miaka minne iliyopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi imara wa familia na taifa kwa ujumla.