Ludewa yatenga Sh130 milioni kila kata mikopo ufugaji wa Samaki
Muktasari:
- Serikali kupitia wizara inayosimamia masuala ya vijana imetenga fedha hizo kwa kila kata ndani ya halmashauri hiyo, kwa lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, hususan ufugaji wa samaki.
Njombe. Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imetenga Sh130 milioni kwa kila kata ili kuwawezesha wananchi kupata mikopo kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika baada ya ziara yake katika kata tano za Lupingu, Lifuma, Makonde, Kilondo na Lumbila.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha wananchi kutumia fursa za mikopo kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa vizimba, ili kujikwamua kiuchumi na kuleta maendeleo katika jamii.
Kwa mujibu wa Thomas, Serikali kupitia wizara inayosimamia masuala ya vijana imetenga fedha hizo kwa kila kata ndani ya halmashauri hiyo, kwa lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, hususan ufugaji wa samaki.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas akizungumza na wananchi wa kata za Mwambao wa ziwa Nyasa huko wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Amesema huu ni wakati muafaka kwa vijana kutumia fursa hiyo, kwa sababu ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba umeonesha kuwa na tija kubwa, hasa kwa wakazi wa maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa.
Aidha, amefafanua kuwa ili kufaidika na mikopo hiyo, vijana wanapaswa kuunda vikundi vyenye wanachama wasiopungua watano, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35, na kuwasilisha maombi yao kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
“Serikali imeleta fedha hizi kwa ajili yenu, ni wajibu wenu kuziomba na kuzitumia ipasavyo ili ziweze kuwaletea maendeleo,” amesema Thomas.
Pia, amewataka wataalamu kutoka halmashauri hiyo pamoja na ofisi yake kuhakikisha wanasogeza huduma muhimu karibu na wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hiyo.
Baadhi ya huduma alizozitaja ni pamoja na usajili wa vitambulisho vya Taifa (Nida) na utoaji wa mafunzo ya namna bora ya kuandaa maombi ya mikopo.
Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas, katika kata za Mwambao wilayani Ludewa.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Mwambao wamepokea kwa furaha mpango huo, wakisema utasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuinua kipato cha kaya nyingi kupitia sekta ya uvuvi.
Miongoni mwao, Anna Ngoe ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo wa mikopo, akieleza kuwa utakuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi.
Hata hivyo, ameomba Serikali kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa samaki watakaozalishwa ili kuwahakikishia wakulima hao faida endelevu.
“Tunaomba Serikali ituhakikishie soko la uhakika pindi tutakapoanza uzalishaji wa samaki,” amesema Ngoe