Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yaonya siasa kuingizwa kwenye miradi ya maendeleo

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyasaricho wilayani Tarime shule ambayo imejengwa kwa zaidi ya Sh1.6 bilioni

Muktasari:

  • Yasema miundombinu ya miradi ya maendeleo inapaswa kulindwa na wananchi wote, badala ya kuhujumiwa au kuharibiwa kutokana na ushawishi wa baadhi ya wanasiasa.

Mara. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanasiasa nchini kufanya siasa za kistaarabu bila kuathiri miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, kikisisitiza kuwa miundombinu yote ya umma inalenga kunufaisha wananchi na si maslahi ya kisiasa.

Wito huo umetolewa leo, Mei 16, 2026 wilayani Tarime na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Kenani Kihongosi, baada ya kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari Nyasaricho, uligharimu zaidi ya Sh1.6 bilioni.

Kihongosi amesema miundombinu ya miradi ya maendeleo inapaswa kulindwa na wananchi wote, badala ya kuhujumiwa au kuharibiwa kutokana na ushawishi wa baadhi ya wanasiasa.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kenani Kihongosi akizungumza baada ya kukagu shule ya Sekondari ya Nyasaricho iliyojengwa kwa zaidibya Sh1.6 bilioni.

“Siasa isiingie kwenye maendeleo. Tuache miradi iendelee kwa faida ya wananchi, hasa wa kipato cha chini. Kuharibu miundombinu ni kuwanyima haki wananchi wasio na hatia,” amesema Kihongosi.

Amesema ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya wanasiasa wakihamasisha uharibifu wa miradi ya Serikali, ikiwemo uchomaji wa miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa ili kuhudumia wananchi.

Kihongosi amesema kuingiza siasa kwenye miradi ya maendeleo kunasababisha wananchi kukosa huduma muhimu zilizokusudiwa kuboresha maisha yao katika sekta mbalimbali.

Amesema CCM itaendelea kushughulikia changamoto za wananchi, akisema ndicho chama chenye dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maisha bora.

Katika hatua nyingine, amewataka wanachama wa CCM wilayani Tarime kuvunja makundi ndani ya chama, akisema umoja na mshikamano ni nguzo muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.

“Makundi yavunjwe. Tunahitaji umoja, upendo na mshikamano. Kiongozi yeyote asibebe mtu kuliko chama,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akikagua maabara katika shule ya Sekondari Nyasaricho wilayani Tarime.

Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa shule hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simon Shati, amesema Sh1.6 bilioni zilizotumika zimetokana na Serikali Kuu na mapato ya ndani ya halmashauri.

Amesema Sh1 bilioni ilitolewa na Serikali Kuu, huku Sh600 milioni zikichangiwa na halmashauri, na kwamba shule hiyo tayari imeanza kutoa huduma kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita.

Shati ameongeza kuwa halmashauri imepanga katika bajeti ya mwaka huu kukamilisha ujenzi wa maabara ya fizikia ili kukamilisha miundombinu ya maabara tatu za sayansi shuleni hapo.