Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BARAZA LA SALIM: Abel da Silva ana haki ya kuenziwa

Katika miaka ya hivi karibuni, hasa kuanzia karne ya 21, mandhari ya miji ya Unguja na Pemba pamoja na maeneo jirani yamebadilika kwa kasi kubwa.

Hali hii imesababishwa na ujenzi wa majengo ya kuvutia, ikiwemo ya ghorofa kwa ajili ya ofisi, biashara na makazi.

Miongoni mwa maendeleo haya ni kufunguliwa kwa kituo cha kisasa cha ukaguzi wa magari kilichopo Dole, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Kituo hiki ni mradi wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), ambao umegharimu takriban Sh2.8 bilioni.

Ni hatua kubwa ya maendeleo, lakini pia ni ushahidi wa busara ya uongozi wa ZBS na serikali kwa jumla, kwa kuamua kukipa kituo hiki jina la "Kwa Silva."

Kituo hiki, ambacho kilizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi miezi miwili iliyopita, kimekusudiwa kuhakikisha usalama wa magari barabarani, kwa madereva, abiria, watumiaji wa vyombo vingine na watembea kwa miguu.

Kina mashine mbili za kisasa pamoja na vifaa vinavyoweza kukagua hadi magari 300 kwa siku, na kinatarajiwa kufanya kazi saa 24 kwa siku.

Hatua hii itaondoa usumbufu wa kusubiri kwa muda mrefu, wakati mwingine hata wiki nzima, ili kukagua gari na kupata kibali cha kulitumia barabarani.

Kwa mtu asiyeifahamu historia ya Zanzibar, huenda asielewe sababu ya kituo hiki kupewa jina la Silva.

Hata hivyo, huu ulikuwa ni uamuzi sahihi na wenye busara. Abel da Silva, ambaye aliaga dunia karibu miaka 10 iliyopita, alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na mchango wake katika sekta ya usafiri Zanzibar, akiendeleza urithi wa familia yake.

Silva alikuwa miongoni mwa Wazanzibari wenye asili ya Goa, jimbo dogo la India lililo upande wa magharibi, eneo la Konkan, pembeni mwa Bahari ya Arabia.

Watu wa Goa, licha ya kuwa na asili ya India, wameathiriwa zaidi na utamaduni wa Kireno, hasa kwenye mavazi, majina na mitindo ya maisha, lakini si sana kwenye vyakula.

Watu wa asili ya Goa walifika Zanzibar zaidi ya miaka 500 iliyopita wakihusika na biashara, elimu, ufundi wa kuchonga, kushona nguo na kazi nyingine.

Kikundi maalumu chenye historia ya kipekee kilifika mwaka 1857, kikiongozwa na baharia wa Jeshi la Uingereza, Richard Francis Burton na kundi la zaidi ya watu 200. Kikundi hicho kilitembelea pia Mombasa, Tanga, Pangani na baadaye Tanganyika.

Kabla ya Mapinduzi ya 1964, kulikuwepo takriban watu 3,500 wa asili ya Goa Zanzibar. Hata hivyo, wengi wao walihamia Uingereza, India au Tanzania Bara baada ya Mapinduzi, na waliobaki waliendelea kufanya kazi kama walimu, mafundi, wapiga picha, wanasheria na kadhalika.

Miongoni mwa familia zilizobaki ni ile ya Wolfango Dourado, mwanasheria mkuu wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na familia ya Silva, aliyekuwa fundi magari.

Abel da Silva alifanya kazi kama mkuu wa kitengo cha ukaguzi wa magari Zanzibar kwa zaidi ya miaka 30 kwa uadilifu mkubwa. Alijulikana kwa msimamo wake mkali dhidi ya uzembe, hata alipokagua magari ya viongozi wa Serikali.

Kutambuliwa kwa mchango wake kupitia kupewa jina la kituo hiki cha ukaguzi ni heshima stahiki.

Ni ishara ya kutambua umuhimu wa watu waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii.

Ninaleta hoja hii ili kukumbusha kuwa historia ya Zanzibar imejaa watu mashuhuri waliochangia katika nyanja mbalimbali, lakini majina yao yameanza kusahaulika.

Wapo viongozi wa dini walioweka msingi wa maadili na elimu; madaktari na walimu wazalendo waliotambulika Afrika Mashariki, India na nchi za Ghuba; wasanii, wanamichezo na wataalamu katika nyanja mbalimbali. Kwa masikitiko, majina yao yamepotea kama moshi hewani.

Kwa sasa, jina la karibu kila barabara, shule, soko au chuo jipya ni la mwanasiasa. Hali hii inahitaji kubadilika.

Ni wakati wa kuenzi mchango wa watu walioweka msingi wa maendeleo ya kweli ya Zanzibar, si kwa maneno pekee, bali kwa vitendo kama ilivyofanywa kwa Abel da Silva.

Nchi haijengwi na wanasiasa pekee. Tunahitaji historia yetu iandikwe upya kwa haki na usawa.