ACT-Wazalendo yatoa hoja sita kwa Serikali kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo,Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita akizungumza na wanachama wa chama hicho mkoani Kigoma kwenye Kongamano la Tatu la Linda Demokrasia lilozinduliwa kwa mara ya kwanza Mkoani Lindi na Kiongozi Mstaafu wa Chama hicho, Zitto Kabwe.
Muktasari:
- ACT-Wazalendo yaja na hoja sita zinazoitaka serikali kuzitekeleza kabla ya kuingia kwenye uchaguzi Mkuu 2025.
Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimewasilisha hoja sita zinazopendekeza hatua ambazo Serikali inapaswa kuzitekeleza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hoja hizo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia.

Akizungumza katika Kongamano la Tatu la operesheni linda demokrasia lililofanyika mkoani Kigoma leo, Aprili 6, 2025, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, amesisitiza umuhimu wa wajumbe wa sasa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kujiuzulu ili wateuliwe wapya kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Mchinjita ametaja kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya utaimarisha imani miongoni mwa wadau wa uchaguzi.
Mchinjita pia amesisitiza kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuepuka ushiriki katika hujuma zozote zinazohusiana na uchaguzi, na kuongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri wasipaswe kuwa wasimamizi wa uchaguzi ili kuepuka migongano ya kimasilahi. Aidha, ameweka wazi kuwa chama hicho kinataka hatua madhubuti zichukuliwe ili kudhibiti kura feki katika michakato ya uchaguzi.

Katika mkutano huo, amesisitiza kuwa mawakala wa vyama wanapaswa kuwa huru katika kufanya kazi zao kwenye vituo vya kupigia kura bila kushurutishwa, na wagombea wasiondolewe kwa misingi ya kisiasa.
Hata hivyo, mwezi uliopita, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, alisisitiza kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki, akieleza dhamira ya CCM kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa wa haki na usio na upendeleo. Wasira alisema kuwa mabadiliko makubwa ya sheria yanapendekezwa ili wasimamizi wa uchaguzi kuwa maofisa waandamizi wa umma badala ya viongozi wa kisiasa.
Mchinjita ameongeza kuwa baadhi ya mambo hayawezi kutekelezwa kwa mabadiliko ya sheria pekee, bali unahitaji utekelezaji wa taratibu zilizopo.
“Tunataka kuwa na uwazi na ushirikishaji katika mchakato mzima wa uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa karatasi za kupigia kura,” amesisitiza Mchinjita. Pia, amekumbusha wajibu wa Serikali katika kuhakikisha mawakala wanapata haki yao ya kuwepo na kuwakilisha masilahi ya wagombea katika vituo vya kupigia kura.