Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo sasa kupigania mageuzi mifumo ya uchaguzi


Muktasari:

  • Lengo kubwa kwenye operesheni hiyo ni kuhakikisha ACT Wazalendo inarejesha thamani ya kura kwa Watanzania na kwamba, itafika kila mkoa.

Lindi. Vuguvugu la mageuzi ya mifumo ya uchaguzi ikiwemo sheria na kanuni za uendeshaji limezidi kupamba moto. Tayari, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiendelea na kampeni yake ya No reforms, no election katika maeneo mbalimbali nchini, leo ACT Wazalendo imezindua operesheni yake.

Operesheni ya ACT Wazalendo inayokwenda kwa jina la Operesheni Linda Demokrasia inalenga kupigania mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na kurejesha thamani ya kura ya kila Mtanzania kwenye uchaguzi.

Uzinduzi wa operesheni hiyo umefanywa na Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano lililofanyika katika Jimbo la Lindi Mjini, leo Machi 29, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma, Shangwe Ayo, Zitto amesema operesheni hiyo ina lengo la kurudisha thamani ya kura kwa Mtanzania.

Zitto amesema kuwa amelaani ukiukwaji wa sheria na misingi ya haki katika chaguzi tatu zilizopita.

“Katika chaguzi tatu mfululizo thamani ya kura imepotea. Uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2019 hakukuwa na kura, takribani wagombea wote wa upinzani walienguliwa. Mwaka 2020 tuliona kwa mara ya kwanza kura feki zikozagaa hovyo. Mwaka 2024 wakafanya kama mwaka 2020,” amesema Zitto.

Zitto amesisitiza kuwa hoja kuu ya “Operesheni Linda Demokrasia” ni mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.

“Tume ya Uchaguzi yenye wajumbe kama Omari Mapuri, ambaye amewahi kuwa Mwenezi wa CCM inawezaje kutenda haki kwa watu wote? Sheria ya sasa ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeweka utaratibu kuwa angalau wajumbe wake wapatikane kwa ushindani. Watu waombe na wafanyiwe usaili. Serikali ya CCM haitaki kutekeleza jambo ambalo wamelitunga wenyewe,” amesema Zitto kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Zitto amesema kutokana na kuvurugwa kwa demokrasia nchini, matokeo yake ni kuporomoka kwa uzalendo miongoni mwa wananchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo- Bara, Isihaka Mchinjita amewahimiza wananchi kupambana kuhakikisha kuwa misingi ya demokrasia nchini inarejeshwa.

“Kulinda demokrasia ni wajibu namba moja wa raia. Raia wanapokosa uhuru wa kuamua nani awe kiongozi wao, wanakuwa watumwa ndani ya nchi yao,” amesisitiza Mchinjita, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

ACT Wazalendo kinaendelea na programu mbalimbali za Operesheni Linda Demokrasia ikiwemo makongamano ya kufafanua dhana hiyo kwenye mikoa mbalimbali na ziara kwa wadau mbalimbali wa demokrasia.