Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo yaja na mambo sita kuhusu mikopo kwa vijana

Muktasari:

  • Aprili 29, 2026, Wizara ya Maendeleo ya Vijana kupitia taarifa yake kwa umma ilieleza kuwa itatoa mafunzo kwa vijana baada ya kubaini dosari katika uandishi wa miradi, lengo likiwa kuhakikisha vijana wanakuwa na uelewa mpana juu ya masuala ya mikopo.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimetoa mapendekezo sita kwa Serikali yatakayowezesha vijana kunufaika na mikopo, ikiwemo kuondolewa kwa kigezo cha leseni ya biashara kwa vijana wanaoanza biashara kuomba mkopo.

Mbali na hayo, chama hicho kimeelezea njia mbili zinazoweza kuchukuliwa na Serikali kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta ili kuleta ahueni ya maisha kwa wananchi.

Msimamo huo wa ACT Wazalendo umetolewa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2026, ajenda kuu ikiwa ni suala la mikopo kwa vijana na changamoto wanazopitia.

Nondo amesema mikopo ya Sh200 bilioni iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Vijana ni sehemu ya maigizo katika suala la uwezeshaji wa vijana kiuchumi na utoaji wa mikopo.

"Wizara na Serikali walitazame kundi la vijana kwa jicho la ukweli, uwazi na dhamira ya dhati katika kushughulikia masuala yao. Awali vijana walikuwa na matumaini na matarajio makubwa kuhusu mikopo hii ya bilioni 200, lakini sasa vijana wameanza kupoteza matumaini na matarajio," amesema.

Hata hivyo, Serikali kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Vijana Aprili 29, 2026, ilieleza mikakati inayochukuliwa, ikiwemo kuanza utoaji wa mafunzo kwa vijana baada ya kubaini mapungufu kwenye uandishi wa miradi ya uombaji wa mikopo hiyo.

Mwenyekiti ya Ngombe ya Vijana Taifa ACT - Wazalendo, Abdul Nondo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Kulingana na wizara hiyo, awamu ya kwanza ya utoaji wa mikopo hiyo iliwanufaisha vijana 1,961 waliomba mikopo kupitia Mfuko wa Vijana, ndiyo maana wakaona umuhimu wa kuanza kutoa mafunzo kwa vijana, mpango utakaoanza Mei mwaka huu.


ACT Wazalendo na mapendekezo

Nondo, katika pendekezo lake la tatu, ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana ifungue haraka dirisha la pili la maombi ya mkopo ili vijana wote ambao hawakupata mkopo waombe na wapewe.

"Tunaitaka Serikali itoe mikopo na kuweka wazi sababu halisi za vijana wote kukosa mkopo. Itaje sababu za kukosa mkopo kwa kila kijana, na kama kuna kasoro kijana apewe nafasi ya kurekebisha taarifa zake na mchakato uendelee.

"Haipaswi kuishia kusema wamekosea. Haiwezekani vijana 78 tu waliopata mkopo ndiyo wamepatia, ilhali vijana 30,306 kati ya 30,384 wamekosea kuandika andiko," amesema.

Pendekezo lingine, Nondo ameitaka Serikali kurejesha fedha zote za Sh200 bilioni zinazohusu vijana zilizopelekwa wizara za kisekta, zirejeshwe kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuutunisha mfuko huo kwa lengo la kunufaisha vijana wengi zaidi.

Ikumbukwe Aprili 26, 2026, visiwani Zanzibar, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa mgeni rasmi katika kongamano la kufunga mafunzo ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) lililoandaliwa na UVCCM na kufanyika Tunguu, aliweka msimamo katika hilo.

Rais Samia amesema pendekezo la kuunganisha mifuko yote ya uwezeshaji wa vijana kuwa chini ya wizara moja haliwezekani, akieleza kuwa kila sekta ina majukumu na mipango yake maalumu kwa vijana.

Hata hivyo, ameahidi jambo linaloweza kufanywa na Serikali ni kuongeza fedha katika mifuko hiyo ili kuwafikia vijana wengi zaidi na si kupunguza kama wanavyopendekeza baadhi ya wadau.

Pendekezo lingine la ACT Wazalendo ni kuitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana kuweka wazi orodha halisi ya vijana waliopata mkopo kutoka kwenye orodha ya walioomba, pamoja na kiasi cha fedha kwa kila aliyekopeshwa, ili kusaidia uwazi, tathmini na uwajibikaji.

Kuhusu mafuta

Katika eneo la bei ya mafuta, Nondo amesema kupanda kwa bei ya mafuta kufikia Sh4,200 kwa lita kunaongeza gharama za maisha.

"Waathirika wa hili ni Watanzania wengi wa kipato cha chini. Nauli zimepanda, gharama za usafiri zimepanda, hivyo kuathiri pia bei za vyakula na kuongeza mfumuko wa bei za bidhaa. Serikali ichukue hatua za haraka," amesema na kuongeza:

"Ngome ya Vijana ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza msimamo wa chama kwamba Serikali ichangie gharama pamoja na mwananchi. Kwa kila lita moja ya mafuta, Serikali ichangie angalau Sh400 kama ruzuku ili kupunguza makali ya bei," amesema.

Jambo lingine, Nondo amesema tozo kwenye mafuta ya petroli na dizeli kwa lita moja ni takribani Sh1,113, akishauri Serikali iondoe baadhi ya kodi na tozo kwenye bidhaa hizo.

Amesema kodi na tozo hizo zina thamani ya Sh500 katika kila lita moja ya mafuta, na lengo la kuziondoa ni kupunguza ukali wa bei na hivyo kusaidia kupunguza kupaa kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei za bidhaa.

Ilichofanya Serikali kwenye mafuta

Hivi karibuni Serikali ilitangaza kutoa ruzuku ya Sh259 kwa kila lita ya dizeli katika jitihada za kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta.

Kwa mujibu wa bei mpya za mwezi Mei 2026 zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), katika jiji la Dar es Salaam, petroli inauzwa kwa Sh4,115 kwa lita.

Bei ya dizeli pia imefikia Sh4,248 kwa lita huku mafuta ya taa yakipanda hadi Sh4,677 kwa lita, hali inayoonyesha kuendelea kwa mwenendo wa kupanda kwa gharama za nishati nchini.

Ruzuku hiyo ya dizeli inalenga kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika licha ya changamoto za kimataifa.